Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nyuma ya pazia : Ronaldinho, Zidane wangemudu soka la kisasa?

Zidane Pic Data Zinedine Zidane

Sun, 29 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi maisha yanavyokwenda kasi unaweza kudhani hili ni swali la kipuuzi. Subiri kwanza. Namna wachezaji wa leo walivyozidiwa vipaji na Ronaldinho Gaucho na Zinedine Zidane, halafu anatokea mjinga mmoja anahoji kama Zidane na Ronaldinho wangeweza kutamba dunia ya leo.

Sio swali rahisi sana. Hawa akina Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Mikel Arteta na wengine wametuharibia vipaji kwa sasa halafu wameunogesha mchezo wenyewe wa mpira wa miguu. Hawa ndio ambao wanatuletea swali hili.

Zamani tulikuwa na vipaji vitamu kuliko timu zenyewe. Siku hizi tuna timu tamu kuliko vipaji vyenyewe. Utaamua mwenyewe uchague kitu gani. Dunia ya kileo si ajabu mchezaji kama Gaucho asingekuwa kama alivyokuwa katika dunia ya kizamani.

Akina Ronaldinho na Zidane walikuwa wanafurahia kitu kinachoitwa Free role. Walikuwa wanafurahia kuupokea mpira na kuufanyia mambo. Waliufanyia mpira mambo ya ajabu ambayo wachezaji wengine wasingeweza. Wametuachia kumbukumbu tamu.

Hawa akina Pep hawataki tena hivyo siku hizi. Wanataka kitu zaidi ya kuufanyia mambo matamu. Wanataka ucheze kitimu. Ukabe kuanzia juu. Mpira ukipenya kuingizwa katikati inabidi ugeuke na kwenda kukaba tena. Ukirudi nyuma inabidi urudi ukabe tena.

Zamani ulikuwa ukigeuka tu unaangalia nyuma. Patrick Vieira anakukabia. Claude Makelele anakukabia. Manu Petit anakukabia. Roy Keane anakukabia. Siku hizi mpira huo umeisha. Wale wote wanaocheza free role miongoni mwa sifa zao kubwa ni kukaba.

Pale Manchester City kuna Kevin de Bruyne. Kazi yake kubwa ni kusambaza mipira na kupiga pasi za mwisho. Ni kazi zile zile za akina Ronaldinho. Lakini zaidi ya hapo anakaba kama kichaa. Pale Arsenal kuna Martin Odegaard. Akaichezesha timu vema lakini anakaba kama mwehu.

Rafiki yangu Mikel Arteta aliachana na Mesut Ozil akaamua kumchukua Odegaard. Usingeweza kumuelewa kwa wakati ule lakini ukweli kwa sasa unamuelewa. Tangu Mvivu Ozil aondoke Arsenal inacheza kitimu zaidi.

Subiri kwanza. Kuna Barcelona ya moto zaidi ya ile ya Pep Guardiola? ilikuwa ina vipaji maridhawa lakini ambavyo vinakaba kila mahala. Ukilinganisha utatu wa Deco, Ronaldinho na Samuel Etoo na ile timu yao iliyokuwa chini ya Franck Rijakaard utagundua kwamba kwa mchezaji mmoja mmoja walikuwa na vipaji lakini kamwe hawakuhi kufikia makali ya Barcelona ya Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Lionel Messi.

Watazame Liverpool wa Jurgen Klopp. Walikuwa wanakabia kuanzia kule juu. Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino utatu wao ulikuwa na makali wakati una mpira na wakati hauna mpira. Walikuwa wanakabia juu mpaka chini.

Huu mpira akina Zidane hawakuwahi kuucheza. Haishangazi kuona zamani viungo wa ulinzi walikuwa wanang’ara kwa sababu kazi ya ulinzi ilikuwa ikabakia kwao zaidi na mabeki. Leo viungo wengi wa chini sio wa ulinzi tena. Ni viungo ambao wanakaa na mipira ‘Holding midfielders’.

Jinsi alivyokuwa anacheza Patrick Vieira ni tofauti na ambavyo Thomas Partey anacheza. Ni nadra kumkuta Partey anafanya ‘tackling’ kama alivyokuwa anafanya Vieira. Ni nadra kukuta Fabinho anafanya ‘tackling’ nyingiu kama Javier Mascherano alivyokuwa anafanya. Ni nadra kukuta Jorginho anafanya ‘tackling’ nyingi kama Claude Makelele alivyokuwa anafanya.

Wachezaji wote wa timu yako wanarudi kwa haraka na kubana nafasi za kati na pembeni. Huu ndio mpira wa kisasa ambao umetuacha tukicheza kitimu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani ambapo wachezaji walikuwa wanacheza mmoja mmoja zaidi.

Desemba 2019 wakati City walipoichapa Arsenal mabao matatu pale Emirates, De Bruyne alisikika akidai kwamba walikuwa wametumia vema upenyo wa wachezaji wa mbele wa Arsenal, Pierre Emerick Aubamayeng, Mesut Ozil na Nicolas Pepe kushindwa kuwabana kwa haraka walinzi wa City kuanzia mbele, lakini kama wangepitwa walikuwa wavivu kurudi katikati kuongeza idadi. Hivi ndivyo mpira ulivyobadilika.

Lakini wakati mwingine unawaza namna ambavyo akina Pep wamebadili tena mpira. Kuna uhamisho wa haraka sana wa mpira kutoka nyuma kwenda mbele. Uhamisho huu sio wa mchezaji mmoja. Inatakiwa uhamishe mpira kwa haraka kwenda kwa mtu aliye mbele yako kujaribu kufika lango la adui kwa haraka.

Ndani ya uhamisho huu wa haraka hautakiwi kuwa na mbwembwe nyingi. Unatakiwa kuwa na jicho la haraka la kupeleka mpira mbele kwa mwenzako. Hapa ndipo ambapo akina Jay Jay Okocha wangekwama. Okocha angetaka kanzu na mbwembwe nyingi ambazo zingechelewesha uhamisho wa mpira.

Ronaldinho kama kawaida yake, angetaka kumvisha mchezaji mmoja kanzu, kisha akamrudia tena, halafu akamrudia tena. Siku hizi haukuti aina hiyo ya uchezaji. Makocha wanataka uhamisho wa mpira kwa haraka zaidi.

Wakati mwingine hata kama hakuna uhamisho wa mpira kwa haraka lakini makocha wanataka mpira utembee zaidi kwa ajili ya kuvuruga akili za wapinzani. Hakuna muda wa mchezaji mmoja kufanya mbwembwe nyingi kama zamani. Sio kwamba hatuna wachezaji wa kufanya hivyo, lakini makocha wanazuia wasifanye hivyo.

Kila siku mchezo wa soka umekuwa wa kasi zaidi. Ukichukua mkanda na kutazama mpira wa miaka ya nyuma utagundua kwamba kwa sasa mpira upo kasi zaidi. Sababu ni hii ya namna ambavyo akina Pep wanataka mpira uwe.

Wachezaji wamekuwa wakikimbia kilomita nyingi zaidi kuliko awali. Ungetazama mikanda ya kombe la dunia miaka ya nyuma ambayo ilikuwa inaonyeshwa na Supersport kabla ya kuanza kwa kombe la dunia pale Qatar utagundua kwamba mpira ulikuwa unakwenda taratibu.

Lakini hata sasa ukitazama pambano lolote kali la La Liga mwaka 2004 ni tofauti na sasa. Mpira unakwenda kasi na hawa akina Pep Guardiola wanaupeleka kasi zaidi. haishangazi kuona mtu kama yeye anakuwa na wachezaji wengi ambao ubora wao unakaribiana. Hii ni kwa sababu ya kuhakikisha hawachoki mapema.

Rafiki yangu Klopp yeye wachezaji wake wamechoka. Alikuwa anawachezesha wale wale kila siku. Leo Mohamed Salah, Trent Alexander Arnold, Andy Robertson wote wapo hoi. Nadhani hata Sadio Mane huko alipo yuko hoi.

Bado natafakari kama Zidane na Gaucho wangeweza kutuonyesha kilekile walichotuonyesha zama zile katika dunia ya leo. Nadhani vipaji vyao vingedhibitiwa zaidi kutokana na namna ambavyo kina Pep wanataka timu zao zicheze.

Columnist: Mwanaspoti