Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

RIPOTI MAALUMU:- Watoto wanavyozama kwenye kamari

D156be832b03054f95c4bb032a3053df RIPOTI MAALUMU:- Watoto wanavyozama kwenye kamari

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UNAPOZUNGUMZIA nidhamu ya watoto, moja kwa moja unagusa weledi wao katika utii wa maelekezo na miongozo iliyowekwa na jamii inayowazunguka.

Wakati ulimwengu ukiendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, gazeti hili limebaini mabadiliko hayo yamekuwa na matokeo hasi kwa baadhi ya watoto waliotumbukia kwenye uraibu wa michezo ya kubahatisha na kamari.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLeo katika mikoa mitano ya Tanzania Bara umebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto ambao sasa wamejikita kwenye michezo ya kubahatisha, baadhi yao ikiwa sababu ya kutofanya vizuri darasani na wengine kuacha masomo kabisa.

HabariLEO imebaini wapo watoto waliofikia hatua ya kuiba fedha za wazazi na walezi wao nyumbani na kuzitumia kushiriki kwenye michezo ya kubahatisha na kamari.

Udadisi wetu pia ulibaini watoto ambao wamekumbwa na baa hilo kutokana na ushawishi kutoka kwa wenzao, matangazo ya kamari na michezo ya kubahatisha na ushawishi wa mawakala wa kampuni za kamari, wanaolenga kuongeza mapato ya biashara hizo.

Maeneo yaliyoguswa na uchunguzi huu ni pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza, Dodoma na Mbeya, uchunguzi ukijumuisha mahojiano na baadhi ya watoto wanaoshiriki michezo hiyo.

Sheria za Tanzania zinazuia watoto (watu wenye umri chini ya miaka 18) kushiriki katika michezo ya kubahatisha na lipo tamko rasmi la Wizara ya Fedha na Mipango la Serikali kuzuia watoto kushiriki, kuingia, kukaa au kuzurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.

DAR, DODOMA, MWANZA NA MBEYA

Uchunguzi wa HabariLEO unapiga kambi kwenye moja ya shule za sekondari wilayani Ilala, Dar es Salaam na kuingia kwa nyakati tofauti kwenye darasa lililokuwa na wanafunzi 72 wa kiume na kike wenye umri wa kati ya miaka 14 na 16.

Baada ya mahojiano na baadhi ya wanafunzi, gazeti hili linabaini idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa hilo wanashiriki katika michezo ya kubahatisha kuhusu matokeo ya soka. Wanafunzi 11 kati yao wakiitupia lawama timu ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya England, kwa kile walichodai “inachana sana mikeka”.

Athumani Bilal (siyo jina halisi) mwenye miaka 13, anasema: “Baba huwa anacheza na wakati mwingine anapata fedha nyingi, mimi nimeshacheza mara nyingi tu na huwa ninapata fedha laki (Sh 100,000), Sh 50,000 na kuna siku nilikula shilingi 160,000. Inategemeana na upepo wa siku hiyo.

“Kuna siku nilikula ‘kilo tano’ (500,000). Tulipokwenda kudai walininyima kwa kuwa walihitaji kitambulisho cha taifa na mimi bado sijapata kitambulisho mpaka miaka 18. Lakini hizi fedha ndogo ndogo huwa ninalipwa moja kwa moja,” anasema na kubainisha kuwa alianza kushiriki michezo hiyo akiwa na umri wa miaka 12 na tayari ameshamfundisha pia binamu yake.

Kimsingi, uchunguzi wa HabariLEO umebaini kadhia ya watoto kujihusisha na kamari na michezo ya kubahatisha imetawala katika maeneo mengi ya jiji hilo la kibiashara.

Uchunguzi wetu ukahamia jijini Dodoma, shida hiyo pia inatikisa katika jiji hilo jipya. Katika moja ya shule za sekondari jijini humo, ilibainika kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi wa kidato cha tatu na nne wamefikia hatua ya kuingia darasani na fomu za michezo hiyo, maarufu mikeka.

“Shule hii haifanyi vizuri sana na hata wanaofaulu mara nyingi ni watoto wa kike. Wanafunzi wengi wa kiume wengi wao wamekuwa wanacheza kamari na michezo mingine ya kubahatisha.

“Mimi nimekamata wengi wakiwa na fomu hizo, si chini ya watano lakini tunawaelimisha kuhusu vitu hivyo na madhara yake,” anaeleza mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Jijini Mwanza, uchunguzi wetu, umebaini kuwa, katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo, ukiwamo Uhuru, kamari na michezo ya kubashiri imepata wateja wengi wakiwamo watoto.

“Michezo ya kubahatisha ni kama biashara nyingine unazojua na mteja yeyote anayekuja, huna jinsi zaidi ya kumhudumia kwani wanapokuwa wengi unakuwa na nafasi ya kupata fedha zaidi.

“Sisi huwa hatukagui kitambulisho mteja anapokuja, kitambulisho tunatumia pale tu mtu anaposhinda fedha, tena inayozidi Sh 500,000.

“Mara kadhaa kuna baadhi ya watu wameshindwa kupata malipo yao kwa kupata usumbufu kwa sababu ya kitambulisho na wengine wamenyimwa. Mara nyingine huwa wanapata bila kitambulisho lakini kama fedha walizoshinda ni kidogo maana huwa tunaweza kuzituma kwa njia ya simu,” mfanyakazi wa kampuni ya michezo ya kubahatisha jijini Mwanza anasema.

Mfanyakazi huyo anakiri kuwa, baadhi ya wanaobashiri ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 18 na mara kadhaa huwa wanawahudumia kwa sharti wasiwe wamevaa sare za shule.

Katika soko la Mwanjelwa jijini Mbeya, mwandishi anabaini kuna kibanda kidogo kinachotoa huduma za simu na michezo ya kubahatisha, na ameshuhudia watoto wawili wenye umri wa mwanafunzi wa shule ya msingi wakitaka kuchukua fomu ya kubashiri matokeo ya soka.

“Nyie watoto mnataka kunifunga jela, jana mwenzenu alikuja na kuacha matatizo hapa baada ya mzazi wake kutuletea polisi. Nyie nendeni sehemu nyingine,” alilalama mfanyabiashara katika kibanda hicho.

Anapoulizwa na HabariLEO kuhusu mkasa uliompata, mfanyabiashara huyo anasema: “Tuna shida ya fedha lakini kwa sasa sheria za michezo hii kwa watoto ni kali, mara moja moja huwa tunachukua fedha maana ubashiri haujawa mkubwa kwenye Jiji la Mbeya.”

SANYAJUU - KILIMANJARO

Victoria Mbando, mkazi wa Kirua mkoani Kilimanjaro, anasema alibaini mwanawe anacheza kamari na wakati mwingine michezo ya kubashiri matokeo ya soka baada ya kumkamata akiwa na Sh 6,000 mfukoni.

“Nilimkuta na Sh 6,000, baada ya kumpekua, nilipomchapa na kumtaka aniambie kazipata wapi, ndiyo akasema anacheza korokoro na wakati mwingine michezo ya kubashiri,” anasema Mbando.

Mkazi wa Kijiji cha Fuka, Sanyajuu mkoani Kilimanjaro, Magdalena Magoma, anasema mwanawe wa darasa la pili aliiba fedha za mauzo ya mayai Sh 1,000 na kwenda kucheza michezo wa kubahatisha aina ya ‘korokoro’ na aligundua mchezo huo baada ya tabia ya wizi kushamiri ndani mwake.

SAUTI ZA WADAU

Jukwaa la Vuguvugu la Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi (TAPO) lililopo Sanyajuu, Wilaya ya Siha, Kilimanjaro, linahoji mikakati ya serikali kudhibiti watoto kushiriki katika michezo ya kubahatisha na kamari.

Wanaharakati hao wanadai idadi ya watoto wanaocheza kamari ya korokoro katika miji midogo ya Sanya Juu na Kirua (Lawate) inahatarisha hatima yao kimasomo.

Mwenyekiti wa TAPO, Christina Kavishe, anasema ukimya wa uongozi wa Wilaya ya Siha katika kudhibiti baa hilo ndiyo unawasukuma kujitokeza hadharani kukemea michezo hiyo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

HabariLeo inatua mezani kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Siha, Marko Masue, kusaka majibu kuhusu malalamiko hayo ya wadau, akisema mamlaka ya kudhibiti vitendo hivyo yanaanzia kwa maofisa watendaji wa vijijiji.

"Nimepokea malalamiko hayo na tutayafanyia kazi, lakini ninataka niseme kwamba mamlaka ya kudhibiti kamari na michezo mingine ya kubahatisha ipo chini kabisa kule kwa watendaji wa vijijiji.

"Kama hali iko hivyo, mwandikieni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha ili achukue hatua zaidi," Ofisa Maendeleo ya Jamii huyo anasema.

WENYE KAMPUNI

Gazeti hili pia linawatafuta wamiliki wa kampuni zinazoendesha michezo hiyo, ikiwamo Kampuni ya Meridianbet Tanzania, inayoeleza kwamba mbali na kujali usalama wa wachezaji wao, inazuia ushiriki wa watoto kwenye michezo ya kubahatisha.

Inaelezwa katika tovuti rasmi ya kampuni hiyo kwamba uthibitisho wa kufikia umri wa ukubwani na tarehe ya kuzaliwa ni utaratibu wa lazima katika kufanya usajili kwa wateja wake wanaoshiriki michezo hiyo kwa njia ya mtandao.

"Nakala zaidi ya kitambulisho cha picha yaweza pia kuhitajika wakati wateja wanapofanya utoaji wa fedha kwa mara yao ya kwanza," kampuni hiyo inafafanua katika tovuti yake.

Vilevile, Kampuni ya MBet kupitia tovuti yake, inabainisha kuwa ni haramu kwa mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 kushiriki kwenye michezo ya kubahatisha.

Zuio kwa watoto kushiriki kwenye michezo hiyo pia ni miongoni mwa masharti ya Kampuni ya Sportpesa ambayo kupitia tovuti yake inakataza mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 kucheza michezo hiyo.

“Sportpesa ina haki ya kujua taarifa kuhusu mteja na inaweza kupata taarifa za ziada za umri wa mteja kwa mamlaka au kada nyingine pale itakapohitaji," kampuni hiyo inafafanua kwenye tovuti yake rasmi.

KAULI YA BODI

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT), James Mbalwe, anapaza sauti kwa jamii kuwalinda watoto kutojihusisha na kucheza kamari kutokana na kukithiri kwa matokeo hasi ya michezo hiyo.

"Tumebaini kuwapo kwa kundi kubwa la wazazi ambao wamekuwa wakitupa malalamiko mengi kuhusu ushiriki wa watoto kwenye michezo ya kubahatisha.

“Bodi kwa kutambua kuwa watoto ni taifa la kesho, tumeona ni lazima tuweke mkazo kwa ajili ya kuihimiza jamii ili kila mtu awe balozi kwa watoto wanaoshiriki kamari. Sisi hatuwezi kuwa kila mahali na ndiyo maana tunataka jamii kuwa mabalozi wetu," anasema.

TAMKO LA SERIKALI

Mwaka 2017, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma, aliyetaka kujua mkakati wa serikali kudhibiti kamari nchini, alisema michezo yote ya kubahatisha ikiwamo kamari inaendeshwa kwa mujibu wa sheria.

Dk. Ashatu alisema sheria za nchi zinakataza watoto kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo inakofanyika michezo ya kubahatisha.

"Mtu yeyote atakayeruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo wa kubahatisha, anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa faini ya Sh. 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

"Endapo kosa hili litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, bodi ina mamlaka kisheria ya kumfutia leseni," Dk. Ashatu alisema na kuongeza kuwa ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha vijana wao wanazingatia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania.

MAPATO YA KAMARI

Mtaalamu wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, Lazaro Mbise, anawalaumu wazazi ambao huwaacha watoto bila uangalizi maalum, akisema ni sehemu ya mzizi wa kuwapa nafasi watoto kujihusisha na kamari.

“Kama wazazi, lazima tujue majukumu yetu. Inasikitisha kwamba kuna wazazi wengine ambao hawafuatilii maendeleo ya watoto wao na hapo ndipo tatizo linapotokea. Wengine wanashiriki kwenye masuala yasiyokuwa na tija wakiwa na watoto hao," anasema.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), katika mwaka wa fedha wa 2017/18, serikali iliiwekea lengo Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kukusanya Sh. bilioni 39.1 lakini bodi hiyo ilipita lengo na kukusanya Sh. bilioni 78.7, sawa na asilimia 201.4 ya lengo.

Mwaka uliofuata, serikali iliiwekea bodi hiyo lengo la kukusanya Sh. bilioni 98.1 lakini bodi hiyo ilikusanya Sh. bilioni 94, sawa na asilimia 95.8 ya lengo.

Columnist: habarileo.co.tz