Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Rustenburg, ni Yanga dhidi ya Yanga yenyewe

Majukumu Yanga Mastaa wa Yanga

Wed, 17 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sijakosea. Ni kweli. Ni Yanga dhidi ya Yanga yenyewe. Nipo Afrika ya Kusini kujaribu kutazama kama Yanga wataweza kujivua gamba wenyewe. Majuzi wametoka kuchukua ubingwa wa 29 wa Ligi kuu ya Tanzania. Sio habari mpya. Kabla ya hapo si walishafanya mara 28?

Walifanya akina Sunday Manara miaka hiyo. Walishafanya akina Ahmed Amasha miaka hiyo. Walishafanya akina Athuman China miaka hiyo. Wakafanya akina Edibily Lunyamila. Wakaja wengine wakafanya. Mpaka juzi akina Fiston Mayele na genge lake wamefanya hivyo. Sio habari mpya sana.

Nadhani hata kocha, Nasreddine Nabi anajua kwamba kuna watu walishafanya mara 27 kabla yeye hajawa kocha wa Yanga. Hata Rais wao, Injinia Hersi Said anajua kwamba kuna watu walishafanya mara nyingi hapo awali. Wakati mwingine labda ni tofauti ndogo tu ya namna ya kufanya, lakini hiki kitu kilishafanywa.

Kitu pekee ambacho hakijawahi kufanywa ni hiki walichofanya baada ya kuifunga Rivers United ya Nigeria. Kwenda nusu fainali yao ya kwanza katika michuano mikubwa ya CAF ni kitu ambacho hawakuwahi kufanya huko nyuma tangu timu yao ianzishwe siku ile ya Februari 1935.

Na baada ya hapo tayari wamecheza mechi ya kwanza dhidi ya Marumo Gallants pale Temeke na kushinda mabao mawili ya Aziz Ki na Bernard Morrison. Sasa ni muda wa kumaliza kazi kwa kwenda fainali. Itakuwa fainali yao ya kwanza CAF na hakuna ambaye amewahi kufanya katika historia ya klabu yao.

Hapo ndipo ninapomaanisha hili ni zaidi ya pambano la soka kwao. Ni Yanga dhidi ya Yanga. Ni kundi kubwa la Yanga la sasa linalojaribu kufanya jambo kubwa dhidi ya makundi makubwa mengine ya zamani ya Yanga yaliyowahi kuitawala Yanga hapo zamani kuanzia kwa viongozi, mabenchi ya ufundi, wachezaji mahiri tunaosimuliwa na wale ambao tumewahi kuwaona.

Tayari kizazi cha sasa cha Yanga kimeshaingia katika historia ya klabu kwa kutinga nusu fainali, lakini ni afadhali waimalizie hadithi hii ta kusisimua kwa kwenda fainali kabisa. Litakuwa jambo jema kwao. Ni taadhari tu kisije kizazi kingine ambacho kitakuja klabuni hapo na kumalizia kazi huku wakiibuka na majina makubwa kuliko hawa wa sasa katika ngazi zote.

Tayari Yanga wamefanya jambo la maana kwa kuwasili Afrika Kusini mapema. Baridi iliyopo hapa sio ya kawaida. Kwa wachezaji ambao hawajawahi kucheza katika mazingira ya baridi inaweza kuwasumbua lakini nawatazama usoni na kwa majina yao yenye uzoefu naamini kwamba wengi wameshazoea kucheza katika mazingira haya.

Kitendo cha kutua katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo jijini Johannesburg na kuchukua Basi ambalo moja kwa moja liliwapeleka katika mji wa Rustenburg kilomita 133 kutoka Johannesburg nadhani pia kilikuwa cha busara. Jiji la Johannesburg lina mambo mengi.

Mji wa Rustenburg ni mdogo na wenye utulivu mkubwa tofauti na Johannesburg ambako kuna Watanzania wengi lakini pia hakuna utulivu rafiki kama vile ilivyo Rustenburg. Yanga watakuwa na mazingira mazuri ya kujiandaa na pambano hili lenye umuhimu zaidi katika historia yao.

Ndani ya uwanja bado pia linabakia kuwa pambano la wenyewe dhidi ya wenyewe. Yanga dhidi ya Yanga. Unawezaje kupoteza uongozi wa mabao 2-0 katika hatua kama hizi? Itashangaza kidogo. Kitu kizuri ni kwamba katika benchi wana Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze. Wote wanaonekana kujua jambo wanalofanya.

Mpaka hapa walipofika ambapo wamechukua ubingwa wa Ligi Kuu, wamefika nusu fainali ya Shirikisho CAF pamoja na Shirikisho Azam ni kwa sababu wanajua wanachokifanya. Sio rahisi kuwakosoa katika mambo mawili ambayo yanahusu mechi. Kwanza kabisa huwa wana mpango maalumu na mechi iliyopo mbele yao. Inaitwa Game plan.

Lakini pia tunajua kwamba wana uwezo mkubwa wa kubadilika kadri mechi inavyoendelea. Haishangazi kuona wakati mwingine tumeshuhudia Yanga ikiwa timu tofauti uwanjani katika kipindi cha pili baada ya mabadiliko fulani wakati wa mapumziko.

Mpaka sasa hatujui mpango kazi wa Nabi utakuwa upi uwanjani baada ya kuongoza kwa mabao mawili Dar es salaam. Yanga watajilinda au watajaribu kuumiliki mchezo au kujaribu kushinda mechi tena? Mwenyewe anakiri kwamba hakufurahishwa na pambano la kwanza licha ya kwamba alishinda.

Ni kweli. Marumo walimiliki mechi vizuri ingawa Yanga walishinda mechi. Yanga wanaweza kumiliki mchezo kama walivyofanya dhidi ya Rivers ugenini? Sijui. Ninachojua ni kwamba Marumo ni timu nzuri uwanjani kuliko Rivers na Yanga wana mechi ngumu mkononi.

Kupita kwa Yanga kutahitaji bao la ugenini zaidi. Kutanua uongozi litakuwa jambo jema kuliko kujilinda. Bahati nzuri tangu Yanga wanaanza mechi yao ya kwanza msimu huu katika michuano yote hakuna mahala ambapo walijilinda. Wanacheza na kiburi kwamba wanaweza kupata matokeo kokote ambako watakwenda. Ina wachezaji wa namna hiyo. Wachezaji ambao wanajiamini kwamba wapo katika ubora wao na wanaweza kushinda mechi yoyote ya soka ambayo wanaingia uwanjani. Kuanzia wale wanaoanza pambano hadi wale ambao wataanzia katika benchi.

Hata hivyo Nabi inabidi awe makini na kasi ya Marumo. Kuna umuhimu mkubwa wa ushirikiano kati ya wachezaji wa mbele na wale wa nyuma. Marumo walikosa mabao kadhaa ya wazi katika pambano lililopita na haionekani kuwa timu ya kubezwa. Kichapo cha mabao mawili, hasa bao la pili la Bernard Morrison kilitokana na tamaa yao ya kuhakikisha wanaondoka Dar es salaam na mabao au bao.

Yanga inabidi icheze kwa tahadhari kubwa kuliko ilivyofanya katika pambano la awali la uwanja wa Taifa. Nabi anajua zaidi. Kwa hiki anachofanya kwa sasa ametukosesha uhalali wa kumkosoa mara kwa mara. Maamuzi yake mengi yanakuwa sahihi kuhusu mkakati wa mechi. Nadhani anajua kwamba Marumo walistahili kuambulia chochote katika pambano lililopita.

Fikiria namna ambavyo wataingia uwanjani kama chui waliojeruhiwa. Wana msimu mbovu katika Ligi kuu ya hapa Afrika Kusini. Akili yao yote wameipeleka Shirikisho. Na hii ni mechi ya machozi, jasho na damu kwao. Wanahitaji kwenda fainali na ikiwezekana kuchukua ubingwa kwa sababu ni sehemu pekee ambayo wanatetea roho yao

Columnist: Mwanaspoti