Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Roy Keane anapotutanguliza vita ya Haaland na Mbappe

Mbappe With Haaland Roy Keane anapotutanguliza vita ya Haaland na Mbappe

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

“Magoli ni kama wanawake, kila moja ni zuri”. Aliwahi kusema hivi mhuni mmoja wa Kifaransa aliyeitwa Eric Cantona. Na mwisho wa siku mchezo wenyewe huwa unahukumiwa na mabao.

Ni hapo hapo ambapo mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ aliwahi kutuambia kwamba mchezo wa soka ni mabao. Haijalishi mchezaji amecheza vipi au timu imecheza vipi lakini kitu muhimu katika mchezo ni mabao. Haya ndio huwa yanaamua mechi.

Amenifikirisha kitu tofauti staa wa zamani wa Manchester United, Roy Keane. Wikiendi ile ambayo Manchester City walikuwa wanacheza na Arsenal alikuwa mchambuzi. Kama kawaida yake akaweka utata. Kwamba? Eti Erling Haaland alikuwa anacheza kama mchezaji wa daraja la tatu pale England.

Kwamba achilia mbali uwezo wake wa kufunga mabao, lakini katika mchezo wa kawaida Haaland hana ubora na anacheza kama mchezaji wa daraja la tatu. Nikajikuta nina mambo mawili kichwani. Bado Keane ana ugomvi na familia ya Haaland? Sidhani. Iliwahi kutokea zamani Keane alichezewa rafu na baba yake Haaland, Alfred Inge Haaland.

Ilikuwa ni katika pambano la Leeds dhidi ya Manchester United. Akaumia akakaa nje kwa muda mrefu. Baba yake Haaland akahamia Manchester City. Wakakutana tena na Keane akamchezea rafu mbaya Alf Inge Haaland. Ilikuwa ni kisasi cha miaka mingi. Akaiweka hiyo habari katika kitabu chake, akafungiwa kucheza soka kwa mechi 12.

Na sasa ametia neno kuhusu uwezo wa Haaland kwa namna anavyocheza nje ya mabao. Kauli yake imeweka utata mkubwa huku kukiwa na hisia tofauti kutoka kwa wachambuzi lakini kocha wa Haaland, Pep Guardiola akisisitiza kwamba Haaland ndiye mshambuliaji bora zaidi duniani. Tukiachana na hilo, je Keane amesema kweli kuhusu Haaland? Inawezekana. Lakini Keane ametutanguliza katika mjadala wa nani bora kati ya Haaland au Kylian Mbappe. Ungemchukua nani katika timu yako? Kwa zaidi ya miaka 15 tulikuwa tukielea katika mjadala wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kwa sababu mbalimbali.

Hatuna muda mrefu tutakuwa tunabishana zaidi kuhusu Mbappe na Haaland. Watu mbalimbali wamekuwa wakiulizwa kuhusu ungemchukua nani kati ya Mbappe au Haaland. Wapo wengi wanaokwenda kwa Mbappe kwa sababu ana mambo mengi katika miguu yake. Ana kasi, uwezo wa kupiga chenga na kufunga. Swali ni kama atazidiwa uwezo wa kufunga na Haaland itakuaje.

Ni kweli Keane kasema kweli, lakini dunia inajitaji mabao. Dunia imepotelewa na watu wa mbele wanaoweza kusimama pale mbele na kuuweka mpira katika nyavu. Sio wote wanaoiweza kazi hii. Haaland anaiweza kwa ufasaha. Ungechagua lipi, awe anaiweza kwa ufasaha na kucheza kama mchezaji wa daraja la tatu au awe haiwezi kwa ufasaha lakini anacheza vyema uwanjani. Katika hali ya kawaida kuna wakati utamhitaji Mbappe, katika hali ya kawaida kuna wakati utamhitaji Haaland. Sidhani kama Keane alikuwa sahihi kwa sababu mwisho wa siku haijalishi unachezaje, ukiwa mshambuliaji inabidi uuweke mpira katika nyavu.

Lakini kama maoni ya Keane yakizingatiwa basi tutegemee kuona Mbappe akimburuza Haaland kwa muda mrefu wa maisha yao ya soka. Mbappe ana mambo mengi. Ana kasi lakini pia anaweza kubishana na Haaland katika mabao ingawa bado katika kufunga sidhani kama ataweza kufika katika kiwango cha Haaland. Haaland alizaliwa kwa ajili ya kufunga. Lakini pia kwa hili lililosemwa na Keane bado inamaanisha Haaland atakutana na vita nyingi mbele yake. Kuna mtu anaitwa Vinicius Junior naye ni moto. Haaland anaweza kuwa anafunga zaidi yake lakini bwana mdogo ana mambo mengi uwanjani kuliko Haaland. Ni hadithi ya Thierry Henry na Ruud Van Nistelrooy. Katika ubora wao, Ruud alikuwa anafunga zaidi kuliko Henry lakini Henry alikuwa na mambo mengi uwanjani kuliko Ruud. Wengi wangependa kumchukua Henry mbele ya Ruud ambaye alijulikana kama mwizi wa mabao.

Hata Ronaldo na Messi wametofautishwa kwa namna hii. Ronaldo anafunga mabao mengi kuliko Messi lakini ndani ya Messi kuna mambo mengi. Ukokotaji wa mpira, pasi za mwisho pamoja na mambo mengine. Ronaldo hamuwezi Messi kwa mambo mengi kama mchezaji ingawa anamzidi mabao. Lakini hata hivyo inachanganya kidogo kwa sababu wakati mwingine kuna wachezaji bora ambao hawakuwahi kuzingatiwa ubora wao kwa sababu hawakufunga mabao mengi. Hawa ndio kina Andrés Iniesta, Kevin De Bruyne na wengineo. Zama za leo imekuaje De Bruyne hajawahi kuwa hata mchezaji bora wa msimu? Tusubiri kumuona Haaland akiwa na Manchester City yake huku Mbappe akielekea Real Madrid. Watakuwa na vita yao fulani lakini Haaland atalazimika kufanya kazi ngumu mbele ya Mbappe kutokana na hiki ambacho Keane amekisema. Hata hivyo haiondoi umuhimu wa mabao yake uwanjani.

Mtihani mwingine wa Haaland kwa Mbappe ni mataifa yao. Wakati Mbappe anacheza kikosi cha Ufaransa kilichosheheni mastaa, Haaland anacheza Norway ambayo ina kina Martin Odegaard tu. Fikiria tu kwamba hata katika michuano ya Euro mwaka huu Haaland atakosekana huku Mbappe akiwa na nafasi ya kuchukua taji.

Columnist: Mwanaspoti