Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Kulihitajika heshima kwa mpira wa miguu

Yanga Yafuzu Tunius Kulihitajika heshima kwa mpira wa miguu

Tue, 15 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Katika maisha kila siku inayopita inatoa fursa ya kujifunza kitu na kusonga mbele. Fursa hiyo ndiyo humpa mtu ujuzi na uzoefu wa jambo lolote linalomtokea, iwe kwa mara ya kwanza au ya pili au kama linatokea kwa kujirudiarudia.

Ndio maana wale walio na muda mrefu duniani hutokea kuwa na uzoefu mkubwa kutokana na kukutana na mambo mengi na kuona njia tofauti za kupambana nayo.

Wiki iliyopita, ilikuwa ni zamu ya mabingwa wa soka nchini, Yanga, kutuongezea ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchambuzi, hasa wa mpira wa miguu. Ni somo ambalo liliwahi kutolewa mara mbili pia na Simba katika michuano ya kimataifa; ya kwanza ikiwa ni ushindi mkubwa wa ugenini ambao Simba ilipata dhidi ya Mufurila Wanderers iliposhinda mabao 5-0 baada ya kukubali kipigo cha mabnao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa mwaka 1979. Ya pili ikiwa ni ushindi wa penalti dhidi ya Zamalek jijini Cairo, Misri 2003.

Kwa kifupi matokeo hayo yangeweza kutumika kuizungumzia mechi ya maruidiano ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Yanga na Club Africain, lakini pengine wengi hawakurudi nyuma katika historia na kutaka kutumia mechi moja tu ya kwanza jijini Dar es Salaam iliyoisha kwa sare ya bila kufungana, kuzungumzia mchezo wa marudiano.

Imekuwa ni kawaida kwa wachambuzi wengi kutotumia taarifa za nyuma kuangalia uwezekano wa matokeo ya mechi inayokuja. Najua hivi sasa wachambuzi wengi wanatumia hoja nyingi kujaribu kupaka rangi juu ya walichokitabiri ili waonekane walikuwa na sababu ya kutoitabiria mema Yanga.

Wengi walishindwa kuupa mchezo wa soka heshima unaostahili kiasi cha kuufanya uwe mchezo ambao kutabirika kwake ni asilimia ndogo na hivyo kupendwa na kampuni zinazoendesha kamari duniani.

Wengine walitaka kutoa maneno ambayo baadaye wangesema ‘nilishaona’ au ‘si nilisema’ badala ya kuangalia hali halisi na utamaduni wa mpira wa miguu wa matokeo yake kutotabirika.

Wengine walisahau ukweli kwamba mpira wa miguu hutoa nafasi kwa aliyefanya vibaya, kujirekebisha na ndio maana ulifuta hata kanuni ya Bao la Dhahabu (sudden death) kwa kuwa lilikuwa la katili lisiloendana na utamaduni wa soka.

Baada ya Yanga kulazimishwa kwa sare ya bila kufungana jijini Dar es Salaam ilikuwa ni rahisi kwa mtu asiyezingatia hayo niliyotaja hapo juu kuzungumzia uwezekano wa matokeo ya mechi ya marudiano. Lililoangaliwa pekee ni utamaduni wa timu za Kiarabu kutumia vyema uwanja wa nyumbani, hasa zinapokutana na timu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki.

Na wengine waliendelea na imani kuwa Yanga haifanyi vizuri kwenye michuano ya kimataifa kwa hiyo haiwezi kufanya lolote Tunisia. Walitumia aina ya ujuzi wa ujumuishaji (generalization) kuzungumzia matokeo ya mechi ya mariudiano.

Wapo waliosema kwa kujiamini kuwa ‘Yanga hatoboi Tunisia’ na wengine ‘safari ya Yanga imeishia Kwa Mkapa’ na wengine walidiriki hata kusema ‘Yanga itakutana na maafa Tunisia.’ Sina tatizo na mashabiki au watumiaji wa mitandao kusema hayo, tatizo langu ni kwa wale walio kwenye vyombo vya habari vinavyohudumia umma.

Ndio yanaweza kuwa ni maoni yao, lakini maoni hujengwa juu ya misingi fulani kama hiyo niliyoitaja hapo juu kuwa ni utamaduni wa mpira wa miguu, uzoefu na matokeo yasiyotabirika.

Naamini kwa kujua hayo, mtu asingeweza kusimama mbele ya kamera na kusema kwa kujiamini kuwa ‘Yanga hatoboi.’ Angeweza kusema hivyo kwa kutumia kiwango kilichoonyeshwa, lakini angekuwa na akiba kwa kuzingatia mambo hayo muhimu katika soka.

Angeweza kusema kama wangecheza vibaya kama walivyocheza Uwanja wa Mkapa, basi uwezekano wa kushinda ugenini au kupata matokeo mazuri ungekuwa mdogo. Kauli kama hiyo ina akiba ya maneno.

Lakini ni kweli Yanga ilicheza vibaya sana kiasi cha kusema isingeweza kupata matokeo mazuri ugenini? Kama kutawala mchezo wa kwanza ilitawala sehemu kubwa; kama ni wageni kuonyesha kuwa ni wakali lakini wamehifadhi ukali wao, hakukuwa na kitu kama hicho. Walichofanya ni kupoteza muda na kumvuruga mwamuzi.

Hii ingempa mtu picha kwamba huenda wakawa hatari nyumbani kwao hasa baada ya kuishinda Kipanga kwa mabao 7-0. Lakini hilo pekee lisingetosha kumpa mtu ujasiri wa kusema kwa uhakika kuwa haitatoboa. Kwamba kusema ‘kwa jinsi walivyopoteza muda, Club Africain lazima washinde nyumbani kwao!’ haileti maana.

Unajiuliza sasa hao wachambuzi waliodiriki kusema hayo walizingatia nini hasa. Bila shaka utagundua kuwa walifanya kwa mazoea kwa kuwa matokeo yakiwa tofauti, wataweza kutumia tena vyombo vya habari kupamba uozo wao.

Kuzungumzia maoni hayo bila ya uchambuzi yakinifu hakuna ubaya kama hilo linafanyika kwenye akaunti binafsi za mitandao ya kijamii kwa kuwa mtu unachora taswira yako binafsi, lakini unapotumia vyombo vya habari vinavyohudumia umma ni muhimu kuwa na tahadhari ya maneno, kuheshimu timu na wachezaji, bila ya kusahau mchezo wenyewe na utamaduni wake.

Na cha muhimu zaidi, uchambuzi si ubashiri wa matokeo kama wengi wanavyofanya, ni jambo linalofanyika kisayansi kwa kutumia ujuzi wa aina tofauti.

Na kwa wenzetu, wachambuzi wao wengi hujiepusha na kutabiri matokeo. Wengi wanapoulizwa wanatarajia nini huweka sentensi mbele kulinda maoni yao kuhusu uwezekano wa matokeo ya mechi nyingine au kipindi cha pili.

Lakini hapa tunatumia ubashiri kuongeza umaarufu iwapo matokeo yatakwenda kulingana na maoni, wakati hakuna hoja za kisayaynsi zilizomfanya mtu atoe ubashiri fulani.

Baada ya Yanga kushinda ugenini ndani ya dakika 90, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania kupata matokeo ya aina hiyo dhidi ya timu za Kaskazini, tumepata elimu kuwa lolote linawezekana katika soka na hivyo ni muhimu kuzingatia mambo mengi kabla ya kutoa ubashiri na kwamba ubashiri uwe na akiba ya maneno.

Wachambuzi waachane na hao mashabiki wanaosema timu fulani ikishinda ‘namtoa mke wangu kwa’ mtu fulani au ‘nitavua nguo na kutembea kutoka Mwenge hadi Morocco.’0 Kauli kama hizo hazisaidii wasomaji, wasikilizaji wa redio au watazamaji televisheni.

Kwanza unatembea uchi ili iweje au ukishamtoa mkeo kwa mwingine inasaidia nini. Hao ni mashabiki wasiojali chochote.

Wachambuzi wakiingiza hayo katika mazungumzo yao redioni, kwenye televisheni au magazetini, hawatofautiani na wale mashabiki wanaowahoji na kutoa viapo hivyo vya mke na kutembea uchi.

Mpira wa miguu ni mchezo unaoongoza duniani kwa kutotabirika.

Hata Brazil iliyokuwa inaaminika kuwa na ngome ngumu kuwahi kutokea nchini humo iliyokuwa na wachezaji kina Maicon, Lucio, Juan, Bastos Michel, Luisao na Dani Alves ambayo ilicheza mechi 10 bila ya kuruhusu bao wakati ikielekea fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010, iliruhusu bao la Jabir Aziz wa Tanzania kwenye Uwanja wa Mkapa.

Lipi haliwezekani? Tuuheshimu mpira wa miguu.

Columnist: Mwanaspoti