Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Bora Simba, Yanga zimepita, sasa tujadili soka

Bora Pic Clatous Chama akimtoka Feisal Salum

Wed, 4 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ahueni! Mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kuwa hawajafurahjishwa na matokeo ya sare isiyo na mabao baina ya timu zao zilizokutana Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini kwangu ni ahueni mechi hiyo kupita.

Si kwa sababu ya sare ambayo haimpi yeyote mamlaka ya kutamba, wala si kwa sababu sare hiyo inazidi kumjengea mmojawapo njia ya ubingwa, wala si kwa sababu sare hiyo ni ya pili mfululizo na inasababisha msimu wa ligi uishe bila ya mbabe baina ya vigogo hao, la hasha.

Bali kupita kwa mchezo huo kunatoa nafasi kwa mchezo wa mpira wa miguu kuzungumzwa kwa dhati na kwa mapana yake.

Kwa takriban wiki mbili na pengine hata mwezi mzima, mpira wa miguu nchini umekuwa ukizungumzwa kwa kuangalia mechi hiyo ambao baadhi wamediriki kuiita ‘derby’ bora ya Afrika Mashariki‚“ kwa sababu tu inajaza uwanja.

Kila kilichozungumzwa kuhusu mpira, kilihusishwa na mechi hiyo. Ajabu, hata Simba wakati inaenda kucheza mechi mbili za robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilichukuliwa kama maandalizi ya derby ya Kariakoo. Umuhimu na ukubwa wa mechi hizo za Afrika haukuzingatiwa.

Yule aliyetaka kuzungumzia hoja nzito, ilipimwa kwa kuangalia mechi hiyo na kama angetaja moja ya timu hizo, angeshambuliwa vikali kuwa, amejaa unazi.

Kwa hiyo ili mtu huyo aonekane anazungumza kitu cha maana ilibidi ahusishe mazungumzo yake na moja ya timu hizo ili aungwe mkono na kundi moja.

Kwa ujumla mchezo wa timu hizo ulitutoa akili, si kwenye redio, televisheni, magazetini au vijiweni, kila mtu alitaka kuzungumzia Simba na Yanga ili aonekane anajua mpira.

Namshangaa hata Haji Manara kuhangaika kuiuza mechi wakati ilishajitangaza kwa takriban mwezi mzima.

Sidhani kama hali kama hii hutawala mazungumzo barani Ulaya zinapokaribia mechi kubwa kama ya Real Madrid na Barcelona. Huwa sioni kiwango hicho cha mijadala kama ya watani hao wa jadi wa Kariakoo.

Kwa kweli tunakosa kitu fulani kwa kujikita kuzungumzia timu mbili tu kana kwamba timu nyingine 14 kwenye Ligi Kuu ni dhaifu sana kiasi cha Simba na Yanga kuwa zinajiokotea pointi tu.

Ukweli ni kwamba nje ya Simba na Yanga kuna mengi mazuri na makubwa, achilia mbali lile bao kali la George Mpole dhidi ya Azam.

Sidhani kama Prince Dube hana mengi ya kujadiliwa pale Azam. Hata ile hali ya kufunga mabao machache msimu huu ni mjadala tosha licha ya ukweli kwamba wakati fulani alikuwa majeruhi.

Chipukizi kama Tepsie Evans aliyefanikiwa kujipenyeza kikosi cha kwanza cha Azam angekuwa gumzo kubwa kama angekuwa kwa watani hao wa jadi. Lakini hatumuoni kwa uzito huo kwa kuwa yuko Azam.

Reliants Luasajo kucheza mechi kadhaa sasa ndani ya zaidi ya miezi miwili bila ya bao ni mjadala mkubwa baada ya kuchomoka katika orodha ya wafungaji na kufikisha mabao tisa wakati kina Fiston Mayele wakiwa na mabao sita tu wakati huo.

Hata Alan Shearer alipokuwa anashindwa kufunga katika mechi kadhaa ilikuwa mjadala, licha ya kwamba hakuwa klabu kubwa wakati huo kama Manchester United au Liverpool.

Wala usimzungumzie Diego Maradona pale Napoli, licha ya kuwepo klabu kubwa Italia kama Juventus, AC Milan na Inter Milan.

Tunahitaji kutumia muda wetu vizuri kuzungumzia mpira na maendeleo yake na si kutafuta umaarufu wa lazima kuzungumzia Simba na Yanga.

Maendeleo ya soka hayawezi kuletwa na Wallace Karia peke yake au Shirikisho la Soka (TFF) pekee, bali kila mmoja kutimiza wajibu wake pale alipo.

Wale ambao mchango wao katika maendeleo ya soka ni kujadili, basi watekeleze jukumu hilo kwa dhati ili Karia na TFF yake wanufaike na mijadala na kuchukua hatua zinazostahili.

Columnist: www.tanzaniaweb.live