Yuko wapi yule aliyesema ‘Nionyeshe marafiki zako nikutajie marafiki zako’. Alikuwa sahihi. Pep Giuardiola, achana na kukaribia kutwaa mataji matatu lakini kuna uhuni fulani hivi ametufanyia katika soka kwa sasa.
Barcelona wametwaa taji lao la La Liga. Kocha nani? Xavi Hernandez. Mtu ambaye alikuwa muhimili wa Barcelona katika staili yake ya soka wakati ule akicheza soka la hali ya juu chini ya Guardiola. Unadhani Xavi alikuwa na sehemu nyingine ya kuiga? Hapana. Ni kwa Guardiola tu.
Asingeweza kuiga kwingine na wala hakuhitaji kuwa na maarifa mengine mapya katika kufundisha soka. Alichokuwa anafundishwa na wenzake ndicho ambacho aliwaambia kina Gavi na Pedri wakafanye uwanjani.
Unachukua mpira hapa, unauachia kwa haraka, unachukua nafasi. Hakuna kubutua kwa urahisi. Inabidi ulazimike kweli kweli ili uweze kubutua lakini vinginevyo mpira inabidi utembee hapa na pale. Ukipoteza mnakaba wote kuanzia juu na katika kila eneo. Wenyewe wanaita kwa lugha ya kiingereza ‘pressing’.
Pale England, Vincent Kompany ameipandisha Burnley daraja kwa staili ya aina yake. Wameonea sana watu. Wamekandamiza watu. Wamenyanyasa watu. Mwishowe wamepanda daraja kwa kuvunja rekodi ya pointi. Wamemaliza wakiwa na pointi 101.
Wamepanda daraja mapema lakini pia wakafanikiwa kuchukua ubingwa. Pale daraja la kwanza unaweza kupanda daraja mapema lakini usichukue ubingwa. Ndio, unaweza kupanda daraja halafu ukaanza kumwaga pointi na kisha kupitwa na wa pili.
Kompany amefanya vyote kwa usahihi, tena kwa kuvunja rekodi mbalimbali. Alichofanya ni kitu rahisi tu. Amekopi mpira wa Pep na kuupeleka daraja la kwanza kwa ajili ya kutesea watu. Hauwezi ukawa mwanafunzi wa Pep katika hatua fulani ya maisha yako halafu ukaenda mahala kufundisha mpira wa Jose Mourinho au Sir Alex Ferguson. Haiwezekani.
Na sasa Kompany ameanza kutakiwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya England. Aliwahi kutajwa kutakiwa na Chelsea na Tottenham. Wanajua kwamba huyu ni mwanafunzi wa Pep na kwa njia za kichina wanaweza kujikuta wakicheza kama Man City endapo watampata Kompany.
Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba Burnley inakuja kusumbua vigogo kama hawatakaa sawa. Niliwahi kutazama pambano lao la Carabao dhidi ya Manchester United msimu huu nikaona wazi kwamba wanakuja kusumbua wakubwa msimu ujao. Kompany ameiga vitu vingi kutoka kwa Master wake.
Vipi kuhusu Mikel Arteta? Msimu huu amewaburuza wengi. Huyu hakucheza chini ya Pep lakini alikuwa msaidizi wake. Alichofanya ni kuuchukua mpira wa Pep na kuupeleka Emirates. Bahati mbaya kwake ni kwamba vijana wake walikosa pumzi mwishoni.
Hakuwa na wachezaji wengi wa kuwabadili mara kwa mara na kwa staili hii ya mpira wa Pep ilikuwa lazima Arsenal wachoke dakika za mwisho. Vyovyote ilivyo watu wengi waliamini kwamba Arteta alikuwa anaingia msimu huu kusaka Top Four, kumbe akajikuta anasaka ubingwa.
Kitu kingine ambacho kilimzuia Arteta asifanye kile ambacho kimefanywa na Xavi na Kompany ni ukweli kwamba alikuwa katika Ligi moja na bosi wake Pep. Sio rahisi sana kumshinda Master wako. Ilionekana katika mechi zote ambazo City alicheza na Arsenal, lakini pia imeonekana namna ambavyo City wamemaliza kwa nguvu katika michuano yote. Bado Arteta anajifunza kwake.
Kama Arteta angekuwa anaucheza mpira huu katika Ligi nyingine si ajabu angekuwa bingwa. Tatizo alikuwa anaucheza mchezo huu katika Ligi ambayo pia Mwalimu wake yupo. Pointi zake zingeweza kutosha katika ubingwa kama angekuwa yupo kwingineko. Bahati mbaya alikuwa Ligi moja na Pep.
Na sasa ni wazi kwamba Pep ameanza kutuletea wanafunzi wake ambao nao wanasumbua katika soka. Awali kuna watu wengi wamejaribu kuiga mpira wake bila ya mafanikio. Wengi wao hawakutoka katika ubavu wake.
Tabia kama vile kipa kutumia miguu yake vema zaidi kuliko hata mikono. Tabia ya mpira lazima uanze kuchezwa nyuma. Tabia za kukabia juu (pressing). Hizi nyingi kuna makocha mbalimbali ambao wameanza kuziiga ulimwenguni kote.
Hata hivyo makocha hao hawajawa wanafunzi wazuri kuliko wale ambao walipita katika mikono ya Pep mwenyewe. Waliopita katika mikono yake mwenyewe wawili wametwaa ubingwa wakati mmoja alimshinda mwenyewe katika mbio za ubingwa.
Na muda si mrefu nadhani akina David Silva watastaafu soka na wao watakuja kutusumbua. Kelvin de Bruyne naye anasomea ukocha kwa sasa. Unadhani ‘role model’ wake ni nani? Wote hawa watakuja kutuletea mpira wa Pep Guardiola.
Baada ya Kompany nasubiri kuona mchezaji mwingine mstaafu wa Barcelona, Bayern Munich au Manchester City akituletea mpira huu wa kisasa ambao kifupi unasumbua dunia kwa sasa. Kila kocha angependa kuwa Pep
Unadhani watakuja kufundisha mpira wa Jose Mourinho au Diego SImeone? Hapana. Watatutelea mpira wa Pep na kutusumbua. Labda kama mpira wenyewe utakuwa umepitwa na wakati. Na sijui wakati huo tutakuwa tunacheza soka la namna gani.
Nadhani hawa akina Arteta wamenufaika katika mambo mengi ya kumuandaa mchezaji nje ya uwanja. Ukitazama namna ambavyo wachezaji wao wapo fiti kuucheza mfumo wenyewe inakupa picha kwamba kuna maandalizi mengi yanafanyika nyuma ya pazia.
Kuna makocha wengi wa zamani ambao walikuwa hodari lakini sidhani kama walitutengenezea makocha wengine waliomudu kufanya vile vile vile ambavyo wao walikuwa wanafanya. Haishangazi hata kuona kwamba mtu kama Sir Alex Ferguson hakutuachia makocha bora ambao zamani walikuwa wachezaji wake.
wachezaji wengi waliocheza chini ya Ferguson hakuwa makocha wazuri. Hata wachezaji wengi waliocheza chini ya Arsene Wenger hawakuja kuwa makocha wazuri.