Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pongezi Rais Magufuli kukataa kunyonga

16664 Pic+kujinyonga Pongezi Rais Magufuli kukataa kunyonga

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUZI wakati akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri katika Ikulu ya Chamwino Dodoma, Rais John Magufuli alitangaza kuwabadilishia adhabu ya kifo wafungwa 256 na kuamuru wafungwe kifungo cha maisha.

Tangu alipoingia madarakani katika awamu yake ya kwanza mwaka 2015 hadi sasa alipoanza awamu ya pili, Rais Magufuli hajasaini hati ya adhabu ya kifo kwa mhalifu yeyote aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa.

Uamuzi huo wa juzi umetoa taswira mpya kwa wadau wa haki za binadamu, kwa kuwabadilishia adhabu wahalifu hao kutoka kunyongwa kuwa wafungwa wa maisha.

Akigusia sababu za kukataa kunyonga, Rais Magufuli alibainisha kuwa hawezi kunyonga idadi hiyo kubwa ya wahalifu 256 wakati inawezekana mhalifu mmoja aliua watu wawili au mmoja. Hivyo, alisema yeye akinyonga wahalifu 256, anakuwa ametenda adhabu kubwa zaidi.

Binafsi ninapongeza uamuzi wa Rais Magufuli wa kukataa kunyonga, kwa kuwa kwanza ni kinyume na haki za binadamu kutoa uhai wa mtu mwingine, kwa kigezo cha kuwa mtu huyo naye aliua.

Alichokifanya Rais Magufuli ni mwanzo mzuri kuelekea hatua ya kuondoa adhabu ya kifo hapa nchini, ambayo imekuwa ikipingwa na wadau wengi wa haki za binadamu.

Rais Magufuli ameonesha kivitendo maana halisi ya kulinda haki na utu watu wengine, hasa kwa uamuzi wake huo ambao umegusa nyoyo za watu wengi.

Kwa kuwa Rais Magufuli ameamua kuwabadilishia adhabu kutoka kwenye kuuawa na kuwa wafungwa wa maisha, hapa ninaona kuwa kuna faida kubwa kwa adhabu hii kwa kuwafunga maisha kutoka kwenye adhabu ya kuwanyonga.

Kwa kuwafunga maisha wahalifu wanakuwa bado ni watu wenye faida, kwa kuwa kwanza watatumia muda wao mwingi kufanya kazi wakiwa gerezani.

Wakiwa gerezani watashiriki shughuli za kiuchumi kama kilimo, ujenzi, utengenezaji wa bidhaa za samani na shughuli nyingine za maendeleo.

Hivyo, idadi hiyo kubwa ya wahalifu, kama itatumika vema kwa kufanya kazi za aina mbalimbali, itachagiza maendeleo wakati kama wangenyongwa, nguvu kazi hiyo ingepotea.

Binafsi napongeza uamuzi huo wa Rais Magufuli. Nawasihi wakuu wa magereza kuendelea kuwanoa kitaaluma wafungwa hao, ambao kwa sasa wanakuwa wafungwa wa maisha, ili watoe mchango kwa kufanya shughuli zinazoendana na taaluma zao.

Ningependa hatua hiyo ya Rais Magufuli kuhusu adhabu hiyo kifo kwa wahalifu hao isiwe sababu ya wahalifu nchini kuona sasa wameruhusiwa kuua.

Kama wapo ambao watachukulia hatua hiyo ya Rais Magufuli, ya kutotelekeza adhabu ya kifo kwa wahalifu hao 256, kuwa ndio sababu ya wao kuendelea kupoteza uhai wa watu, basi wajue kuwa wamejidanganya.

Ni imani yangu kuwa kubadilishwa kwa adhabu ya kifo na kuwa ya maisha, siyo chachu ya watu wengine kuendelea kutenda kosa la kuua. Bali, hatua hii ifanye watu hao waachane kabisa na matukio ya uhalifu, hasa huo wa kupoteza roho za watu.

Columnist: habarileo.co.tz