Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pongezi mikoa iliyoongoza ufaulu

52ef5aac9b9c5353ad28d56137ea0fd1 Pongezi mikoa iliyoongoza ufaulu

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi lilitangaza matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 nchini huku yakionesha ongezeko la ufaulu wa zaidi ya asilimia 1.18 dhidi ya matokeo ya mwaka jana baada ya wanafunzi 833,672 sawa na asilimia 82.68, kati ya wanafunzi 1,008,307 waliofanya mtihani huo kufaulu.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde sambamba na hilo, ufaulu huo, masomo ya lugha ya Kiswahili, Kiingereza pamoja na maarifa ya jamii umepanda kwa asilimia kati ya 0.43 hadi 5.10 ikilinganishwa na mwaka 2019 hatua inayoonyesha kasi ya ukuaji wa maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Pia Dk Msonde aliitaja mikoa iliyopenya na kushika nafasi 10 kuwa ni pamoja na Dar es Salaam iliyoshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Arusha, Simiyu, Katavi, Kilimanjaro, Iringa, Kagera, Morogoro, Pwani na Mwanza huku mikoa ya Mtwara na Singida ikitajwa kushuka kwa ufaulu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Binafsi napenda kuchukua fursa hii kutoa kongole kwa wakuu wa mikoa, maafisa wa elimu, walimu pamoja na wanafunzi katika mikoa yote iliyofanya vizuri kwa jitihada zao za dhati kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kujiletea mafanikiko kwa kuwa hilo ndiyo jambo pekee litakalozidi kuleta msukumo wa maendeleo ya Taifa hili.

Lakini pamoja na pongezi hizo kwa mikoa iliyofanya vizuri, nitumie fursa hiyo hiyo pia kuwatia moyo viongozi wa mikoa iliyofanya vibaya katika matokeo hayo huku nikiwakumbusha kuwa hakuna njia ya mkato ili kufikia mafanikio wanayoyataka zaidi ya kujituma ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja kama viongozi wa mkoa na kutatua changamoto zote za kielimu pale zinapojitokeza.

Kwa mikoa iliyofanya vizuri, napenda kuwakumbusha kufanya maandalizi ya miundombinu ya shule maalumu ili kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuanza masomo yao mapema mwakani.

Nayasema haya kwa kuwa mara nyingi inapofika kipindi cha msimu mpya wa masomo unaoendana na ingizo la wanafunzi wa kidato cha kwanza au cha sita, baadhi ya shule hujikuta katika changamoto kubwa ya upungufu wa vyumba vya madarasa na hata madawati na hivyo kusababisha usomaji wa taabu kwa wanafunzi na wakati mwingine hata kuchelewa kuanza kwa masomo.

Jambo hili ambalo kwa baadhi ya shule limekuwa kama mazoea kwa kujitokeza mara kwa mara, ni wazi kuwa limekuwa likichangia kuharibu saikolojia za wanafunzi ambao matarajio yao ni kuanza masomo na kusoma bila changamoto za miundombinu pale wanaporipoti shuleni.

Kuna muda wa takribani mwezi mmoja na nusu kuanzia sasa hadi Januari kipindi ambacho wanafunzi hao wataanza masomo yao, hivyo kwa shule ambazo zinajiona wazi kuwa na upungufu wa miundombinu hyo zinaweza kuutumia kutatua changamoto hizo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa masomo hapo mwakani.

Matarajio yangu na pengine wadau wote wa sekta ya elimu ni kuona suala hilo likifanyiwa kazi mapema katika muda uliobakia.

Sio vyema kusubiri hadi Januari wakati wanafunzi watapoanza kuripoti kwani watakumbana na msongamano madarasani kutokana na changamoto ya madarasa na ukosefu wa madawati.

Columnist: habarileo.co.tz