Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ronaldo haamini kama jua limezama magharibi

EDD3D423 1991 44EC 9C19 E5BD027460A3.jpeg Cristiano Ronaldo

Sun, 23 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwisho wa kila siku njema au mbaya, jua huwa linazama upande wa Magharibi. Linaacha rangi nzito ya kupendeza. Njano iliyochanganyika na nyekundu. Haijalishi ni siku uliyopokea habari ya msiba, haijalishi kama ulipokea habari ya kushinda mabilioni ya pesa za bahati nasibu. Jua huzama.

Wapo watu wachache wanaokataa kuzama kwa jua. Mmojawapo ni Cristiano Ronaldo. Maisha yake ya mpira ni kama jua lililochomoza Mashariki kwenda Magharibi. Miezi michache iliyopita ilithibitika Ronaldo ni jua linalozama. Bahati nzuri kwake alikuwa na siku nzima. Alikuwa na maisha mazuri katika soka.

Bahati mbaya hataki kuamini kwamba jua limezama au linazama. Wikiendi iliyopita, Mbinafsi kama alivyo, Ronaldo alitolewa na kocha wake, Erik Ten Hag katika pambano dhidi ya Newcastle United pale Old Trafford.

Alichofanya ni kutikisa kichwa kwa kutoamini. Ni kana alikuwa anafanya kazi za maana uwanjani na kocha alikuwa amekosea. Watu wa United waliungana mkono na Ten Hag. Ronaldo huyu sio yule. Wote tunafahamu lakini ni yeye mwenyewe tu ndiye ambaye hafahamu.

Kutikisha kichwa ilikuwa ni kumshtakia Ten Hag kwetu? Nadhani. Lakini kama alidhani Ten Hag alikuwa amekosea basi labda kama angefanya hivyo miaka saba iliyopita. Uwanja wote wa Old Trafford ungezomea na kumshangaa. Lakini leo hatumshangai Ten Hag. Ronaldo wa leo sio wa zamani.

Jumatano usiku ilikuwa siku nyingine ambayo tulimshangaa Ronaldo kwanini hataki kukubali jua limezama. Ten Hag hakumpanga katika pambano dhidi ya Tottenham. Hakumpanga wala kumuingiza baadaye. Akaingiza wachezaji wengine.

Kulikuwa na mambo mawili. Inawezekana alitaka kumuonyesha Ronaldo kwamba bosi ni nani kati yake na yeye. Lakini pia inawezekana alifanya hiki cha pili ilikuwa ni mechi yenye kasi na ambayo ilihitaji nguvu ambayo hauwezi kuipata kwa mchezaji ambaye Februari 5 mwakani anatimiza miaka 38.

Bahati nzuri Ten Hag alipatia. United ilicheza mpira mkubwa ambao hawajawahi kucheza tangu msimu huu uanze. Antonio Conte alikimbizwa hasa na fomesheni yake mbovu ya kujilinda. United ilishinda mabao 2-0 na kipa wa Spurs, Hugo Lloris alikuwa mchezaji bora uwanjani.

Baada ya kumaliza mabadiliko yake uwanjani, Ten Hag na mashabiki wa soka duniani kote walimshuhudia Ronaldo akizira na kuondoka uwanjani katika dakika ya 89. Sijui alikuwa anawahi kuondoka uwanjani ili aende wapi?

Kwanza ni ukosefu wa heshima kwa benchi la ufundi na wachezaji wenzake. Ukosefu wa adabu. Ronaldo haoni kama anastahili kutolewa, na wala haoni kama anastahili kutopangwa mechi nzima. Pengine ni wakati sahihi wa kumtafutia mikanda yake ya zamani na kumuonesha yeye alikuwa nani zama zake.

Sidhani kama Ronaldo ni mkweli wa nafsi yake. Angekuwa mwanadamu mkweli nadhani hakupaswa kufanya haya anayoyafanya. Kitu cha kwanza anamuweka kocha wake katika wakati mgumu. Anamuweka kocha wake katika mawazo ya kumridhisha Ronaldo hata kama anamuona hafai uwanjani.

Bahati nzuri Ten Hag anaonekana kuwa imara. Anafanya kitu kwa ajili ya timu na sio kumridhisha Ronaldo. Baada ya Ronaldo kusikitika sana wakati anatolewa katika pambano dhidi ya Newcastle kocha mwingine angeweza kumridhisha kwa kumpanga au kumuingiza katika pambano dhidi ya Spurs. Ten Hag hakufanya hivyo. Alimtoa kabisa katika kikosi kilichocheza jana dhidi ya Chelsea. Ten Hag ni imara.

Ukweli hapa Teg Hag nadhani hakumuihitaji Ronaldo tangu mwanzo wa msimu. Labda matajiri wa United ilimuhitaji kwa sababu za kibiashara lakini ukweli kwa mpira wa kisasa au mpira ambao Ten Hag anaweza kuuhitaji katika kuisuka United mpya sidhani kama wanamuhitaji mchezaji anayekaribia miaka 38 hata kama ana uwezo wa kufunga mabao. Mpira wa kukaba kila mahali, kukimbia na mpira kwa kasi kila mahala, sidhani kama Ronaldo anauweza kwa sasa. Labda kama angekuwa anaichezea Manchester United iliyokamilika tungeweza kusema anaweza kupumzika ndani ya uwanjani. Kwa sasa United ndio kwanza inajitafuta.

Nafahamu Ten Hag lazima atakuwa anataka kuifanyia United kile ambacho Mikel Arteta anaonekana kuifanyia Arsenal. Anataka kuipa mwanzo mpya. Na ndio maana siamini kama alimuhitaji Ronaldo tangu katika dirisha kubwa lililopita.

Kwa upande wa Ronaldo kuna mambo mawili. Kwanza kabisa lazima akubali kwamba kama anataka kucheza kwa raha na kupangwa kila wikiendi basi Ligi Kuu ya England sio mahala kwake. Labda atafute ligi ambayo haina upinzani kwa sasa. Kwa jina lake lilivyo anaweza kuendelea kuchuma mamilioni ya dola akiwa Qatar, Saudi Arabia au Marekani.

Lakini pia awe makini katika kutochafua jina lake na heshima yake Old Trafford ambayo ameijenga kwa muda mrefu. Mashabiki wa United hawawezi kukubali hali hii. jaribu kufikiria namna alivyofanya juu chini kuutia dosari ushindi mtamu ambao United iliupata dhidi ya Spurs.

Wakati vyombo vya habari vilitazamia kuandika kwa urefu namna ambavyo Ten Hag alimzamisha Conte, wao wakajikuta wakijadili kwa muda mrefu tukio la Ronaldo kuondoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika. Kifupi Ronaldo alituondoa uwanjani akatuweka katika himaya yake. Mwisho wa siku nadhani Ronaldo anaweza kuondoka zake Trafford Januari. Pande zote mbili zitakubaliana ukweli Ten Hag atamuona Ronaldo anamuharibia utulivu klabuni, wakati huo huo Ronaldo ataona hawezi kuvumilia benchi.

Kitu kitakachokera ni ukweli Ronaldo alipaswa kuondoka kwa heshima Old Trafford. Wenzake walipokaribia mwisho wa maisha yao pale Old Trafford waliondoka kwa amani kabisa. Hawakuvuruga hali ya hewa kwa kulazimisha kutaka kupangwa kwenye michezo ya Man United hata kama kasi yao ilionekana kupungua uwanjani.

Columnist: Mwanaspoti