Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Rafiki yangu Magoma amenikumbusha mwaka ‘47’

Mama Fatma X Magoma Rafiki yangu Magoma amenikumbusha mwaka ‘47’

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 2003 pale Nairobi niliingia night club moja na rafiki yangu aliyeitwa Jonnie. Alikuwa msanii maarufu wa Hip Hop Kenya nyakati hizo akiliwakilisha kundi maarufu la Kalamashaka. Tulienda kustarehe tu.

Ghafla akaanzisha ugomvi ambao sikuona kama una mbele wale nyuma. Hakukuwa na sababu yoyote ya kufanya alichokifanya. Wakati tunarudi mtaani kwetu maeneo ya Dandora, usiku wa manane, nilimuuliza kwa nini alianzisha ugomvi ule.

Jibu lake lilikuwa kichekesho. Aliniambia; “Hakukuwa na sababu, lakini wanaume lazima tugombane disko.” Niliishia kucheka naye akacheka. Mara nyingi huwa nakumbuka tukio lile. Wakenya ni watu wakorofi. Lakini hata Tanzania tuna watu wetu wakorofi.

Miaka 21 baadaye nimemkumbuka tena rafiki yangu, Jonnie baada ya majuzi kulitazama sakata aliloanzisha rafiki yangu mwingine, Juma Ally Magoma. Mzee na Komandoo wa Yanga. Kumbe alikuwa na kesi mahakamani akipigania jambo fulani kuhusu wadhamini wa Yanga. Au tuseme kuhusu klabu yake. Au tuseme kuhusu Katiba Mpya wa Yanga.

Rafiki yangu Magoma ana historia ndefu ya ugomvi ndani ya Yanga. Ni wale watu ambao wakienda disko lazima wakagombane tu. Ili mradi tu. Hakuna sababu ya msingi sana, lakini kwa nini tuishi kwa amani? Ndivyo alivyo rafiki yetu. Watu wa namna hii wanapatikana kila mahala.

Kwa mfano. Wakati watu wanapambana kuijenga Yanga mpya baada ya awali kupitia katika msoto baada ya tukio la kuwekwa ndani kwa mfadhili wao wa zamani, Yusuf Manji, watu wengi wa Yanga walikuwa wameamua kukaa chini na kukubaliana walihitaji uelekeo mpya.

Akajitokeza Ghalib Said Mohamed maarufu kama GSM. Akaamua ilikuwa imetosha kwa Yanga kujiendesha kwa kutembeza bakuli kama ambavyo ilikuwa inafanywa. Muda mwingi wakati huo wa njaa hata nahodha Ibrahim Ajibu na kocha wake, Mwinyi Zahera walikuwa wanahusika.

Inawezekana kulikuwa na mapungufu fulani katika mchakato mzima, lakini Mzee Magoma ni wale wazee ambao hawawezi kukaa mezani na kutoa michango yao kwa njia za amani kabisa. Alijificha alikojificha ili baadaye aibue zogo.

Unadhani ilikuwa mara yake ya kwanza? Hata utawala wa Manji alikuwa akiwasumbua kwa njia hizi hizi tu. Kuna namna ambavyo Manji aliunganisha kambi mbili za wazee ambao zilikuwa na ugomvi wa kila siku. Yanga Asili na Yanga Kampuni. Rafiki yangu alipoona makubaliano yanaweza kufikiwa akaamua kukaa kando peke yake ili azushe zogo.

Baada ya kila kitu ambacho kimeendelea pale Jangwani, rafiki yangu kumbe alikuwa anaandaa zogo lake. Amefanikiwa kuiteka nchi katika hoja ambazo zingeweza kuwekwa mezani zikatatulika kwa urahisi tu. Haya yanafanyika huku akiwa hajali sana kinachoendelea Jangwani.

Kwamba wadhamini mbalimbali wameona Yanga ina amani ndiyo maana wanatia mabilioni ya pesa katika udhamini, hiyo siyo habari yake. Kwamba Yanga imefika fainali za Kombe la Shirikisho, hiyo siyo habari yake. kwamba Yanga kwa sasa inatumia mabilioni kusajili wachezaji mahiri, hiyo siyo shughuli yake. Kwamba Yanga ipo kambini Afrika Kusini, hiyo siyo habari yake. Kitu cha msingi ni lazima tugombane.

Siku hizi kuna vyombo vingi vya habari. Baada ya ustaa wake wa ghafla kuna vipaza sauti vinakesha nyumbani kwake. Nikacheka katika mambo mawili kati ya mengi ambayo amekuwa akihojiwa. Kuna mahala anasema haiwezekani Yanga ikawa ya watu wachache.

Moja wa mfano wake ukawa, uwakilishi wa wanachama katika mkutano mkuu unabagua. Kila tawi linatoa watu watatu katika kundi la watu 95 hadi 100. Rafiki yangu Magoma angependa wanachama wote wahudhurie mkutano.

Kwa umri wake anaruhusiwa kuwa na mawazo haya ya kizamani. Mawazo ya kutaka kila mwenye kadi awe mkutanoni. Ni kama vile ambavyo katika siasa angeweza kutaka kila mwananchi aende bungeni pale Dodoma. Ingewezekana vipi? Ndio maana tuna wawakilishi.

Wanachama wote kuhudhuria mkutano ni uzamani. Wachache wanaweza kuwakilisha mawazo ya wengine katika mkutano. Huu ndiyo usasa. Hivi ndivyo kina Manchester United, Arsenal, Real Madrid, Barcelona na wengineo wanaendesha mambo yao. Kuna watu wana kadi za Manchester United huku Tanzania na hawawezi kuhudhuria mikutano hii.

Katika kauli yake nyingine kwa vipaza sauti vinavyojaa nyumbani kwake nimemsikia akidai yeye ndiye aliyewashauri Yanga wamchukue Aziz Ki. Nilicheka. Nani alikuwa hataki timu yake, iwe Simba au Yanga imsajili Aziz Ki baada ya kiwango chake alichoonyesha akiwa na ASEC wakati ule. Aziz alikichafua kuanzia Dar es Salaam hadi Abidjan. Alikichafua katika michezo mingi ya CAF.

Kilichohitajika kilikuwa pesa tu. Nilidhani rafiki yangu Magoma angedai yeye ndiye aliyetoa pesa za kumchukua Aziz Ki na ndiye anayemlipa Aziz mshahara wake. Kumbe alitoa wazo ambalo lilitolewa na mamilioni ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa klabu zao wakati ule.

Rafiki yangu Magoma amenikumbusha mbali. Amenikumbusha mwaka ‘1947’. Wakati ule ambao makomandoo walipenda migogoro. Wakati ule hata wanachama walipenda migogoro. Tatizo kubwa ni yeye na wale walio nyuma yake wameshindwa kusoma alama za nyakati.

Kuna matajiri wameingia hapa katikati na ‘wametanua magoli’. Kununua wachezaji ni pesa kubwa. Kulipa mishahara ni pesa kubwa. Kuhudumia kambi ni pesa kubwa. Ukiteleza kidogo tu basi kuna klabu nyingi mbili kubwa nchini zinasubiri kukuacha nyuma uteseka.

Mashabiki na wanachama wameshtukia mtego huu. Hawataki tena watu wa aina yake. Zamani ungeweza kupata kundi kubwa la watu ndani ya klabu. Siku hizi utashabikiwa na mashabiki wa timu pinzani tu ambao wangependa kuchochea mgogoro kwa adui.

Magoma amejikuta akipigana vita ambayo hawezi kushinda. Kila akigeuka atakutana na mtu mmoja tu aliyemtuma kwa masilahi yake binafsi. Hawezi kugeuka nyuma na kukuta kundi kubwa la watu kama zilivyokuwa vita za zamani. Mpira umegeuka kuwa pesa. Mahitaji ya pesa yamekuwa makubwa hadi mashabiki na wanachama wananyoosha mikono juu.

Tuendelee kutazama vita hii itapoishia, lakini sioni kama atashinda. Mahitaji makubwa ya pesa yamewatia unyonge makomandoo wenzake kiasi, wamesalimu amri kwa matajiri na mifumo yao. Hata hivyo, tabia yake imenikumbusha mwaka 1947 wakati tulipokuwa na vita nyingi ambazo hazikuwa na sababu.

Columnist: Mwanaspoti