Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Propaganda za Kane, Bellingham katika ubora

Kane Jude Propaganda za Kane, Bellingham katika ubora

Sun, 24 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hawakututawala sana lakini ile siku Mzungu Mwingereza Richard Turnbull alipokabidhi madaraka kwetu Desemba 9, 1961 tujitawale wenyewe Waingereza walikuwa wametuachia chembechembe fulani hivi za tabia zao.

Ukitutazama tunajiona sisi kama wao. Tuna chembechembe, lakini hatuwezi kuwafikia Waingereza katika ubora wao wa kujitengenezea majina na ufalme hasa linapokuja suala la mchezo wa soka. Namna wanavyoweza kukupaisha kwa sababu ya Uingereza wako.

Jumanne na Jumatano nilikuwa nimejikunyata katika kochi nikifuatilia Ligi ya Mabingwa Ulaya. Waingereza walinikumbusha mbali. Namna wanavyofahamu propaganda. Namna wanavyojua kuwapamba watu wao na mambo yao kwa ujumla.

Walinikumbusha wakati ule walipomtengeneza David Beckham na kumpeleka juu ya Ronaldo de Lima, Zinedine Zidane, Rivaldo na wengineo. Namna Beckham alivyokwenda Real Madrid na mkewe Victoria Beckham.

Waingereza walitengeneza homa ambayo haikuwepo. Hata kama Beckham angetema mate bado wangeweka kuwa ‘breaking news’ katika mitandao yao. Kila kitu kilikuwa breaking news. Waingereza walikuwa katika ubora.

Maandalizi ya pambano la Shakhtar Donetsk dhidi ya Porto, Watanzania walijaa katika mtandao wa klabu hii ya Ukraine kufuatilia habari za Novatus Dismas Miroshi. Hata mechi yenyewe ikaangaliwa na Watanzania wengi kwa sababu ya Novatus tu. Basi. Mimi ni mmojawao.

Lakini sisi ni wadogo. Tuna haki ya kumfuatilia mchezaji wetu. Yupo mmoja tu anayecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa Waingereza imekuwa tofauti. Wamenikumbusha propaganda walizokuwa wanafanya wakati wa Beckham.

Sasa kuna timu mbili kubwa ambazo zinafuatiliwa vilivyo na vyombo vya habari vya Uingereza pamoja na Waingereza kwa ujumla. Bayern Munich kwa sababu ya Harry Kane, na Real Madrid kwa sababu ya Jude Bellingham.

Waingereza wameitawala dunia. Huwa hawana habari sana na mambo ya nje mpaka linapokuja suala hili hapa. Mfano ni huu hapa. Kwa sasa Bayern Munich ipo katika midomo yao. Kisa? Kane. Tangu amekwenda Bayern Munich imekuwa haitoki katika televisheni za Waingereza. Kisa Kane.

Kuna waandishi wa Kiingereza wameweka kambi katika uwanja wa mazoezi wa Bayern Munich uitwao Sabener Strasse. Kane akiwa wa kwanza kuingia ndani ya uwanja wa mazoezi kwao ni habari. Akiwa wa mwisho kwao ni habari. Akizungumza na mchezaji yeyote kwao ni habari.

Kuelekea pambano la Bayern Munich dhidi ya Manchester United pale Munich katikati ya wiki hii walikuwa wanaripoti kama vile Kane alikuwa anacheza peke yake. Mara nyingi walikuwa wanasema “Harry Kane dhidi ya Manchester United.”

Ikatokea bahati Bayern Munich wakapata penalti na Kane akafunga. Ikawa habari kubwa zaidi. Bahati mbaya ni kwamba kipa wa Manchester United, Andre Onana alifungwa bao la kizembe ambalo kwa kiasi lilitengeneza habari ya mechi. Vinginevyo habari kubwa zaidi katika mechi ingekuwa bao la penalti la Kane.

Na ndicho kinachoendelea pale Real Madrid. Kuna waandishi wa Kiingereza wameweka kambi kwa ajili ya Bellingham.

Ni kweli anafanya vyema tangu ajiunge na wababe hawa wa Santiago Bernabeu, lakini nahisi Waingereza wanatia chumvi habari ya Jude.

Tangu amekwenda Madrid ghafla jina la Real Madrid limerudi katika chati katika vyombo vya habari vya Kiingereza. Ni propaganda. Kila anachofanya kuanzia mazoezini hadi katika mechi ni habari kubwa kwao. Hawa ndio Waingereza katika ubora.

Na kama ilivyo kwa Kane, Jude naye aliifungia Real Madrid bao katika pambano dhidi ya Union Berlin. Mpira ulimkuta Jude katika mstari wa lango. Lilikuwa ni suala la kuusukuma tu kuupeleka wavuni. Haikuchukua hata hatua moja. Bao la penalti lingekuwa gumu kuliko hili.

Baada ya hapo Waingereza wakaamka na Jude. Ni kama vile lilikuwa bao ambalo limefungwa katika fainali za Kombe la Dunia. Kumbe zilikuwa pointi tatu za mechi ya kwanza ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata kama wangetoka sare wangeweza kujirekebisha mbele ya safari.

Wanachonikosha ni kwamba kama ilivyo kwa Kane pia basi imegeuka kwa Jude pindi wanapoitamka Real Madrid. Ni kama vile Bob Marley and Wailers. Na ndicho wanachofanya. ‘Jude Bellingham and Real Madrid will face Atletico Madrid this weekend’.

Sijui kama naipenda tabia hii ya Waingereza au sijui kama naichukia. Ninachojua ni namna ambavyo wananiacha mdomo wazi. Wanajua kuwatengeneza wachezaji wao. Sijui wengine tuwaige au tuachane nao lakini ukweli ni kwamba wanajua.

Ninachojiuliza ni kama watu wa mataifa mengine wapo bize na wachezaji wao wanaocheza Uingereza kiasi cha kuweka kambi katika miji mbalimbali ambayo wachezaji wao wanacheza. Kuna waandishi wa Norway kazi yao ni kumfuatilia Erling Haaland pale Manchester? Kuna waandishi wa Kibrazili ambao kazi yao ni kuwafuatilia kina Casemiro, Gabriel Jesus, Gabriel Martinelli, Bruno Guimares na wengineo ambao wanacheza England? Sidhani. Niliwahi kuwa Brazil mwaka 2007 lakini hawakuonekana sana kufuatilia Ligi Kuu England.

Vipi kuhusu Wafaransa ambao wanacheza England? Vyombo vya Ufaransa vinawafuatilia sana pale England? Sidhani. Vipi kuhusu Waargentina? Wahispaniola? Na wao wanawafuatilia sana wachezaji wao wanaocheza England kama Waingereza wanavyowafuatilia akina Kane na Jude waliopo katika mataifa yao? Sina uhakika.

Ninachofahamu ni kwamba mbele ya safari Waingereza watapenda zaidi Bayern Munich au Real Madrid mmoja wao achukue ubingwa wa Ulaya kwa ajili ya Kane au Jude. Hii itawapa habari na ufalme mwingi katika vyombo vya habari vya nyumbani. Lakini vipi kuhusu bei zao sokoni? Utalazimika kulipa pesa kubwa pindi utakapomuhitaji Declan Rice. Wameitengeneza hivyo.

Kama unawalalamikia Brighton and Hove kwa kumuuza Moises Caicedo kwenda Chelsea kwa pesa nyingi, basi ujue aliuzwa kwa pesa kidogo. Ni vile tu alikuwa staa wa kimataifa wa Ecuador. Kama angekuwa Mwingereza basi Chelsea wangelazimika kutoa hadi kiasi cha pauni 120 milioni kwa ajili ya kupata huduma zake. Ndivyo Waingereza walivyo. Hatuna tunachoweza kuwafanya

Columnist: Mwanaspoti