Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Kuna haja ya weledi katika uchambuzi

Uchambuzi Pic Kuna haja ya weledi katika uchambuzi

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kadri mpira unavyokua ndivyo mabadiliko yanavyotokea katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya uwanja. Ndivyo yalivyo mabadiliko katika kila nyanja.

Zamani mpira wa miguu haukuwa na waamuzi, bali mtu ambaye aliaminiwa na wengi ndiye aliyepewa jukumu la kupuliza filimbi bila ya kujali anatoka moja ya timu zinazopambana.

Lakini baadaye kukaonekana haja ya kuwa na watu maalum kwa ajili ya uamuzi na hivyo uamuzi ukatengenezewa kanuni zake na miiko na hivyo kuwa taaluma.

Kadri mpira ulivyokuwa ndivyo mabadiliko yalivyozidi kutokea na hadi sasa tayari kuna waamuzi wa kulipwa wanaochezesha mechi za ligi za juu, achilia mbali kina Pierluigi Collina ambao walikuwa wa ridhaa wakitegemea riziki zao sehemu nyingine za kazi.

Hata makocha hawakuwa na taaluma maalum zaidi ya mtu mmoja mzoefu kuteuliwa kuwaongoza wenzake, hadi ilipoibuka haja ya kuwa na watu maalum kwa ajili ya kazi hiyo. Na hivyo kanuni zikaandaliwa miiko na sayansi ikawekwa ndani yake ili kuwa na watu maalum kwa ajili ya kazi hiyo.

Walimu nao wakagawanyika. Sasa wapo wale maalum kwa kikosi cha kwanza, kwa ajili ya makipa, kwa ajili ya mabeki, kwa ajili ya washambuliaji na kwa ajili ya utimamu wa mwili.

Mpira hapa Tanzania sasa unahitaji wachambuzi kurahisishia mashabiki kuelewa matukio ya uwanjani, mifumo inayotumika, mbinu, ujanja wa wachezaji na sheria ambazo huibua mijadala mingi.

Wenzetu wanatumia wachezaji wa zamani kuchambua mechi—si kila jambo—kutokana na uzoefu wao wa uwanjani, wa maelekezo ya walimu, siasa za nje ya uwanja au vyumbani na tabia za wachezaji. Na hawa huchukuliwa sababu kwa kuwa timu zinazocheza siku hiyo labda katika matukio machache. Yaani Andy Cole ataitwa siku ambayo Manchester United inacheza.

Kwetu ni wachezaji wachache wa zamani wanaitwa. Haijulikani ni kwa nini.

Hoja yangu kubwa leo ni suala la kuweka maadili katika uchambuzi. Wachambuzi tulio nao hawaishii kuchambua mechi tu, bali kila kitu-- mifumo ya uongozi, udhamini, uendeshaji klabu na shirikisho, masuala ya fedha, usimamizi wa wachezaji na uwakala wa mechi, kwa kutaja machache.

Lakini, kama binadamu, wana shughuli nyingine za kujipatia kipato. Ila kilicho karibu yao ni fursa zilizopo katika mpira wa miguu. Kuna kundi la wachambuzi linaloingia katika kazi ya kusimamia wachezaji. Hili linakua kwa kasi na si siri.

Inawezekana basi wakachambua wachezaji haohao wanaowasimamia au wasiowasimamia? Wakachambua ubovu au uzuri wa viongozi wa klabu? Wakalichambua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au mambo mengine mengi yaliyo kwenye 18 zao?

Kuna kiwango gani cha weledi kinachoweza kuwazuia hawa wasichanganye maslahi binafsi katika masuala wanayochambua? Kwamba mchezaji wa meneja fulani hakucheza vizuri na kesho amseme bayana kuwa ndiye aliyeiponza timu yake? Haiwezekani! Ni lazima mzigo utapunguzwa kidogo kwa mteja wake.

Vipi kwa viongozi ambao watamtimua mchezaji aliye chini ya menejimenti yake? Kuna uwezekano hao viongozi ndio wakawa wanashambuliwa kila siku katika uchambuzi wao kuwa ni wabovu.

Vipi kwa matajiri ambao wanawafadhili au kuwapa fursa za kiuchumi. Wakiboronga katika uongozi au udhamini, watachambuliwa kwa haki? Nadhani suala la mabadiliko ya kimfumo ya Simba na Yanga yamejionyesha.

Ni muhimu katika mazingira kama hayo kuwe na kanuni za maadili zitakazowaongoza wachambuzi katika kazi zao. Kwa kuwa tunawahitaji na pia tunahitaji kitu kilichochambuliwa kwa haki, ni lazima tuangalie hili suala kwa makini, la sivyo hizi kelele dhidi ya wachambuzi zitazidi na mwisho zitaonekana za kweli.

Columnist: Mwanaspoti