Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Bado sana, lakini sakata la Chelsea lina somo

Zengwe Pic SIO ZENGWE: Bado sana, lakini sakata la Chelsea lina somo

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna shabiki wa Chelsea anayefurahishwa na kile kinachoendelea kwa sasa kuhusu umiliki wa klabu hiyo baada ya serikali ya Uingereza kumuwekea vikwazo vya kiuchumi mwekezaji wake, Roman Abramovich.

Wengi wamefikia hatua ya kusema sasa si Abramovich tena, bali ni kuisakama klabu hiyo ambayo kwa sasa ni bingwa wa dunia na inatetea ubingwa wa Ulaya.

Kutokana na Abramovich kuwa na ukaribu na rais wa Russia, Vladimir Putin, serikali ya Uingereza imeamua kumuwekea vikwazo na hata kuzuia biashara na mali zake baada ya taifa hilo la Mashariki kuivamia Ukraine kinyume na sheria za kimataifa ambazo zilizuia nchi moja kuivamia nyingine kimabavu baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia.

Kutokana na siasa za kimataifa, ni vigumu kwa sasa nchi nyingine kwenda kuisaidia Ukraine kwa kutuma majeshi kwa kuwa inaweza kuwa hatari duniani, hivyo njia pekee ya kuiweka Russia katika hali ngumu ni kuiwekea vikwazo, kuiondoa katika mfumo wa kifedha wa kimataifa, kuwatenga watu walio karibu na serikali ya Kremlin na vikwazo vingine kadha wa kadha.

Hatua hiyo ya serikali ya Uingereza imefuatiwa na kampuni kadhaa pia kujiondoa katika udhamini, hali kadhalika washirika wengine wa Chelsea katika mkakati wa kutaka taasisi hiyo ya Mrussia isinufaike kibiashara wakati maelfu ya watu wanafariki nchini Ukraine kutokana na uvamizi wa Russia.

Jambo hilo limekuja siku chache baada ya kampuni ya uwekezaji ya Saudi Arabia kukamilisha mpango wa muda mrefu wa kuinunua Newcastle United. Mpango huo ulichukua muda mrefu kutokana na klabu 19 zinazoshiriki Ligi Kuu kuipinga kampuni hiyo ya serikali kwa madai kadhaa yakiwemo ya Saudi Arabia kukiuka haki za binadamu kama tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanahabari Kashogi.

Suala hilo lilichafua siasa za Uingereza na likawa kete kwa waziri mkuu wa sasa, Boris Johnson ambaye aliahidi angehakikisha mpango huo unafanikiwa baada ya kukwama miaka mitatu iliyopita. Lakini litavurugika iwapo Saudi Arabia itaingia katika kashfa nyingine ya ukiukwaji haki za binadamu. Mbali na Abramovich, mabilionea wengine sita wa Russia wanaotuhumiwa kuwa washirika wa karibu wa Putin pia wamewekewa vikwazo, lakini kwa kuwa hawajihusishi na soka, hilo halituumi.

Sitaki kuingia ndani sana kuchambua suala hilo, bali kuangalia somo ambalo tunalipata katika sakata hilo hata kama tuko katika dunia ya tatu ambayo haijafikiria kuwa na sheria na kanuni kama hizo zisizo za kimichezo lakini zinapofanya kazi zinaathiri michezo.

Habari hizo mbili za Abramovich na Newcastle United zinazungumzia usafi wa watu wanaojitokeza kuwekeza katika michezo na si kwa sababu ya rangi zao au utaifa wao.

Kutokana na umaarufu wa mchezo wa soka, wafanyabiashara wa kila aina wanataka kuingia kuwekeza hasa katika soka la Uingereza ambalo limefanikiwa sana kutangaza chapa yake kiasi cha kuvutia watu wa mataifa mbalimbali.

Usingetegemea mfanyabiashara kutoka nchi kama Russia, China, Qatar au Saudi Arbia kununua hisa za umiliki wa klabu nchini Uingereza au Ufaransa, lakini ndivyo ilivyo. Kampuni zenye utajiri mkubwa kutoka mataifa hayo na Marekani zinamiminika Ulaya kununua klabu.

Lakini wenzetu wamejiwekea misingi ya ufanyaji biashara. Kwamba mwekezaji asijihusishe na aina yoyote ya ufisadi, ukiukaji wa haki za binadamu, kukumbatia siasa chafu na asikiuke mambo mengine ya kimaadili. Haya ni mambo ambayo wenzetu wanazingatia sana. Hawatangulizi mbele fedha, bali usafi wa mwenye fedha ndio kipa umbele cha kwanza.

Hii ni kwa lengo la kuzifanya klabu zisitetereke kunapotokea matatizo ya kisiasa kama ilivyo kwa Abramovich au kuzizuia kuingia makubaliano na mtu ambaye rekodi zake si nzuri na hivyo wakati wowote anaweza kuingia matatizoni na kuyumbisha klabu kiuchumi.

Najua huko ni mbali, lakini kuna mengi ya kujifunza katika sakata la Ukraine, hasa wakati huu ambao klabu zetu zinasema zinataka zibadilishe mfumo wa umiliki ili wawekezaji binafsi waingie.

Lakini Yanga ilishaonja machungu hayo wakati Yusuf Manji alipoingia katika mgogoro na serikali.

Columnist: www.tanzaniaweb.live