Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

RIPOTI MAALUMU Wazazi wanavyobariki biashara haramu ya mabinti mijini  

E489ae86db3d144c66ae377e16eef9c1.jpeg RIPOTI MAALUMU Wazazi wanavyobariki biashara haramu ya mabinti mijini  

Mon, 7 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“NIMEKUJA jijini Dar es Salaam kutoka Mpwapwa kipindi cha Krismasi Desemba 2019. Nililetwa na baba mmoja niliyekabidhiwa kwake na mama yangu mzazi ili anitafutie kazi,” anaeleza Aisha Said (si jina halisi), mwenye umri wa miaka 13 katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni.

Anayasema hayo baada ya kufukuzwa nyumbani kwa aliyekuwa mwajiri wake.

Hata hivyo anasema, alifanya kazi miezi 10, lakini alilipwa miezi mitatu tu na kwamba, aliyemwajiri aliahidi kulipa malimbikizo ya malipo hayo kila mwezi, lakini mwishowe aligoma kumlipa kwa madai kuwa anapata chakula na malazi bure.

“Nilipoajiriwa tulikubaliana kuwa nitalipwa shilingi 50,000 kwa mwezi na nilimweleza fika mwajiri kuwa mama yangu anahitaji kutumiwa sehemu ya fedha yaani, shilingi 20,000 kila mwezi. Alifanya hivyo lakini alinilipa miezi mitatu tu tena bila kumpa chochote mama yangu.

“Nilipouliza na kumkumbusha, mama mwenye nyumba aliniahidi mara kwa mara kuwa watanilipa na kwamba, wananitunzia fedha zangu. Baada ya kuona kuwa mzazi wangu hatumiwi chochote, nikakumbushia sana na ndipo akaamua kunifukuza na kudai kuwa anaingia gharama kubwa kugharimia kukaa; kula na malazi yangu,” Aisha anaeleza madhila yaliyomfika.

Angelina Ziwani (si jina halisi) akiwa na umri wa miaka 10, aliondoka kijijini kwao katika huko Mpwapwa mkoani Dodoma na kwenda Arusha kutafuta kazi. Alifikia kwa ndugu yake.

Anasema: "Niliajiriwa miaka minne iliyopita wakati huo nikiwa na miaka 10, tena nikafanya kwenye mazingira magumu kweli yaani, mhhhh! Nilikuwa sipewi chakula cha kutosha, mahitaji mengine muhimu na waajiri wangu na walikuwa wakinidhalilisha kwa kuniita majina ya ajabu huku wakinilipa shilingi 40,000 kwa mwezi. Lakini nilitakiwa kuanza kazi alfariji na kuhitimisha usiku.”

Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inamwelezea mtoto kuwa ni mtu mwenye umri wa miaka chini ya 18. Inafafanua kuwa, ukatili kwa watoto unajumuisha ajira mbaya na hatarishi dhidi ya maslahi ya kwa watoto zikiwemo ajira zinazowanyonya watoto.

Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mtoto kinaeleza kuwa mtoto hatahusishwa katika kazi yoyote inayoweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake.

MNADA WA ‘MAHOUSE GIRL’ MPWAPWA

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, gazeti hili lilifika kwenye ‘baa’ moja mjini Mpwapwa na kushuhudia mabinti watano wakiwa mikononi mwa mwanaume anayedaiwa kuwa dalali wa mabinti tayari kwa kuunganishwa na watu wanaotafuta mabinti wa kazi mijini.

Mwandishi alimshuhudia mama mmoja aliyedaiwa kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta binti wa kufanya kazi za ndani akiletewa mabinti hao achague.

Chanzo kimoja kilichokuwa kimeongozana na gazeti hili (jina tunalo) kilisema, “Kwa mwonekano, watoto hao wana maumbo madogo na mhusika hapo anawahoji ili kupata yule anayeona anamfaa, lakini wanaangalia wenye miili mikubwa na wenye uwezo wa kufanya shughuli za mapishi na usafi.”

Neema Mushi ambaye amekuwa akifanya biashara mbalimbali katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 12, anasema: “Mara kadhaa nimekuwa nikishuhudia watoto au mabinti wadogo hasa siku za Jumanne na Alhamisi wakiletwa hapa na kuna watu huwa wanakuja kuongea nao kuwa watawapa kazi,” anaseme na kuongeza: “Sijui huwa wanaangalia vigezo gani, lakini huwa mwisho wa siku wanaondoka nao huku wakiwa wamebeba nguo kwenye ile mifuko wanayoita ‘shangazi kaja.”

WAZAZI CHANZO UTUMIKISHWAJI

Mwinyimwinyi ambaye ni mmoja wa wazazi wa watoto hao anasema: “Hatuna tunachojivunia kama kuwa na watoto wetu. Ndio wanaotuweka na kutufanya tuzidi kuishi, sisi toka tukiwa watoto tuliwatumikia wazazi wetu tena tulifaya kazi kama za kuchunga mifugo na kufanya shughuli za kilimo.

“Fahamu kuwa, kwa sasa watoto wangu ni kama mtaji kwangu… ndio wanaotuwezesha kula na hata kusaidia wadogo zao,” anasema mama huyo, mkazi wa Mpwapwa mwenye watoto wanne ambao wote wanafanya kazi za nyumbani mijini.

Maria Singano ambaye mwanaye yupo mjini akifanya kazi tangu akiwa na miaka 10 anasema: “Nimembeba mwenyewe, nimemlea mwenyewe tena kwa shida, sasa kama anapata kazi ambazo atalipwa kwa nini nisimruhusu kwenda kufanya?”

DALALI WA BIASHARA HIYO

Selemani Iluja (si jina halisi), ambaye huwaunganisha mabinti wanaotafuta kazi na waajiri wao anasema wazazi wa watoto huwa wanamtafuta kwa ajili ya kuwatafutia kazi watoto wao na kwamba, wakati mwingine huwa wanalazimika kutoa ahadi za uwongo ili wazazi waweze kuwaruhusu kwani na wao wanapata fedha za kwa ajili ya udalali

MABINTI 150 WAKOMBOLEWA KWA MWAKA DAR

Katika kutatua changamoto na kupunguza wimbi la mabinti wanaorubuniwa na kufanyishwa kazi za nyumbani, Taasisi ya Daughters of Mary Immaculate (DMI) ya Dar es Salaam imekuwa ikiwanusuru kati ya watoto wa kike 120 hadi 150 kila mwaka mkoani humo.

Meneja Programu wa DMI nchini, Fatima Rani anasema tangu waanzishe kituo chao mwaka 2017, wameokoa mabinti takribani 600 (wastani wa 150 kwa mwaka) waliopelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kutumikishwa katika kazi za nyumbani na kwamba, wamekuwa wakichukua na kuwapa mafunzo, stadi mbalimbali na kisha kuwarudisha kwao.

“Kupitia Idara ya Uhamiaji, na Sekretarieti ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu, tumepokea watoto wa kike kutoka mikoa ya Dodoma (ikiwemo Mpwapwa), Iringa, Mbeya, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Tanga, wote wakiwa ni waathirika wa biashara hii haramu.”

Anaongeza: “Pia tumekuwa tukiwanusuru baadhi waliofika nchini wakitokea Malawi, Uganda, Burundi na Angola.”

Fatima anasema: “Kati ya wale 150 tunaowapokea kila mwaka, asilimia 85 huwa wamesafirishwa kwa ajili ya kutumikishwa, asilimia 15 ni wale ambao wametoroka maisha na mazingira magumu nyumbani kwao.

“Pia katika asilimia 85 ya mabinti hao 150, asilimia 50 yake ni wale ambao wanatumikishwa kingono na asilimia nyingine 50 wanalazimishwa kufanya kazi ngumu nyumbani ambazo wakati mwingine haziendani na umri wao,” anasema meneja huyo.

Anaongeza kuwa, kati ya mabinti 10 hadi 15 ambao huwa wanapokelewa kituoni kwake kwa ajili ya msaada kila mwaka, huwa tayari ni wajawazito licha ya kuwa wengi wao wapo kati ya umri wa miaka 13 na 17.

HALI ILIVYO HALMASHAURI YA MPWAPWA

Kamati ya Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa iliketi Septemba 26, 2018 chini ya Kaimu Mwenyekiti, Khamlo Njovu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kujadili mambo mbalimbali na taarifa kadhaa za wadau kuhusu utekelezaji wa shughuli za ulinzi wa mwanamke na mtoto.

Hata hivyo, Idara ya Elimu Sekondari inayosimamia na kuratibu shughuli zote za Elimu Sekondari katika Wilaya ya Mpwapwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari wanapata haki ya kumaliza elimu ya sekondari.

Kamati ilibaini katika mwaka 2018, shule za sekondari za halmashauri hiyo ziliingiza wanafunzi 10,224 (wasichana 5,200 na wavulana 5,024), lakini takwimu zinaonesha utoro wa wanafunzi, sababu zikiwa ni mimba kwa watoto wa kike, utoro sugu, ugonjwa, vifo na kufukuzwa shule kutokana na utovu wa nidhamu.

Kwa upande wa utoro takwimu zinaonesha wasichana walikuwa 180 na wavulana 334 na kufanya idadi kuwa 514. Mimba zilikuwa 44, ugonjwa watoto wanne wote na wasichana, waliofukuzwa wasichana wawili na mvulana mmoja na upande wa vifo alifariki mtoto mmoja wa kiume.

WAZIRI AONYA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene anasema hali ni mbaya hasa katika maeneo ya miji mikubwa ambapo biashara ya kusafirisha watu bado imeshamiri hasa kwa wanawake na watoto wa kike.

Simbachawene anasema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukomesha hali hiyo.

Anasema: “Usafirishaji haramu wa binadamu ni shida kubwa nchini Tanzania, kuna watu ambao wanafaidika kwa kuwarubuni wasichana wadogo kutoka katika familia zilizo katika mazingira magumu na kuwapeleka kwenye familia za mijini kama wafanyakazi wa nyumbani.”

Katika kukabiliana na hali hiyo, waziri huyo anasema: "Wasimamizi wa sheria hawapaswi kuendelea kusubiri kupokea malalamiko katika ofisi zao, bali waende nje na kupambana na biashara hiyo.”

Aidha, anasema alishaviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini kote kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18, anayesafirishwa kutoka eneo moja kwenda lingine anakuwa na kibali cha mzazi na kile cha kiongozi wa serikali za mitaa.

Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya DMI mwaka 2020, asilimia 97 ya usafirishaji haramu wa binadamu nchini Tanzania ni wa ndani, hasa ukiwahusisha vijana kati ya miaka 12 hadi 17 na asilimia 74 ya waathirika hao ni wasichana wadogo.

KAMATI YA KUPAMBANA NA BIASHARA HARAMU

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Adatus Magere, anasema mtandao wa biashara ya usafirishaji ni mkubwa kitaifa na kimataifa.

"Karibu asilimia 80 ya watu wanaouzwa duniani ni wanawake na wasichana chini ya miaka 18. Kwa changamoto hiyo, nchini Tanzania Serikali imebanwa na rasilimali duni kushughulikia masuala ipasavyo licha ya kuwa inapambana,” anaeleza.

UMOJA WA MATAIFA

Agosti 12, 2020, Mkuu wa Ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) nchini Tanzania, Dk Qasim Sufi, alisema jamii ya kimataifa ikiwemo IOM inaangalia usafirishaji haramu wa binadamu duniani hususani nchini Tanzania kama moja ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

"Kuna njia nyingi ambazo watu huangukia kwenye biashara haramu ya binadamu, lakini matokeo ni yale yale, wengi wanapoteza haki zao na kudhalilishwa. Shida hii ipo ulimwenguni kote,” anaeleza Dk Sufi na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuzingatia Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Watu ya 2008.

WADAU WASHAURI

Katika kutatua changamoto hizo, Meneja Programu wa Taasisi ya DMI, Fatima Rani, anaishauri serikali kutoa elimu kwa jamii ikiwemo kwa wazazi ambao wamekuwa sehemu ya tatizo hilo.

“Elimu kwa wananchi wakiwemo wazazi ni muhimu kwani huwa tunapata vitisho tunavyofanya uokozi wa mabinti hawa, na vitisho vinatoka kwa wale wanaowasafirisha au wanaoruhusu mabinti wao kusafirishwa hivyo naomba vyombo vya dola na Serikali iendelee kutusaidia,” anasema.

Columnist: www.habarileo.co.tz