Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pogba na mzimu wa Ronaldo halisi

Paul Labile Pogba Miss Qatar Paul Pogba

Fri, 18 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ni jina linalochukiwa zaidi na Wareno na mashabiki wa Manchester United. Hawataki kabisa kusikia Ronaldo de Lima akiitwa ‘The Real Ronaldo’. Kwao ni kijembe kwa shujaa wao Cristiano Ronaldo. Ronaldo halisi atakumbukwa kwa mambo matatu.

Kwanza, uchezaji wake uwanjani. Ronaldo alikuwa namba tisa halisi. Kasi yake na nguvu zake zilikuwa ushuhuda kwa kila beki aliyekumbana nae. Mabao yake ya kusisimua yanabaki kuwa njozi mbaya kwa kila kipa aliyekutana naye. Pengine mwenye simulizi nzuri zaidi ni Oliver Kahn wa Ujerumani.

Yale mabao mawili aliyomtungua kule Korea Kusini mwaka 2002, bado anayaota mpaka kesho.

Nikiikumbuka Brazil ile ya mwaka 2002, nagundua kweli soka limebadilika. Nagundua kweli kila zama na mfalme wake. Naikumbuka sura ya Ricardo Kaka, naikumbuka sura ya Ronaldinho Gaucho. Brazil kama Brazil. Ufundi mwingi kwenye miguu ya wachezaji. Ufundi mwingi kwenye benchi la ufundi likiongozwa na Luiz Philipe Scolari.

Kingine kwa Ronaldo de Lima ni maisha yake mabovu ya nje ya uwanja. Kama Wabrazil wengi, Ronaldo alikuwa mtu wa bata na pengine ni kati ya vitu vilivyoathiri sana uwezo wake. Lakini kikubwa zaidi kilichommaliza ni majeraha.

Alikuwa na mwili mkubwa wenye asili ya majeraha. Kama huyu De Lima tunamzungumza leo kama mshambuliaji hatari kuwahi kutokea, vipi kama asingeandamwa na majeraha?

Wachezaji wengi kutoka Amerika ya Kusini ni kama wachezaji wa Kiafrika tu. Ukisoma historia za wachezaji wengi wa Afrika wanakotoka na umasikini wa familia zao utagundua hakuna tofauti kubwa na wachezaji kutoka Amerika Kusini. Ukitazama maisha yao yanavyobadilika na kuwa watu wa starehe sana baada ya kufanikiwa, utagundua hawa wote ni watoto wa baba mmoja.

Ni tofauti sana na watoto wa Ulaya. Ni tofauti sana na wachezaji wanaotoka Ulaya ambao wengi wao wamekuta miundombinu na maisha ya nyumbani yakiwa yameimarika zaidi. Paul Pogba, bishoo wa Kifaransa atakosa fainali za Kombe la Dunia kwa sababu ya majeraha. Kabla ya yote, Pogba hajacheza msimu huu, ametumia takribani msimu mzima kujiuguza. Lakini kila shabiki ukimuuliza, atakuambia Pogba ana kipaji. Ni kati ya viungo mafundi wapiga pasi waliosalia duniani. Lakini haonekani uwanjani.

Haishangazi kuona baada ya Manchester United amerudi nyuma kwa kwenda Juventus. Alipaswa kwenda Real Madrid au Barcelona lakini amerudi nyuma. Majeraha yanamkwamisha Pogba kama alivyokwama De Lima.

Kuna kazi kubwa sana kwa Ufaransa kuziba majukumu ya Pogba uwanjani. Labda Pogba wa Manchester United hakuondoka vizuri na hivyo wengi wanaweza wasikumbuke mchango wake lakini, Pogba wa timu ya Taifa ni yule yule fundi wa mpira. Ni yule yule kiungo wa pasi ndefu kuelekea eneo la mpinzani. Ni yule yule fundi mwenye uwezo wa kuunganisha vyema idara ya ulinzi na ile ya ushambuliaji.

Kama kuna kiumbe anapitia wakati mgumu basi ni Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps. Historia inaonyesha bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia ameondolewa kwenye hatua za awali kwenye michuano ya Kombe la Dunia mara tatu mfululizo kuanzia msimu uliopita pale nchini Urusi.

Kingine ni kuona Deschamps anawakosa Ngolo Kante na Pogba kwa pamoja. Pamoja na mambo mengine, uwezo wa Pogba na Kante uliisaidia sana Ufaransa kutwaa ubingwa wa dunia pale nchini Urusi. Kante ni mwanadamu wa pekee anajua kutibua mipango ya timu pinzani kuliko pengine mchezaji mwingine yoyote wa kizazi hiki. Sio mtu wa maneno mengi lakini kazi yake uwanjani ni levo nyingine kabisa.

Ni kweli Ufaransa wana kijana wao Eduardo Camavinga na Aurelien Tchouameni lakini, napata wasiwasi mkubwa kama timu itakuwa salama. Kombe la Dunia sio michuano ya kujaribishia wachezaji. Ni mahali wanaume wanakuja kushindana na sio kujaribiana. Unaiona Ufaransa ikiwa salama bila Pogba na Kante?

Columnist: Mwanaspoti