Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Simba, Yanga wanapokuwa wenyeji ugenini

Simba SC 1140x640 Wekundu wa Msimbazi

Tue, 1 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Katika miaka ya hivi karibuni nguvu ya klabu za Simba na Yanga inazidi kuwa kubwa, huku klabu nyingine zinazoshindana nazo zikionyesha nguvu yake ndani ya dakika tisini tu.

Hivi sasa Yanga na Simba kwenda hata Morogoro ni kitu kikubwa kama vile kwenda Nigeria au Cameroon kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa wa Afrika au Kombe la CAF.

Ni kama vile klabu nyingine 14 zinazoshindana nazo kwenye Ligi Kuu hazina shabiki hata mmoja zaidi ya kutegemea mashabiki wa moja ya timu hizo kuwashangilia wanapocheza na moja ya klabu hizo kongwe.

Hata Coastal Union ambayo ina historia ya muda mrefu katika soka nchini, bado inahaha kuwa na mashabiki wake yenyewe, hali kadhalika Mtibwa Sugar, Kagera na hata Azam ambazo zina muda wa kutosha kwenye soka nchini.

Nini kinasababisha klabu hizo kutokuwa na mashabiki wafia timu licha ya kuwa na muda mrefu kwenye soka?

Ni kweli kwamba Yanga na Simba zina historia kubwa si tu kwenye soka nchini, bali hata kwenye katika historia ya nchi hivyo si ajabu kwao kuvuna mashabiki kiasilia bila ya hata kutumia nguvu kubwa.

Pengine tatizo kwao ni kutumia mtaji mkubwa wa mashabiki wao kugeuza kuwa fedha. Bado hazina vyanzo vizuri vya mapato vitokanavyo na uwingi wa mashabiki wao.

Lakini nimeona katika siku za karibuni Yanga ikianzisha kitengo cha ushirikishaji mashabiki (fans engagement), ambacho kwanza kilikuwa kinaongozwa na Antonio Nugaz na sasa kimewekwa chini ya Haji Manara.

Pengine ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa propaganda ndio maana amepewa kitengo hicho pamoja na kile cha habari, lakini sidhani kama kimetengenezewa vipimo vya ufanisi wake.

Ni vigumu kwa klabu kujiendesha bila ya kuwa na mashabiki wake kindakindaki. Na ni ajabu kwa klabu kuwepo mchezoni kwa zaidi ya miaka kumi lakini haijajenga wigo mpana wa mashabiki kiasi kwamba hata inapocheza mechi za nyumbani dhidi ya timu kama Simba au Yanga, ndio kwanza inaonekana iko ugenini.

Hili ni jambo ambalo haliji kwa bahati tu kama inavyodhaniwa kwa Simba na Yanga, bali kwa mipango ya kisayansi. Watafiti wanasema moja ya mambo yanayoweza kugeuza mashabiki kuwa kindakindaki ni ushindi wa uwanjani.

Ni lazima kwanza klabu iwe na matokeo mazuri uwanjani ndipo ianze kuvutia mashabiki. Lakini wanasema matokeo pekee hayavutii sana mashabiki, hasa kwa nchi kama hii ambayo ni kama imegawanyika nusu kwa nusu kwa kuziangalia Simba na Yanga.

Mashabiki pia huangalia ni jinsi gani wanahusiana na timu zao, hapa ni kuangalia uimara wa klabu na utamaduni wake. Yaani leo klabu inapata matokeo haya, zengwe linaanza hadi uongozi unang’oka, keshokutwa tatizo jingine hadi mashabiki hawaelewi kinachoendelea.

Wataalamu hao wanaona kuwa ushirikishaji mashabiki lazima uangaliwe katika mambo manne; siku za mechi, siku zisizo za mechi, mazoezini na nje ya mazoezi. Mashabiki wanashirikishwaje?

Kuna program gani za kushirikisha mashabiki siku za mechi, siku zisizo za mechi, mazoezini na nje ya mazoezi? Kuna tiketi maalum kwa ajili ya mashabiki kuungana na viongozi na wachezaji nyota siku za mechi?

Labda kwa sababu huku viwanja ni vya wazi, mashabiki huweza kuhudhuria mazoezi ya timu yao. Kwa wenzetu, siku za mashabiki kuhudhuria mazoezi ya timu ni maalum, na hasa siku ambazo kocha hafundishi mbinu. Huku tunashirikishaje mashabiki siku za mazoezi?

Lakini kitu kingine kikubwa ambacho kinaendana na wakati ni kushirikisha mashabiki kwa kutumia mitandao ya kijamii kupeleka habari muhimu na za kufurahisha mashabiki. Simba, Yanga na Azam zimeanza kwa nguvu, lakini zimeishia kutoa taarifa tu, lakini si kushirikisha mashabiki.

Inakuwaje klabu kama Mtibwa Sugar, Kagera, Coastal Union, Prisons hazina akaunti za mitandao ya kijamii kwa ajili ya kushirikisha mashabiki wao?

Tunategemea mashabiki waje kwa bahati au tunaridhika kushangiliwa na mashabiki wa Yanga wakati timu tukicheza dhidi ya Simba?

Hatukasirishwi na hali ya viwanja kuwa tupu tunapocheza dhidi ya timu nyingine, ukiondoa Yanga na Simba?

Bila ya kuanza program maalum za kushirikisha mashabiki, Yanga na Simba wataendelea kuwa wenyeji ugenini.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz