Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Pamoja na corona, magonjwa mengine pia yasisahaulike

B0c945ee9d24e4f6f38195bcdcb7a1bb Pamoja na corona, magonjwa mengine pia yasisahaulike

Fri, 26 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ipo kwenye vita na mapambano dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (covid 19).

Ugonjwa huo tangu uibuke nchini China mwaka jana, mpaka sasa umesambaa takribani duniani kote na kusababisha vifo vingi vinavyofikia watu milioni 2.49.

Kwa mujibu wa tovuti ya worldometers jumla ya watu wanaofikia milioni 112.7 wamepata maambukizi ya ugonjwa huo duniani kote, kati yao milioni 2.49 wamekufa na milioni 88.28 wamepona.

Ukweli ni kwamba, tangu ugonjwa huo uibuke nchi nyingi zimekuwa katika hali mbaya kutokana na uamuzi wa kuzuia shughuli zote muhimu na wananchi wake kutakiwa kutotoka nje kama tahadhari ya kudhibiti kuenea zaidi.

Kupitia tovuti hiyo, nchi zinazoongoza kwa maambukizi na vifo vya ugonjwa huo ni Marekani, India, Urusi, Brazil na Uingereza.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo pia zimeathirika na ugonjwa huo kama nchi nyingine ingawa kutokana na msimamo wa serikali ya Rais John Magufuli nchi imefanikiwa kuudhibiti ikilinganishwa nan chi nyingine.

Hata hivyo, kwa kuwa Tanzania si kisiwa na kwa kuwa nchi zinazopakana nayo zimeendelea kushambuliwa na ugonjwa huo, nayo imelazimika kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona.

Tahadhari hiyo ni pamoja na wananchi kutakiwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya kwa kunawa mikono na maji yanayotiririka, kutumia vitakatisha mikono, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja baina ya mtu.

Hata hivyo, siku hizi za karibuni tangu kuibuka tena kwa janga hilo, wananchi wengi wamekuwa na hofu kutokana na baadhi ya watu kuendekeza uzushi hususani inapotokea misiba.

Sasa hivi imekuwa kawaida mtu anapokufa hata bila kutambua sababu ya kifo chake ni kawaida kusikia kuwa amekufa kwa corona.

Kila mtu anatakiwa kuchukua tahadhari lakini ukweli unabaki kuwa bado yapo magonjwa mengine ambayo ni hatari na yanahitaji kudhibitiwa pia lakini ni kama vile watu sasa hawatambui uwapo wake.

Magonjwa kama shinikizo la damu, saratani, kisukari, malaria, ukimwi, kifua kikuu na mengineyo bado ni changamoto kubwa katika jamii na yanahitaji kupewa kipaumbele.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel alibainisha kuwa si kila anayekufa kwa kushindwa kupumua ni kutokana na tatizo la corona.

Alieleza kuwa tatizo la kushindwa pumua linashika namba mbili kwa vifo nchini na duniani kwa ujumla.

Anasema magonjwa kama vile nimonia, kisukari na ugonjwa wa moyo yote dalili zake ni mgonjwa kushindwa kupumua vizuri.

Dk Mollel hakuishia hapo bali alielezea takwimu za magonjwa yanayoongoza kuua nchini kuanzia mwaka 2006/2015 kuwa ni malaria asilimia 12.7, magonjwa ya kupumua asilimia 10.8, ukimwi asilimia 8.4, matatizo ya damu asilimia 7.7 na ugonjwa wa moyo asilimia 6.3.

Kutokana na takwimu hizo, ni wazi kuwa kuna kila sababu ya Watanzania pamoja na kupambana na corona, lakini pia kutoyapuuzia magonjwa mengine ambayo nayo ni hatari kwa maisha yao.

Kama ilivyo kwa corona, malaria, ukimwi, shinikizo la damu au magonjwa ya moyo, sukari na mengineyo, bado ni hatari na magonjwa hayo yanapaswa kudhibitiwa kwa hali na mali.

Mtu akiumwa kwa sasa hisia isiende kwenye corona tu, bali pia izingatie magonjwa mengine na kubwa zaidi ni kuwahi hospitali kupata tiba na ushauri wa watalaamu.

Hivyo basi, mamlaka husika kama vile Wizara ya Afya, taasisi na asasi zinazoshughulikia masuala ya afya hazina budi kuelimisha jamii juu ya kuendelea kuchukua tahadhari si tu kwa corona, bali pia magonjwa mengine hatari kwa maisha ya binadamu.

Hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa endapo nguvu kubwa pekee zitaegemea kwenye kudhibiti corona pekee, kuna uwezekano magonjwa mengine yakaendelea kumaliza nguvu kazi ya taifa kama yasipodhibitiwa.

Columnist: habarileo.co.tz