Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Mbwana Makata angepewa heshima, sio adhabu

Mbwana Makata Mbwanaaa Mbwana Makata angepewa heshima, sio adhabu

Tue, 24 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mjadala mkubwa wa wiki iliyopita ulihusu adhabu ya kufungiwa miaka mitano kujihusisha na soka kwa kocha mzoefu, Mbwana Makata.

Mjadala haukuwa mkubwa kwa sababu Makata ni kocha mkubwa nchini, la hasha! Na haukuwa mkubwa kwa sababu ni adhabu ya kwanza kubwa, la hasha! Na wala haukuwa mkubwa kwa sababu adhabu hiyo ni kubwa, la hasha!

Ulikuwa mkubwa kwa sababu adhabu za aina hiyo sasa zimekithiri. Ni kama kuna watu wamekaririshwa kwamba mwanamichezo akikosea adhabu ianzie miaka mitano hadi kufungiwa maisha.

Ndiko mwenendo wa adhabu zinazoendelea kutolewa na vyombo vya haki vya Shirikisho la Soka (TFF). Na vyombo hivyo havijadili kwa kina kilichotokea, bali kuadhibu yeyote atakayewasilishwa mbele yao na si kumsikiliza!

Na wanaopeleka masuala hayo mbele ya vyombo hivyo ni walewale. Wao hawakosei. Mfano ile fedheha ya mwaka jana ya mechi ya Simba na Yanga kutofanyika, haijawahi kutolewa uamuzi wala adhabu kwa aliyehusika.

Kuna madai kuwa serikali ndio iliyoagiza muda wa kuanza mchezo huo usogezwe mbele kutoka saa 11:00 jioni hadi saa 1:00 usiku. Kwa kuwa ni serikali, ofisa mmoja wa TFF alijifungia ofisini na kuchoronga barua ya kusogeza mbele mchezo.

Hakusumbuka kuangalia kanuni zinasemaje, alishika maagizo hayo. Hakusumbuka kuziita klabu hizo mbili na kujadili nini kifanyike, bali alijifungia na kuandika baruapepe kuahirisha mchezo huo.

Huyu mpaka leo hajulikani na adhabu haijatolewa, achilia mbali kuomba radhi wapenzi na mashabiki waliokusanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, walioenda kwenye vituo vinavyoonyesha mechi moja kwa moja au waliosalia majumbani kujuona mchezo huo kwenye runinga.

Leo Mbwana Makata anafungiwa miaka mitano eti kwa sababu alishawishi wachezaji wa Mbeya Kwanza kususia mchezo wao na Namungo kutokana na kutokuwepo kwa gari la wagonjwa.

Alichofanya Makata hakitofautiani na kilichofanywa na Yanga siku ile; kufuata kanuni zinasemaje kuhusu muda wa kuanza mchezo na kwenxda uwanjani kama ilivyotakiwa.

Yaani, kama ni kweli alioshawishi wachezaji, Makata alisimamia kanuni zinazotaka kuwepo na gari la wagonjwa uwanjani na si gari jingine lolote linaloweza kumuwahisha mchezaji au mgonjwa hospitalini.

Gari la wagonjwa lina sifa zake tofauti na gari jingine lolote lile, hata liwe V8. Yule kipa wa Arusha aliyefariki baada ya kuchanwa koromeo na kiatu cha mchezaji, hakuhitaji gari la kumuwahisha hospitali bali uharaka wa huduma ya kwanza pale uwanjani na wakati akipelekwa hospitali.

Huduma ya kwanza maana yake ni kuwa na watabibu sahihi, vifaa sahihi ndani ya gari na dawa sahihi kwa ajili ya mgonjwa wakati akiwahishwa hospitalini kwa matibabu makubwa zaidi.

Makata na wenzake walitaka kanuni hii iheshimiwe kwa kuwa inahusu uhai wa wachezaji. Kwamba gari lilikuwepo baadaye likaitwa kumpeleka mjamzito hospitali, ni ngonjera zilizoandaliwa kuwalinda wakosefu.

Kwamba gari lilikuja uwanjani muda mfupi kabla ya mchezo kuanza ni ngonjera nyingine za kuwalinda wakosefu.

Wako wenyeji waliotakiwa kuhakikisha huduma ya uhakika ya gari la wagonjwa inakuwepo uwanjani. Hawa wamechukuliwa hatua gani. Yupo mkuu wa kituo ambaye alitakiwa kuhakikisha haya yote yanakamilishwa kabla ya mchezo, amechukuliwqa hatua gani. Yupo msimamizi wa mechi aliyetakiwa kuhakikisha masuala yote kuhusu mechi yanakamilishwa mapema na kuwekwa bayana katika kikao cha asubuhi cha pande zote, huyu amechukuliwa hatua gani.

Yaani kama hao wote wangewajibika, Makata na wenzake wasingefanya kosa lile. Iweje TFF ihangaike na ilipoanguka badala ya ilipojikwaa?

Kwangu Makata alistahili heshima kwa kujaribu kulinda kanuni za TFF badala ya hizi adhabu za kukariri za miaka mitano au maisha kwa kufanya kosa kwa mara ya kwanza.

Adhabu hizi hazitasaidia kuleta nidhamu katika mpira, bali kulea uozo ambao utaharibu zaidi mpira wa miguu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz