Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pole Kaze, haya ndio maisha nje ya Yanga

Cedrick Kazeeee Cedrick Kaze

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Siku moja pale hotelini Tunisia ambako Yanga ilikwenda kucheza na Monastir ya kule nilipata nafasi ya kupiga stori nyingi na rafiki yangu Cedric Kaze. Wakati huo alikuwa kocha msaidizi wa Nasireddine Nabi. Nimekumbuka kitu.

Kaze mtu wa mpira hasa. Anaupenda mpira. Anauishi mpira. Aliwahi kuniambia ndoto yake kubwa katika soka la Tanzania. Aliniambia anatamani siku moja aondoke Yanga aende katika timu ya kawaida kabisa. Akaifundishe kutandaza kandanda na iwe timu simulizi hapa nchini.

Kwanini sio Yanga? Nilimuelewa. Alihitaji timu yake ambayo ataimiliki. Timu ambayo wachezaji watamtii. Timu ambayo wachezaji watafuata maelekezo yake na kumtii bila ya shuruti. Nadhani nilimuelewa vyema. Mpira wa kisasa ni mchezo wa kitumwa.

Labda ndio maana Pep Guardiola aliwaondoa Ronaldinho, Samuel Etoo na Deco pale alipofika kikosi cha wakubwa Barcelona. Nadhani alihitaji watu wa kumtii. Wale walishajiona kuwa wakubwa kuliko klabu. Walikuwa wamefanya mengi ya kuwafanya wajione wakubwa.

Nimemkumbuka rafiki yangu Kaze juzi baada ya kuisoma taarifa yake ya kuondoka timu ya Namungo. Akilini nilikuwa nawaza. Namungo ndio timu ambayo ilikuwa katika mawazo ya Kaze au alihitaji timu ndogo zaidi? Kwa wasifu aliokuja nao wakati ule inaonekana kwamba hata Yanga ilikuwa timu ya saizi yake.

Nadhani Namungo ingeweza kuwa timu ya kutimiza ndoto zake. Timu ambayo angeifundisha na kuacha alama kubwa klabuni hapo. Hata hivyo mambo hayajaenda hivyo. Namungo imekuwa na mfululizo wa matokeo mabovu mpaka yeye mwenyewe ameamua kuachia ngazi. Inawezekana pia Kaze na Namungo wamesitiriana. Hatujui nani amemuacha mwenzake.

Aina ya maandishi ya Kaze ni busara ambayo wanatumia Wazungu. Wakati mwingine wanakufukuza, lakini wanakwambia uandike barua ya kuomba kuondoka. Wakati mwingine pia wanakufukuza, lakini wanasema ‘tumefikia makubaliano ya kuachana’. Hiyo ni “thank you” yenye busara kubwa.

Kitu pekee ambacho Kaze hakuweza kukielewa ni kwamba kuna ugumu mkubwa wa kutimiza ndoto zake Tanzania. Naijua vyema nchi hii. Naujua mpira wake. Kwanini Azam FC wenyewe wanashindwa kutimiza ndoto zao na wana kila kitu katika klabu yao? Angejiuliza Kaze.

Kilichopo ni kwamba unaweza kudhani maisha ya soka Tanzania pale unapokuwa Simba au Yanga. Ukiwa kama kocha, kiongozi au mchezaji maisha ni rahisi Simba na Yanga. Ukiondoka Simba na Yanga maisha sio rahisi sana kama ulivyokuwa unafikiri. Imewatokea watu wengi na sasa Kaze anakuwa mfano mwingine.

Kwa mfano, Kaze alikuwa anaamini kwamba nje ya Simba na Yanga angepata utulivu mkubwa wa kufanya kazi yake na kutuletea timu ambayo inaonyesha ubora mkubwa uwanjani. Asichojua ni kwamba hata wachezaji wa Simba na Yanga muda mwingi wanacheza kwa ajili ya kuwatumikia mashabiki. Wanajituma zaidi kwa sababu hiyo na sio kwa sababu ya kocha na benchi la ufundi.

Nadhani alipokuwa Namungo, Kaze ameshuhudia wachezaji ambao wanacheza bila presha ya matokeo. Simba na Yanga kufungwa au sare sio matokeo yanayokubalika katika mechi za Ligi Kuu, lakini Namungo imecheza mechi tano mfululizo bila ushindi na hakuna anayeshangaa. Lakini hata hatima yake haikuwa gumzo pale Lindi. Vipi kama angekuwa ni kocha wa Simba na Yanga?

Lakini kuna mambo mengine ambayo alipaswa kuyajua. Namungo kusafiri na basi kwa umbali mrefu ni jambo la kawaida. Namungo kuonewa na mwamuzi ni jambo la kawaida. Zaidi ya hapo Namungo inajikuta katika wakati mgumu wa kukamiwa na timu za kawaida kwa sababu wanaiona ni timu saizi yao.

Najua nikikutana na rafiki yangu Kaze ataniambia mengi kuhusu maisha yake mafupi pale Namungo. Anaweza kuandika hadi kitabu cha malalamiko chenye kurasa nyingi kuhusu mpira wa Tanzania. Ndani ya muda mfupi tu alioishi Namungo atajua kwamba Yanga ilimuandalia mazingira mazuri ya kuwa kocha mzuri nchini.

Sio yeye tu. Majuzi Tanga walikuwa wamekutana kufanya kikao cha kumfukuza kocha Mwinyi Zahera. Huyu aliikuta Yanga ikiwa katika mazingira magumu, lakini bado akashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu. Tumuulize maisha yalikwenda vipi alipokwenda Polisi Tanzania na kisha Coastal Union ya Tanga? Naye anaweza kuandika kitabu chenye kurasa nyingi za malalamiko kuhusu mpira wetu.

Maisha sio rahisi sana nje ya Simba na Yanga. Wakati mwingine unasadiki kwamba mpira wetu uliundwa kwa ajili ya Simba na Yanga. Hata Taifa Stars ni ndogo kwa Simba na Yanga. Waulize wachezaji watakuthibitishia hiki ninachosema. Mara kibao wachezaji wamejiumiza na kukacha kambi ya Taifa Stars, lakini huwa hawawezi kuzikacha kambi za Simba na Yanga.

Nampa pole rafiki yangu Kaze. Zamani kulikuwa na timu mbili zilizowahi kutimiza ndoto zake. Ushirika ya Moshi na Pamba ya Mwanza. Zilikuwa zinaweka mpira chini na kucheza soka la kuvutia ambalo hata Simba na Yanga hawakuweza kucheza. Hata hivyo walikuwa wanatoa burudani tu, lakini hawakuweza kushindana kwa kiasi kikubwa.

Si tunakumbuka majuzi walikuja kina Deus Kaseke na Mbeya City yao? Iko wapi sasa hivi? Tangu tulipoamua kuumilikisha mpira wetu kwa Simba na Yanga maisha yamekuwa magumu kwa watu wengine ambao wapo nje ya mzunguko wao. Huu ni ukweli ambao sasa Kaze ameujua.

Inawezekana bado Namungo ilikuwa timu yenye mizengwe kwake kwa sababu ya umiliki wake, lakini nadhani mambo yangekuwa yale yale tu kwa Kaze hata kama angekwenda Coastal Union, Kagera Sugar, Prisons na kwingineko. Kuacha alama ukiwa kocha au mchezaji nje ya Simba na Yanga ni jambo gumu kwa mazingira ya mpira wetu.

Kila la heri kocha Kaze. Kwa sasa tunamsubiri pia Fei Toto. Anaweza kujikuta katika mazingira hayahaya. Nitaandika kitu kuhusu yeye wiki ijayo, lakini kwa kutoitwa tu katika timu ya taifa baadhi ya wabashiri wa mambo wanaamini inawezekana ni kutokana na kuondoka kwake Yanga.

Columnist: Mwanaspoti