Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Nyuma ya pazia la Comoro kuna makubwa

Comoro Pic Data Nyuma ya pazia la Comoro kuna makubwa

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Comoro imeshangaza wengi kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu. Na si tu kufuzu, imezidi kushangaza wengi kutokana na matokeo yake na hasa kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Ghana, moja ya nchi zilizokuwa zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kabla ya kuanza kwa fainali hizo.

Comoro, ambayo ilijiunga na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka 2003 na baadaye Fifa mwaka 2005, ilifuzu kucheza fainali za mwaka huu kwa kushika nafasi ya pili katika kundi lililokuwa na nchi za Misri, Kenya na Togo.

Imekuwa ni maendeleo madogo madogo tangu kuundwa kwa shirikisho la soka la Comoro mwaka 1979, baadhi ya mafanikio ni pamoja na kupata ushindi wa kwanza katika michuano ya Cosafa iliposhiriki kwa mara ya pili mwaka 2009,ilipoilaza Seychelles na baadaye kutoka sare na Botswana kabla ya kufungwa mabao 3-0 na Swaziland na kutolewa mashindanoni. Mafanikio makubwa iliyapata mwaka 2019, ikiwa ni miaka miwili baada ya kutoshiriki mashindano hayo kuanzia 2013 hadi 2017. Mwaka huo iliongoza kundi lake baada ya Angola kujitoa na kuishinda Mauritius na kutoka sare ya Swaziland, lakini ikafungwa na Zimbabwe katika nusu fainali.

Tangu ijiunge na FIFA mwaka 2005, Comoro imenufaika na ruzuku ya dola milioni 1.3 za Kimarekani kwa mwaka na imeingia katika programu za maendeleo za Fifa, Imeweza kukarabati Shule ya Soka ya Twamaya Academy Near ya Moroni, wakati Dola 11.4 Milioni zitatumika katika ujenzi wa jengo jipya la utawala ifikapo mwaka huu.

Uwanjani, uamuzi sahihi kabisa ulikuwa wa kumteua Amir Abdou mwenye miaka 49 kuwa kocha wa timu ya taifa. Awali alitakiwa awe msaidizi wa kocha wa zamani wa klabu ya Marseille na Raja Casablanca, Henri Stambouli, lakini Mfaransa huyo akajiondoa baadaye.

Mzaliwa huyo chotara wa Ufaransa alifanya kazi ya kusaka wachezaji wenye asili ya Comoro katika Ligi Daraja la Pili na Tatu Kusini mwa Ufaransa. Na karibu wachezaji wote aliowapata ni chotara wa ama Kifaransa na Comoro, au Kibelgiji na Comoro.

Hi ni moja ya njia mbili za kuiwezesha timu ya taifa kupata mafanikio kwa nchi ndogo; wekeza katika soka na endeleza soka la watoto ama tafuta wachezaji waliolowea katika nchi zilizoendelea kisoka.

Comoro ni moja ya nchi tatu kutoka Cosafa (Baraza la Soka cha Nchi za Kusini mwa Afrika), zilizofuzu kucheza fainali za mwaka huu za AFCON, ikiwa pamoja na Malawi na Zimbabwe. Comoro, ambayo ina watu takriban 900,000 na Malawi zimefuzu kucheza 16 Bora.

Ni mafanikio ambayo si ya kubahatisha kwa nchi hizo mbili, na hata kwa Zimbabwe ambayo imetolewa, zote zikiwa zimeonyesha soka la hali ya juu, kujituma na nidhamu ya mbinu.

Nchi wanachama wa Cosafa zimekuwa zikijikita sana katika programu za maendeleo ya soka, na hasa soka la watoto na vijana. Mafanikio ya programu za nchi hizo hupimwa katika michuano ya umri tofauti ya Cosafa, ambayo ni pamoja na vijana walio na umri chini ya miaka 17 na 20 kwa vijana wa kiume na kike ambayo hufanyika kila mwaka, huku yale ya wakubwa yakitumika zaidi kujaribu wachezaji wa ndani.

Uwezo wa Cosafa katika kutafuta fedha za kuendeshea mashindano hayo umewezesha chombo hicho kuandaa mashindano hayo yote kila mwaka bila ya kutetereka na hivyo kuzalisha wachezaji waliopigwa kisayansi wenye uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu.

Wakati Comoro na Cosafa bado ni changa, ushiriki wa nchi za Afrika Mashariki, ambao unahusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini umekuwa hauna uhakika sana.

Katika fainali za mwaka huu ni ukanda wa Afrika Mashariki pekee ambao hauna uwakilishi licha ya Cecafa kuwa ni shirikisho lenye mashindano yenye umri mkubwa kuliko ukanda mwingine wowote barani Afrika.

Kutoweka umuhimu katika soka la watoto na vijana ni moja ya sababu ambazo zinafanya ushiriki wa nchi za Cecafa kuwa wa kubahatisha. Wakati angalau Uganda ina shule za kuaminika, nchi nyingine hazina shule za kuaminika ama kubahatisha, kitu ambacho huwezi kuwa na uhakika nacho.

Hapa Tanzania shule zinaibuka kwa matarajio makubwa ya kuuza wachezaji baada ya muda mfupi, lakini baadaye zinayeyuka au kufifia.

Ukikosa shule za soka, hata kuuza nje wachezaji inakuwa ni kwa kubahatisha kwa kuwa hata hao wanaotoka hawatoi picha nzuri ya hali ya soka nchini.

Na usipouza wachezaji nje, uwezekano wa kuwa na timu bora ya taifa ya nchi ambayo ubora wa ligi yake kuu si wa hali ya juu, ni mdogo na hivyo inakuwa ngumu kupanda katika viwango vya Fifa na hivyo masharti kwa wachezaji wetu kuwa magumu zaidi.

Huwezi kucheza Uingereza kama nchi iko chini ya timu 50 bora katika viwango vya Fifa. Na hii ni sheria za kazi za nchi, na wala si kanuni za chama cha soka. Mbwana Samatta alicheza England kwa kuwa alitokea Ubelgiji.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz