Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Hakuna kosa linalohalalisha kosa jingine

Refareee SIO ZENGWE: Hakuna kosa linalohalalisha kosa jingine

Tue, 7 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MARTIN Saanya alikuwa gumzo la mashabiki wa soka kwa wiki nzima iliyopita baada ya kutumia yale mamlaka yake anayopewa na sharia za mpira wa miguu ya kufanya uamuzi wa mwisho kwa mtazamo wake.

Hata walioendelea kwa teknolojia ambao hivi sasa wanatumia mwamuzi msaidizi wa video (V.A.R) kumsaidia mwamuzi wa kati kufanya uamuzi sasa, bado wamemuachia refa wa kati mamlaka kamili kufanya uamuzi kwa mtazamo wake.

Atakachofanya ni kwenda kwenye runinga iliyowekwa pale uwanjani, kuangalia marudio ya tukio ambalo hakuliona vizuri na kufanya uamuzi. V.A.R haimlazimishi mwamuzi kubatilisha uamuzi wake au kufanya uamuzi tukio ambalo lilimpita, bali humsaidia kuliona kutoka sehemu tofauti na kufanya uamuzi kwa mtazamo wake na tafsiri ya sheria.

Hata kama atakosea, matokeo ya mchezo huo hayatabatilishwa kutokana na uamuzi wake mbovu. Kwa nchi ambazo hawataki masihara, mwamuzi huyo anaweza kuadhibiwa kwa kumuondoa kwenye orodha ya daraja analochezea, kumpeleka ligi za chini ajikosoe zaidi na kuimarika.

Ndivyo ilivyo duniani kote. Utamaduni huo wa mpira huweza kusababisha watu wenye mioyo midogo kutoona umuhimu wa kujadili kosa ambalo haliwezi kusahihishwa kwa kuwa mijadala haitabadili matokeo.

Lakini kwa sababu mpira wa miguu unachezwa na binadamu ambao hurekebisha mambo kadri siku zinavyokwenda ili kuwa na kitu kizuri, ni muhimu makossa ya waamuzi yakawa yanajadiliwa kwa kina ili kutafuta mbinu japo ya kuyapunguza.

Nimemsikia rais wa TFF, Wallace Karia anasema kuna baadhi ya matukio yanakuzwa kwa sababu yanazihusu Yanga na Simba, lakini akasema makosa ya waamuzi yapo mengi tu katika mechi ambazo hazifuatiliwi na mashabiki wa timu kubwa.

Kwa kifupi alikuwa akikiri kuwa kuna tatizo katika uamuzi na njia ya kuuimarisha mchezo huu pendwa ni kutafuta suluhisho la janga hili linalozidi kuondoa hamu ya soka. Kama bingwa atapatikana kwa njia ya makosa ya waamuzi, ni dhahiri kuwa mchezo huu utapoteza mvuto na watu wengi kuacha kuufuatilia.

Rekodi za mahudhurio ya mashabiki viwanjani mwaka jana iliyotolewa na Bodi ya Ligi, ni mfano tosha. Kuna tatizo mahali fulani linalohitaji tiba ya haraka.

Ni ajabu kwamba watu wanaoaminika katika soka ndio wanaokimbilia kuzima mjadala wa kosa la Saanya kwa kuwatuhumu wanaolizungumzia kuwa wanaingiza ushabiki.

Wapo walioamua hata kutumia clip za video zilipochukuliwa kutoka mgongoni mwa George Mpepo aliyefunga, kudai kuwa clip hiyo imewathibitishia kuwa mfungaji ‘alimgusa’ Shomari Kapombe kabla ya kuruka kufunga.

Wapo wanaotumia clip ya video inayoonyesha Mpepo akimshika mkono Kapombe na kutafsiri kuwa alikuwa akimuomba radhi kwa kumsukuma, na si kwamba anaweza kuwa alikuwa anamtaka athibitishe kuwa alisukumwa.

Na kundi baya zaidi ni lile linalotumia video za matukio ya mechi nyingine alizochezesha Saanya kuhalalisha kosa hilo la juzi. Wazungu wanasema “no wrong right another”, yaani hakuna kosa linalohalalisha kosa jingine.

Ukikamatwa unaiba, huwezi kujitetea mahakamani kuwa mbona na fulani aliiba. Adhabu itakuhusu wewe uliyekamatwa.

Mwaka jana, bao lililofungwa na Simba kwa kichwa lilikataliwa na mwamuzi aliyedai kuwa mpira ulitoka nje kabla ya kurudi uwanjani. Siku chache baadaye refa mwingine akakataa bao la Yanga kwa maelezo kama hayo.

Kosa la mwamuzi wa mechi ya Simba likatumika kuhalalisha kosa la mwamuzi wa mechi ya Yanga. Kwa hiyo hakuna haja ya kujadili. Hao ndio watu wa mpira.

Kwa kifupi kuna tatizo kubwa katika uamuzi. Mpira unahitaji uwekezaji mkubwa sana katika eneo hilo. Wenzetu wamewekeza teknolojia ya hali ya juu ili waamuzi wafanye uamuzi wa haki.

Walitumia hata waamuzi wasaidizi watano, kitu ambacho ni gharama kubwa. Sisi huku ambao kiuchumi bado tuko nyuma, hatuna budi kuangalia nini kinaweza kutusaidia kuboresha eneo hilo. Kibaya sana, Saanya anaweza kuwa ndio mzoefu kuliko waamuzi wengi wa Ligi Kuu, lakini anaweza kuwa ndiye mwenye matukio tata makubwa.

Hata hivyo, Saanya ni samaki mmoja tu kati ya wengi wenye uzoefu. Angalau tuanzie hapo kuliko kuendelea kutumia makossa kuhalalisha mengine.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz