Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

PAZIA LA UCHAGUZI: Wazee Mbeya wanasubiri tu Oktoba 28 wafanye yao

636b8157f8772a764f4c4d789607a002 PAZIA LA UCHAGUZI: Wazee Mbeya wanasubiri tu Oktoba 28 wafanye yao

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI Chama Cha Mapinduzi kikiwakumbusha watanzania yaliyofanywa na serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ili wakichague tena mwaka huu, wazee mkoani Mbeya wanasema walishafanya tathmini yao ni nani watampa kura.

Wazee hao wa Mbeya wanasema haikuwachukua miezi mingi baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 kugundua kwamba John Magufuli alikuwa chaguo sahihi kupewa kiti cha urais na kwamba anastahili kuongezewa muda wa kuongoza.

Wanasema ukongwe wao umetosha kumtathmini ndani ya muda mfupi na ndiyo sababu hata katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wao ni kama vile wanasubiri tu siku ifike.

Wazee wanatoa kauli hiyo walipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya hivi karibuni.

Wanasema wameridhishwa kwa kiasi kikubwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli tangu alipoapishwa kuongoza nchi, ikiwa ni pamoja na kutowaonea aibu mafisadi, wazembe na wezi wa mali ya umma.

Mengine yanayowakosha wanasema ni kuibua na kujenga miradi mikubwa ya kimkakati, kusimamia vyema matumizi sahihi ya fedha za walipa kodi na kutimiza ndoto nyingi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ndoto hizo wanazitaja kuwa ni pamoja na kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuzalisha umeme, kulirudishia uhai shirika la ndege ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Nyerere iliyoko Kwanga mjini Musoma iliyosimama kwa takribani miaka 40 na mengine mengi.

“Shirika la ndege lilikuwa na heshima wakati wa Nyerere na leo tunaona heshima yake inarejea baada ya Dk Magufuli kununua ndege. Tulikuwa na viwanda ambavyo hapo katikati vilipotea lakini leo tunaona vingi vinafufuliwa. Haya ndiyo yalikuwa maono ya Mwalimu Nyerere,” anasema Mwenyekiti wa umoja wa wazee jijini Mbeya, Isakwisa Mwambulukutu akiwakilisha pia mawazo ya wenzake.

Anaongeza: “Lakini pia tunashuhudia uadilifu mkubwa sasa uliopo wa watumishi wa serikali. Ilifika wakati ilikuwa vigumu wasio na sauti kusikika kwa kuwa hawakuwa na pesa. Leo hii hata watu wa chini tunasikilizwa na kupewa nafasi. Naona namna pia watu mnaoteuliwa na Rais (ukiwemo wewe mkuu wa mkoa) mnavyojituma katika kutekeleza majukumu yenu tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.”

Katika mkutano huo wa kufahamiana uligubikwa zaidi na kueleza jitihada zinazofanywa na Dk Magufuli katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo kusimamia miradi iliyokuwa imekufa.

“Sisi wazee pia tumeridhika na uteuzi wako na jinsi kazi ulivyoifanya kwa kipindi chako kifupi… Tunakupongeza sana mpaka sasa,” anasema Mwambulukutu.

Akielezea zaidi kuhusu ufufuaji wa Shirika la Ndege, Mwambulukutu anasema takribani wazee wote waliokuwa ukumbini wanakumbuka namna Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Shirika la Ndege la Tanzania baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini alipokufa na lenyewe likafa.

Mwambulukutu anasema wanashangaa kuona baadhi ya watu wakibeza hatua ya serikali kuimarisha shirika hilo la ndege wakiwemo wabunge wa upinzani waliokuwa wakishangaa nchi kukosa ndege.

Mwambulukutu anasema ufufuaji wa Shirika la Ndege umenyanyua hadhi na heshima ya Tanzania kimataifa.

“Tumekuwa tukifuatilia nini kimekuwa kikifanyika katika nchi yetu, sijui wazee wenzetu wa mikoa mingine lakini sisi hapa Mbeya tumetosheka sana… Rais ameleta elimu bure katika nchi hii, mashule yanaboreshwa, vyuo vinajengwa. Kazi yote ameifanya kwa kipindi chake kifupi sasa sijui wanataka afanye nini? Sisi wengine kwa sasa hatuna watoto wa kusomesha, ninyi mlionao mnasomesha bure kuanzia darasa la kwanza mpaka sekondari, kusomesha siyo kazi nyepesi.”

Huku akiungwa mkono na wazee wenzake, Mwambulukutu anagusia eneo la afya akitaja namna Magufuli alivyoongeza bajeti ya dawa, akaongeza maradufu vituo vya afya na maboresho mengi yanayofanyika katika mahospitali nchini.

Akizungumzia viwanda, Mwambulukutu anasema: “Enzi za Mwalimu viwanda vilikuwepo nchi hii. Ninyi wazee wenzangu mnajua tulikuwa na viwanda vingapi hata hapa Mbeya lakini vyote vikafa. Sasa kiongozi wetu huyu Magufuli anafufua viwanda vilivyokuwepo na anaendelea kujenga vingine, sasa wazee kweli tusimpongeze! Tulitaka atufanyie nini watanzania?” Anahoji.

Mwambulukutu anasema Magufuli ni zawadi kwa Watanzania na hasa alivyomudu kusafisha rushwa nchini iliyokuwa kama imeshindikana.

“Tulikotoka huko nyuma, rushwa ilikithiri sana, ikawa kama kitu cha kawaida kabisa. Hata kama bado rushwa ipo lakini imepungua kwa kiasi kikubwa… Hili lazima mkuu wa mkoa tumpongeze rais wetu kwa kazi kubwa aliyofanya,” anasema.

Kiongozi huyo wa wazee wa Mbeya anasema Watanzania wana kila sababu ya kumchangua Magufuli kwa kuzingatia namna alivyosimamia mapato ya nchi, hali ambayo imesaidia sana miradi mingi ikiwemo ya vituo vya afya, barabara, reli na kadhalika kujengwa.

“Bila usimamizi mzuri wa mapato ya ndani ingekuwa ndoto kufanyika kwa miradi mingi tunayoona. Sisi wazee tumeridhika na kama wapo watu wanasema hawajaridhika basi ndivyo baadhi ya binadamu walivyo. Hata ufanye nini hawaridhiki,” anasema.

Mwambulukutu pia hakuacha kuumwagia sifa uongozi wa mkoa wa Mbeya na wilaya zake akisema walijipanga kwa umoja na kuendesha mambo kwa utaratibu uliowakosha wakati wa ziara ya Rais Magufuli aliyoifanya mkoani hapa Aprili hadi Mei mwaka huu.

Chifu Rocket Mwanshinga, kiongozi wa kimila wa kabla la Wasafwa ambao hasa ndio wenyeji wa jiji la Mbeya anasifia kazi nzuri inayofanywa na Dk Magufuli pamoja na wateule wake akiwemo mkuu wa mkoa wa Mbeya.

“Kwa sisi machifu wa mkoa wa Mbeya tunashukuru kuwa karibu na kijana wetu, mkuu wa mkoa. Kijana unafuata nyayo za Rais wetu Magufuli katika kujenga mkoa bila kuangalia ukabila, rangi wala dini,” anasema Chifu Mwanshinga.

Anampongeza mkuu huyo wa mkoa hasa aliposhirikisha wazee wakati wa ziara ya Rais Magufuli Mbeya.

Kwa upande wake, mmoja wa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Helena Mwaipasi anamtaka rais kuwapuuza wachache wanaobeza yanayofanywa na serikali yake akisema wana vijiba vya moyo kiasi kwamba wanaumizwa na maendeleo yanayofanyika.

“Rais Magufuli namwita kijana wangu kwa sababu mimi ni zao la TANU. Nasema rais huyu ametushushia Mungu kwa kuwa anatujua mahitaji yetu,” anasema bibi huyo ambaye wakati nchi inapata uhuru alikuwa binti anayejitambua vizuri, akishuhudia bendera ya mkoloni ikishushwa na kupandishwa ya Mtanzania.

“Rais wetu anatujali sana Watanzania. Hawa wanaotaka kuharibu amani Mungu atawaona. Wanaoanza kuzungumza vitu na walikuwa ndani halafu leo wanazungumza vitu vya kuharibu kwa kweli ni mbaya sana.

“Mimi namwomba Magufuli Mungu amsaidie… Amshushie amani ndani ya moyo wake wala asijisikie hofu. Mungu yupo atamlinda na atamlinda kwa kazi zake nzuri ambazo anatufanyia sisi wananchi,” anasema Mwaipasi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Chalamila, anawataka wazee mkoani Mbeya kuendelea kutambua na kuthamini maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na wasije wakahadaiwa na waongo wanaojaribu kupaka matope mafanikio yaliyofikiwa.

Chalamila anasema umakini na ufuatiliaji wa karibu wa Dk Magufuli umewezesha uadilifu mkubwa kufanyika, hatua iliyosababisha hata miradi karibuni yote kutekelezwa kwa gharama stahiki tofauti na ilivyokuwa awali.

Mkuu huyo wa mkoa anaahidi kuendelea kushirikiana na wazee kwa kuwa wanayo mambo mengi ya kushauri na yeye kujifunza kutoka kwao.

Columnist: habarileo.co.tz