Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Kuanza, kuisha kwa msimu kuwe sheria

Tff Office Shirikisho la Soka Tanzania, TFF

Wed, 8 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki tuliyoimaliza na hii tunayoendelea nayo zilikuwa za mechi za kimataifa za mashindano tofauti duniani; Ulaya, Amerika Kusini, Asia, Afrika na Amerika Kaskazini.

Wachezaji wa mataifa hayo wameenda kutumikia timu zao za taifa bila ya mizozo na klabu zao, kama ambavyo imezoeleka wakati klabu zinapojaribu kuzuia wachezaji wao kwa visingizio tofauti kama majeraha na mambo mengine.

Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya dunia imeshamaliza msimu wa soka na hivyo wale wachezaji walio na majukumu ya kitaifa wanaenda kwenye timu zao bila ya matatizo, lakini wale ambao hawana wameshaanza mapumziko ya muda mrefu, baadhi wakija kutalii Tanzania.

Viongozi katika klabu wanaweka mambo sawa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa soka ambao kwa nchi nyingi huanza Septemba na inapofika mwishoni mwa Desemba ndipo kunakuwa na mapumziko mafupi ambayo hutumiwa kama dirisha dogo kwa ajili ya usajili.

Na kikubwa zaidi, mwaka huu mwishoni kutakuwa na Fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika kuanzia Novemba hadi Desemba, hivyo ni lazima nchi ambazo zimefuzu, zitakuwa zimeweka mazingira ya kusimamisha mashindano wakati huo.

Lakini hali ni tofauti hapa kwetu. Hadi tunakwenda mapumziko marefu ya majira ya joto ambayo huwa kuanzia Juni, ligi zetu bado hazijamalizika.

Bado Ligi Kuu imebakiza raundi sita kuhitimishwa, kitu kinachomaanisha ligi yaweza kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni au mapema Julai.

Kwa kuwa viongozi wa baadhi ya klabu walijua ligi yetu ingewahi kuisha, mikataba ya wachezaji kama Saido Ntibazonkiza ilipangwa iishe Mei, lakini bahati mbaya ligi ndio kwanza inatafuta tamati yake.

Maana yake ni kwamba wachezaji hawatakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika na kama watapewa muda wa kutosha, maana yake ligi itachelewa kuanza na hivyo itachelewa tena kuisha!

Klabu zitaingia sokoni kusaka wachezaji kwa pupa kutokana na ukweli kwamba mambo mengi hujulikana baada ya ligi kuisha rasmi.

Pia klabu haziweza kuwa na mipango thabiti ya maandalizi ya msimu mpya, hasa zile mechi ambazo huchezwa wakati wa mapumziko wakati timu zikianza kujaribisha vikosi baada ya mazoezi magumu ya kurudisha utimamu wa mwili wa wachezaji.

Yaani tutakuta wenzetu wameshavuka hatua fulani ya maandalizi na hivyo litakalofanyika ni kucheza mechi za humuhumu ndani na si dhidi ya timu za nje kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi.

Hii pia inasababisha kusiwepo na mwanya wa kuanzisha mashindano mengine makubwa. England au nchi zote za Ulaya zina michuano kama ya ligi za kitaifa, Kombe la FA na Kombe la Ligi au Hispania wanalo Kombe la Mfalme. Uwingi wa mashindano pia ni jukwaa la kupata wadhamini na hali kadhalika kutumia wachezaji wengi zaidi kuliko kuwa na michuano michache.

Inaonekana kama suala la kuchelewa kuanza na kumaliza msimu limekuwa ni tatizo kubwa na ambalo wahusika hawaoni athari zake kwa haraka au kama wameziona wana majibu mepesi ya kutetea hali hiyo.

Kama inaonekana ni tatizo kubwa, basi ni vyema suala linatakiwa liwekwe kwenye katiba kwamba “msimu wa mashindano utaanza Oktoba na kumalizika Mei”. Hii itafanya yeyote atakayehusika kuchelewesha ligi kuanza au kumalizika, awe amekiuka katiba na hivyo kustahili kuondolewa kabisa kwa kuwa ukiukwaji wa katiba ni kosa kubwa.

Bila kufanya hivyo, mechi zitakuwa zinaahirishwa kiholela na itaendelea kufinyisha nafasi ya kuandaa mashindano mengine makubwa.

Ni muhimu suala hili likafanyiwa kazi vizuri na ikiwezekana basi liundiwe sharia ili asiwepo mkiukaji.

Columnist: Mwanaspoti