Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Rekodi zasimama upande wa Mgunda Simba SC

Mgunda Kocha Juma Mgunda

Sat, 15 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Namba hazidanganyi! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kinachofanywa na Juma Mgunda, tangu alipokabidhiwa kikosi cha Simba Septemba 7 akimpokea Zoran Maki aliyetimkia Al Ittihad ya Misri.

Uteuzi wa Mgunda kutoka Coastal Union awali ulitajwa ni wa kuokoa jahazi la kuisimamia timu kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.

Kazi aliyoifanya kwenye mchezo huo na mingine imemfanya kuwafunga midomo waliouponda uteuzi wake, kwani namba zinambeba na kuwafunika baadhi ya makocha wa kigeni walioinoa timu hiyo.

Licha ya muda mchache Simba imebadilika kiuchezaji tofauti na kipindi cha nyuma licha ya wachezaji kuwa wale wale ambao kandanda lao lilikuwa halivutii licha ya kushinda michezo yake.

REKODI TAMU

Tangu Mgunda aanze dhidi ya Nyasa Big Bullet ugenini na kushinda 2-0, kisha Simba ikacheza Ligi Kuu Bara na kuvunja mwiko kwa Tanzania Prisons kwa kuwachapa bao 1-0.

Iliporudiana na Big Bullets jijini Dar, ikashinda tena 2-0 na timu kufuzu raundi ya kwanza na baadaye ikacheza Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda mabao 3-0.

Baada ya hapo ikaenda kambini visiwani Zanzibara na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Malindi na kushinda 1-0, kisha kuipasua Kipanga mabao 3-0 na kusafiri hadi Luanda nchini Angola kuvaana na Primeiro de Agosto katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Afrika.

Kama ilivyofanya kwa Wamalawi, Simba ya Mgunda ikaikandamiza Agosto mabao 3-1 na kufanya iecheze mechi mechi tano za mashindano na mbili za kirafiki kushinda zote na kufunga mabao 15, yakiwamo 11 ya kimashindano na kuruhusu bao moja pekee dhidi ya Agosto.

Rekodi hizo zimafanya waliompinga Mgunda kumkubali kidogo safi na mwenyewe amefunguka, katika maisha yake anamwamini na kumtanguliza Mungu ili aweze kufikia malengo na bahati nzuri ndani ya Simba amekutana na wachezaji wenye uwezo na uelewa mkubwa wa kunasa mbinu zake.

“Simba ni timu kubwa kila mtu anayeingia kuitumikia lazima ujipange, naamini tutafanya vizuri kwa ushirikiano na wachezaji na viongozi wetu,” anasema nyota huyo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyetamba na Coastal Union na kubeba nao ubingwa wa Bara mwaka 1988.

Rekodi hizo zimefunika baadhi ya makocha wa kigeni walioajiriwa kwa gharama kubwa Msimbazi wakiwamo waliorodheshwa hapa chini;

PABLO FRANCO

Licha ya Simba kukosa ubingwa msimu 2021/22 uliotwaliwa na Yanga Kocha Pablo Franco alishindwa kutimiza malengo yake kimkataba ya kuifikisha timu nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilitolewa katika michuano hiyo na Gwaneng Galaxy baada ya kushinda ugenini mabao 2-0 na ilipoteza nyumbani kwa mabao 3-1 na kuangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo ilifika robo fainali na kutolewa na Orlando Pirates.

Kwa upande wa ligi, Pablo naye alipata ushindi wa mechi mbili akishinda 3-1 na 2-1 na kukusanya pointi sita na mabao matano na kufungwa mawili.

ZORAN MAKI

Huyu kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi Simba, siku 67, licha ya muda mchache lakini alisifika kwa ukali uliosababisha baadhi ya wachezaji kukosa morali naye.

Mechi zilizochezwa chini yake nyingi ni za kirafiki, ikiwamo zile za pre-season nchini Misri kabla ya kwenda Sudan aliposhinda 4-2 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na kupasuka 1-0 kwa Al Hilal kisha na iliporudi nchini ilicheza tena kirafiki na Arta Solar 7 na Simba kulala tena 1-0 na katika ligi, Zoran alicheza mechi mbili akiiongoza Simba kushinda 3-0 dhidi ya Geita Gold kisha kuifumua Kagera Sugar kwa mabao 2-0 na hivyo naye kukusanya pointi sita na mabao matano, bila wavu wake kuguswa kabla ya kujiuzulu Septemba 6 wakati timu ikijiandaa kwenda kucheza na KMC iliyosimamiwa na msaidizi wake, Seleman Matola na kumaliza kwa sare ya 2-2.

DIDIER GOMES

Huyu aliondolewa Simba baada ya kikosi chake kushindwa kutinga nusu fainali Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilitolewa na Kaizer Cheafs ya Afrika Kusini katika hatua ya robo fainali iliyofanya kocha huyo Mfaransa kufungashiwa virago, lakini alama ameiacha ya kuipa timu hiyo taji la msimu 2020/21. Kwa upande wa ligi, Gomes katika mechi mbili za awali alipata pointi nne alishinda 2-1 akatoka 2-2 na kuachwa nyuma na Mgunda ameliyeshinda mbili na na kukusanya pointi sita na mabao manne, bila wavu wake kuguswa.

SVEN VANDENBROECK

Aliipa Simba mataji ya matatu msimu 2019/20 na msimu 2020/21 akaiacha timu hatua ya makundi na kusepa zake. Licha ya rekodi hiyo, lakini amezidiwa kimahesabu na Mgunda katika mechi zake za kimataifa na za Ligi. Sven ndiye aliyetisha kwenye mechi mbili za awali akiwa na Simba kwani alishinda 4-0 na 2-0 na kuklusanya pointi sita kama Mgunda, lakini akivuna mabao sita na wavu wake kutoguswa kama ilivyo kwa Mgosi.

PATRICK AUSSEMS

Mbelgiji Patrick Aussems ‘Uchebe’ aliipeleka makundi Simba kwa mara ya kwanza dhidi ya Nkana ya Zambia mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Mbali na kuweka historia hiyo pia aliipa timu hiyo mataji mawili ya Ligi Kuu msimu wa 2018/19 na msimu wa 2019/2020, kuondolewa kwake Simba ilitokana na tabia yake ya kuwapa uhuru zaidi wachezaji. Katika ligi Aussems alishinda mechi mbili za awali za ligi akishinda 1-0, kisha 2-0 na kukusanya pia pointi sita na kufunga mabao matatu bila wavu wake kuguswa kama Mgunda.

WASIKIE WADAU

Kenny Mwaisabula mchezaji wa zamani sasa ni kocha anasema, mafanikio yanatokana na makocha wazawa hao wageni wanapewa nafasi kubwa bure.

“Wampe nafasi ambayo wanapewa wazungu wampe kila kitu, kuanzia mshahara kama ambao wageni wanalipwa waone atakavyoifikisha timu,”

“Mfano Israel Mwenda alivyobadilika muone Chama anafanya kila kitu anashambulia, anakaba na kufunga na kuna mabadiliko ya wachezaji wanaonekana kuwa na furahana kocha wao.’’

“Waswahili hatupendani kitendo cha Simba kumpa heshima Mgunda wengine kinawauma lakini nawapongeza sana viongozi ni jambo jema wamefanya tuwaamini wazawa.

Kessy Mziray aliyewahi kukinoa kikosi cha Alliance FC anasema, tatizo la Watanzania hawataki kuamini vya kwao wakati vipo vizuri zaidi ya hao wageni.

“Binafsi namuona mbali sana Mgunda endapo watamuamini na kumpa timu sina shaka naye hata kidogo anajua namna gani ya timu icheze kwa wakati gani,’’ anasema. Abdallah Kibadeni anasema Simba ilichelewa kumpata Mgunda kwani uwezo wake ni mkubwa na hata mabadiliko ya timu yanaonekana.

“Wapo wazawa wengine kama Fredy Felix ‘Minziro’ wana uwezo sana wapewe nafasi lakini kwa Simba hii Mgunda ndiye wa kuandika historia ya kuifikisha timu mbali zaidi ya hao makocha wengine waliopita na yeye ndiye wa kutuokoa wazawa,’’anasema Kibadeni.

Kibadeni anasema Seleman Matola anatakiwa kumsaidia vilivyo Mgunda waaminiwe wapewe timu wanaweza kuifikisha mbali timu.

WACHEZAJI SHANGWE

Baadhi ya wachezaji wa Simba (Majina tunayo) ambao wameonekana kumuelewa Mgunda wakimuhita ‘Father’ na Matola ‘Brother’.

“Mgunda ni zaidi ya kocha sisi wachezaji tunamkubali na tunafurahia kufanya nae kazi, ni kama baba ukikosea anakuonya yanaisha maisha yanaendelea tunamuelewa sana,’’kauli ya nyota Simba.

Mgunda mbali nakuwanoa Wagosi naSimba amewahi kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ hivyo uzoefu wake ni mkubwa katika soka.

Columnist: Mwanaspoti