Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pensheni ya wanamichezo itasaidia sana

Steven Gerrard Pensheni Frank Lampard

Sun, 30 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wanamichezo ni miongoni mwa waajiriwa ambao ajira zao hudumu kwa muda mfupi. Mpira wa miguu ni mfano mzuri, Shirikikisho la Mpira wa Miguu ulimwenguni (Fifa), linakadiria umri wa mchezaji kustaafu kuwa kati ya miaka 32-34 yaani akiwa ametumika miaka 10 au zaidi kidogo kwa wachezaji walio wengi.

Wakati huo, wafanyakazi katika sekta nyingine ndiyo kwanza wanahesabu miaka kama 30 mbele ya kuendelea kuajiriwa. Baada ya miaka mingi ya kufanya kazi inayotumia nguvu nyingi, wanamichezo hufika mahali wakakosa umiliki wa miili yao, yaani akili inataka kufanya jambo lakini mwili hauko tayari kutii.wachezaji wengine hupata majeraha au magonjwa yanayoweza kuwalazimisha kustaafu mapema.

Baadhi ya wanamichezo hurudi kuajiriwa kwenye michezo yao katika majukumu tofauti baada ya kustaafu mfano kwa kuwa waalimu, waamuzi, wataalam wa viungo na hata wachambuzi wa habari.

Wako waliofanikiwa kama wanamichezo na kufanikiwa pia kama wataalam kwenye michezo waliyohusika nayo. Dunia imejaa maofisa wa michezo waliokuwa wachezaji.

Wako wanaofanya kazi kama makocha mfano wa wachezaji wa karibuni kwa upande wa soka ni kama Frank Lampard na John Terry Wa Chelsea, Steven Gerard wa Liverpool, Thierry Henry na Patrick Vierra wa Arsenal, Vincent Kompany wa Manchester City; idadi ni kubwa.

Hata hivyo, siyo wachezaji wote hubahatika kurudi na kupata ajira katika mchezo waalioufanya mfano soka, ngumi, riadha, kikapu na kadharika hivyo uanza kutafuta maisha mengine baada ya kustaafu.

Wako waliotumia nafasi zao za zamani kujiingiza katika siasa mfano ni Rais w sasa wa Liberia George Weah aliyekuwa mcheza soka,Rais wa 36 wa Marekani Dwight D Einsenhower aliyecheza kikapu na michezo mingine na bondia Manny Pacquiao aliyepata kuwa mbunge. Orodha ni ndefu

Hadithi za wanamichezo waliofanikiwa ni utamu kolea kweli kwani michezo ni moja ya ajira zinazolipa sana na kumfanya mtu maarufu hasa anapocheza kwa kiwango cha juu. Ni watu wachache duniani wasiojua jina la Pele au Maradona, Mwenyezi Mungu awarehemu.

Si watu wengi wanajua jina la rais wa Brazil auwa rais argentina. Hata hivyo, upande wa pili wa hadithi za wanamichezo wastaafu ni wa kusikitisha;ni jinamizi.

Wanamichezo wengi baada ya kustaafu wamejikuta wanabadilisha mtindo wa maisha ghafla hasa katika umri mdogo wa chini ya miaka 40. Vipato vimepungua,ajira za maana hakuna basi maisha yakaonekana kwenda kinyume na wao.

Wako waliojikuta katika migogoro ya ndoa, madeni, unywaji kupindukia na hata utumiaji wa madawa ya kulevya.Wako wanamichezo waliojaribu kukatiza uhai wao kutokana na msongo wa mawazo.

Huku kwetu Afrika,ni wanamichezo wachache hufanikiwa kupata ajira za kueleweka baada ya kustaafu.Michezo kwa ujumla haijawa chanzo kikubwa cha mapato kama nchi zilizoendelea.

Huko nyuma ,kwa nchi nyingi za Afrika michezo ilichukuliwa kama shughuli ya burudani baada ya kazi.Haishangazi wazazi waliwahimiza watoto wao kuzingatia masomo na kuepuka michezo.Hata sasa jamii kubwa bado inachukulia michezo kama michezo.

Wako wanamichezo ambao baada ya kustaafu wamekuwa hawana shughuli ya maana ya kufanya kiasi cha kugeuka ombaomba.Kwa bahati mbaya sana,michezo yenyewe na jamii kwa ujumla haikuwaandalia mazingira ya baada ya kustaafu.Hadithi za wanamichezo wastaafu wengi ni za kusikitisha.

Tumekuwa tukisikia maombi ya michango kwa ajili ya tiba za wanamichezo wastaafu. Watu wengine wamekwenda mbali na kulaumu waajiri wa zamani kama vilabu lawama ambazo nadhani si za haki.

Klabu ni mwajiri kama walivyo waajiri wengine hivyo wanabeba lawama pale ambako wamekwenda kinyume na makubaliano ya ajira kwa wachezaji kama walivyo wafanyakazi wengine. Klabu haipaswi kulaumiwa kwa changamoto zinazowakuta watumishi wao wa zamani miaka mingi baada ya kustaafu.

Hata hivyo, kama ambavyo klabu na taifa zinajivunia mafanikio waliyoleta wanamichezo basi itapendeza kama wanakuwa sehemu ya mpango wa maisha bora ya wanamichezo baada ya kustaafu.

Katika baadhi ya nchi zilizoendelea,pamoja na wanamichezo kupewa nafasi ya utumishi katika michezo na nyanja zingine, jamii pia imeandaa mazingira mazuri kwao kwa ajili ya wakati ambao kipato kinaingia kwa wingi na hata kipato kitakapopungua au hata kukauka kabisa.Bima ya wanamichezo ni moja ya suluhu za ugumu wa maisha ya wanamichezo hasa waliostaafu.

Mfumo wa bima au pensheni za wanamichezo hufanya kazi kama mifuko mingine ya pensheni kwa kuwakata kiasi fulani wanamichezo kutoka mishahara yao na pia mwajiri na idara ya serikali inayohusika na michezo kuchangia kiasi kingine hivyo kuwawezesha wanamichezo kupata mafao kiasi fulani na huduma kama ya matibabu baada ya kustaafu.

Nchini Uingereza, chama cha wachezaji wa kulipwa (PFA) kina mfuko wa pensheni ambao huwaudumia wachezaji na wategemezi wao.Mchezaji huchangia asilimia Fulani ya kipato chake na mwajiri pia huchangia.Mchezaji anaweza kuanza kuchukua pensheni kwenye umri wa miaka 55 au hata chini yake ikiwa ana changamoto za maisha au afya.

Imefika wakati hapa kwetu,wadau wa michezo ikiwemo wizara inayohusika na michezo kutafuta namna ya mafao kwa ajili ya wanamichezo wetu.Hatua hii itahamasisha wazazi kuwahimiza watoto wao kujihusisha na michezo kwani zile hadithi za mwisho mbaya zitapungua.

Pensheni na bima za wanamichezo zitapunguza gharama za matibabu kwa wanamichezo wastaafu waliokuwa wakiangukia katika uraibu na mitindo mibaya ya maisha kutokana na msongo wa mawazo baada ya kukosa kipato. Pensheni kwa wanamichezo wanaoingiza kipato leo liwe jambo la lazima ili kuepusha mzigo wa gharama na lawama kesho.

Columnist: Mwanaspoti