Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Ni vituko uwanja wa Kaitaba kufungiwa eti kwa kukosa uzio

Kaitaba Stadium Pp Ni vituko uwanja wa Kaitaba kufungiwa eti kwa kukosa uzio

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Katika maeneo ambayo huwa na mikusanyiko, kuna mabango yanayoelekeza watu maeneo ya kukimbilia kama kuna tatizo lolote kama moto, tetemeko la ardhi au jengo kuanza kuanguka na majanga mengine.

Hii ni kwa sababu za kiusalama kwa watu hao ambao wamekusanyika eneo hilo kwa ajili ya huduma tofauti kama kazi, burudani, ibada, matibabu au kufuata vitu kama maji kwa maeneo ambayo huduma hiyo ni ngumu kupatikana.

Maana yake, kunapotokea janga lolote, watu hawana budi kukimbilia eneo hilo kwanza kwa sababu za kiusalama. Hii ina maanisha eneo hilo ni lazima liwe rahisi kufikika kwa mtu yeyote aliyepo uwanjani.

Kwenye kampuni zilizo na mitambo kama makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ni lazima kuwe na eneo la wazi kwa ajili ya usalama iwapo kutatokea moto, shambulio au tatizo jingine lolote.

Ndivyo inavyotakiwa kuwa katika viwanja vya michezo. Kwamba mashabiki wanaoenda kuangalia mechi, ni lazima usalama wao uhakikishwe kwa kuwepo eneo ambalo wataweza kukimbilia kwa ajili ya kujikinga kama kutatokea janga kama la moto, tetemeko la ardhi, shambulio la kigaidi, kiwewe au tatizo jingine lolote ambalo halikutarajiwa.

Bila kuwepo na eneo kama hilo, maana yake kama janga lolote likitokea uwezekano wa watu wengi kuathirika ni mkubwa. Kama watu hawajui sehemu ya kujiokoa, wanaweza kukanyagana na hatimaye wengi kupoteza maisha kwa kuwa sehemu ya usalama haikujulikana au ni ngumu kufikika.

Wakati wa kuelekea fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1998 nchini Ufaransa, kuliibuka mjadala mkubwa kati ya wenyeji Ufaransa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuhusu uzio uliokuwa ukiwekwa viwanjani kwa ajili ya kudhibiti mashabiki wasiingie eneo la kuchezea soka.

Ufaransa iliona ni jambo jema kuweka uzio viwanjani kudhibiti mashabiki kuvamia uwanja na kufanya fujo, lakini Fifa iliweka msimamo kuwa mashabiki ni binadamu kama wengine na hawahitaji kudhibitiwa kama wanyama.

Fifa ilieleza wazi kuwa kwa ajili ya usalama wa mashabiki ni muhimu sehemu ya kuchezea mpira ndio ikawa kimbilio la usalama na rahisi kufikika kuliko maeneo mengine ili kuwanusuru mashabiki na janga lolote linaloweza kutokea na kuwa hatari kwa usalama wao.

Hivyo, Fifa ikataka Ufaransa ihakikishe viwanja vyote vinakuwa na urahisi kwa mashabiki kufika eneo la kuchezea mpira iwapo kunaibuka tatizo lolote. Pengine ni kutokana na msimamo huo wa Fifa ndio maana wale mashabiki wanaoenda viwanjani na ajenda zao binafsi, huweza kukwepa walinzi na kuingia viwanjani na mabango yao au kwenda moja kwa moja kwa wachezaji wanaowazimia na kuomba kupiga nao picha.

Lakini ujanja wa wavamizi hao wenye ajenda binafsi, hauwezi kuondoa umuhimu kwa viwanja vya michezo kuwahakikishia mashabiki usalama wao wanapokuwa wanaangalia michezo.

Leo hii kuna mawasiliano makubwa baina ya wachezaji na mashabiki na hilo hujionyesha wakati mchezaji anapofunga bao au anapofanya jambo muhimu kwa kuwa huweza kwenda eneo la mashabiki na kukumbatiana nao na hata kuwakabidhi kitu kama jezi iwapo mchezo unakuwa umeisha.

Ilikuwa ni bahati mbaya sana wakati Fifa wanazozana na Ufaransa kuhusu uzio na usalama wa mashabiki, huku kwetu kulikuwa kunaendelea ukarabati wa Uwanja wa Taifa (sasa hivi wa Uhuru). Kama Fifa walivyopinga, ndivyo sisi tulivyofanya.

Pamoja na uwanja huo kuwa wa viwango vya Olimpiki, yaani unaoruhusu michezo tofauti kama soka na riadha, bado uzio mkubwa uliwekwa wenye vyuma ambavyo kwa kiasi fulani vinazinga mashabiki kuona matukio ya karibu. Lakini hakuna aliyekosoa kwa kuwa ukarabati huo ulifanywa kwa utashi wa waziri wa wakati huo na kwa kuwa serikali ndio mmiliki, hakukuwa na ukosoaji wowote.

Leo hii Uwanja wa Kaitaba ndio kwanza umeruhusiwa kuanza kutumika tena baada ya kufungiwa kwa miezi kadhaa ‘eti’ kwa sababu hauna uzio wa kudhibiti mashabiki kuingia sehemu ya kuchezea.

Ni bahati mbaya sana hilo limetokea miaka kadhaa baada ya ule mzozo wa Ufaransa na Fifa kuhusu usalama wa mashabiki.

Kibaya zaidi, hilo linafanyika katika kipindi ambacho Tanzania haijawahi kupata tatizo kubwa la vifo vya mashabiki kama lile la Mei 29, 1985 wakati mashabiki 39 walipopoteza maisha kwenye uwanja wa Heysel nchini Ubelgiji walipokwenda kuangalia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baina ya Liverpool na Juventus au lile la mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA baina ya Liverpool na Nottingham Forest Aprili mwaka 1989 kwenye Uwanja wa Hillsboroung ambako watu 97 walipoteza maisha.

Tukio la Hillsaboroung ndilo lililobadilisha usalama wa mashabiki viwanjani England hadi leo hii.

Hatutakiwi kusubiri majanga yanayopoteza maisha ya watu ndipo tuanze kutafuta njia za kudhibiti usalama wa mashabiki. Matukio yaliyotokea pande tofauti za dunia ni fundisho tosha la kutufanya tuanze kuchukua tahadhari mapema.

Hatua za kufungia Uwanja wa Kaitaba ‘eti’ kwa kutokuwa na uzio wa kudhibiti mashabiki, ni za kizamani sana na zinatengeneza bomu ambalo tutakuja kujutia baadaye.

Ni muhimu sana kwa Kamati ya Leseni za Klabu ya Bodi ya Ligi ikaangalia kwa makini mahitaji ya msingi ya viwanja kabla ya kuvifungia.

Taarifa zilizopo za wakaguzi kufanyiwa takrima na kuidhinisha viwanja ambavyo baadaye hufungiwa bila maelezo ya maana, hazitakiwi ziendelee kulelewa wakati zinaharibu taswira ya mpira wetu, hasa kwa wawekezaji ambao ni wadau muhimu kwa soka letu.

Kunahitajika majadiliano ya kina baina ya wamiliki wa viwanja na Kamati ya Leseni ya Bodi ya Ligi kuhusu uboreshaji wa viwanja kabla ya kuchukua hatua ambazo kiuchumi huathiri klabu zinazotakiwa zitupe burudani, hasa zinapocheza nyumbani.

Si vyema kuona klabu za Ligi Kuu zinazurura mikoani kutafuta viwanja vya nyumbani, huko ni kurudi nyuma sana.

Columnist: Mwanaspoti