Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pan ilinyimwa ubingwa 1978

Mjuaji Pic Pan ilinyimwa ubingwa 1978

Tue, 18 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Julai 29, 1978 Simba ilimtumia mchezaji Mohammed Bakary ‘Tall’ katika mchezo wa Ligi ya Taifa dhidi ya Pan African kwa mara ya kwanza.

Ikumbukwe pia, mchezaji huyo aliyeitwa ‘Tall’ kutokana na urefu wake, aliwahi pia kuitumia Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam pia.

Kitendo cha Simba kumchezesha Tall kiliifanya Pan kukata rufaa kwa kuwa mchezaji huyo tayari alishacheza ligi hiyo na sheria ilikuwa hairuhusu mchezaji mmoja kuzitumikia timu mbili kwenye msimu mmoja wa ligi.

FAT YAPOTEZEA

Hata hivyo, Chama cha Soka cha Tanzania (FAT) na IFOZA. Baada ya kukataliwa, Pan ilikwenda mbele zaidi kwa kuifikisha rufaa yake kwa Baraza la Michezo (BMT) kabla ligi ya msimu huo haijaingia hatua ya pili.

Agosti 5, 1978, BMT iliitaarifu Pan haitaweza kuingilia rufani yao mpaka Ligi ya Taifa ya msimu huo itapomalizika.

SIMBA YATWAA UBINGWA

Ligi ya Taifa ya mwaka 1978 ilipomalizika, Pan African ilishika nafasi ya pili na kutakiwa kushiriki Kombe la Washindi Afrika.

Wakati Simba ilitwaa ubingwa wa na kuwakilisha nchi katika Klabu Bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika).

Hapo ndipo Mwenyekiti wa BMT, Joseph Mungai alipojitokeza mbele ya waandishi wa habari na kudai FAT ilifanya makosa kuiruhusu Simba kumtumia Tall kwenye msimu huo wa ligi.

Hata hivyo, Mungai alisema ni baraza lake lisingeweza kuchukua hatua yoyote zaidi ya kuipa onyo FAT. “Ni vigumu kufanya uamuzi mwingine zaidi ya kuipa onyo FAT,” alisema Mungai

PAN YACHARUKA

Baada ya taarifa ya BMT, viongozi wa Pan African walicharuka na kutaka kupewa ushindi katika mchezo dhidi ya Simba na itangazwe kuwa bingwa wa Ligi ya Taifa. Laiti kama Simba ingepokonywa pointi mbili na mabao mawili, Pan African ingetangaza ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Taifa.

Lakini Pan ilibidi kusubiri baada ya miaka minne kuweza kutwaa ubingwa Tanzania. Katika hali ya kukata tamaa, Pan iliishutumu BMT kwa kujiingiza katika njama za FAT na Simba za kuvunja sheria kwa makusudi ili kuipatia Simba ubingwa usiokuwa wa halali.

Klabu hiyo ilisema licha ya BMT kukubaliana na Pan kuwa Tall aliitumikia Simba kimakosa, haikuchukua hatua zozote na hivyo, Pan imelazimika kukosa haki yake kutokana na makosa ya watu wengine.

Pan ilisema ilishangazwa na kitendo cha BMT kuilamu FAT na kushindwa kuchukua hatua dhidi ya Simba ambayo ilifahamu wazi kumchezesha Tall ilikuwa ikifanya makosa kinyume na sheria za Ligi ya Taifa.

Pan ilisema kabla ya ligi kuanza, sheria pamoja na taratibu za ligi ziligaiwa kwa klabu ili makosa kama hayo yasijitokeze.

Simba ilimuona Mohamed Tall akiichezea timu ya Ruvu Stars, ndipo ilipoimba FAT iiruhusu imtumie kwenye ligi.

“Simba kama wangekuwa hawajui sheria wasingeomba ruhusa kutoka FAT kama mchezaji wao,” taarifa ya viongoziwa Pan ilisema na kuongeza.

“Kwa mantinki hii tunaamini Simba na FAT walishirikiana kumchezesha Tall kwenye klabu mbili katika msimu mmoja, kinyume na kifungu cha sheria namba 5.3.” Pan ilisema sheria inapovunjwa klabu iliyofanya makosa inanyimwa ushindi kutokana na sababu hizo ilidai haki yake ya kupewa pointi mbili na mabao mawili.

WATINGA KWA WAZIRI

Kama vile haitoshi, Pan haikutaka kuishia kwa BMT tu, bali iliamua kumwandikia barua waziri wa utamaduni wa taifa na vijana kumataka kuingia suala hilo ili haki itendeke. Hata hivyo, haki haikutendeka na Pan haikupewa haki yake 1978.

HATA YANGA WAMO

Mwaka 1987, katika mchezo wake wa kwanza, kiungo Athuman Abdallah ‘China’ aliichezea Yanga dhidi ya Majimaji ya Songea.

Lakini baada tu ya mchezo huo ambao Majimaji ilipoteza ilikata rufaa dhidi ya Yanga kwamba mchezaji huyo alikuwa mchezaji halali wa Timu ya Ligi Daraja la Nne ya Tumaini lakini Majimaji ikaambiwa ilichelewa kukata rufaa.

China hakucheza tena hadi alipokuja kusajili msimu unaofuata kama mchezaji huru kutoka kikosi cha pili.

HISTORIA YA PAN

Pan African ni klabu iliyotoka ubavuni mwa Yanga African kutokana na mgogoro uliochukua muda mrefu zaidi ndani ya Yanga kuanzia 1974-1975, Yanga ilipopasuka vipande viwili.

PAN YASAJILIWA RASMI

Agosti 1976 Pan African ilisajiliwa rasmi Wilaya ya Ilala baada ya kuwekewa ngumu kwa muda na serikali kwa kutosajiliwa klabu yoyote.

Ugumu huu ulitokana baada ya viongozi wa Simba waliojiengua mwaka 1975 na kwenda kuanzisha timu ya Nyota Nyekundu ‘Red Star’.

Hatimaye, viongozi waliojiengua kutoka Yanga walizungumza na Klabu ya Zamalik (Zama za Kale) ya Upanga jijini Dar es Salaam iliyokuwa timu ya maveterani waliokuwa wakifanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zao na kukubaliwa kubadilisha jina na kuitwa Pan Afrika.

Pan iliwahi kushinda mataji ya Kombela Nyerere miaka ya 1978, 1979 na 1981. Mwaka 1983 ilitolewa raundi ya pili ya Klabu Bingwa Afrika na 1989 ilitolewa raundi ya awali.

KOMBE LA WASHINDI

Mwaka 1979 iliwahi kushiriki Kombe la Washindi Afrika na kutolewa raundu ya pili.

Pia ilishiriki kombe hilo tena katika miaka ya 1980 na 1982 na mara zote kutolewa raundi ya pili. Pan African ilishuka daraja mwaka 1984.

Columnist: Mwanaspoti