Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NyotaNjema: Vijana wanaotimiza ndoto kusaidia kaya masikini

NOTA.webp NyotaNjema: Vijana wanaotimiza ndoto kusaidia kaya masikini

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

VIJANA ni moja ya kundi kubwa katika jamii ambao wana uwezo mkubwa wa ushawishi katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimabli na kuleta matokeo chanya.

Hii inatokana na nguvu walizonazo katika kutumia elimu, vipaji na utendaji wao kazi. Wapo walioongoza kwenye mabadiliko ya kisera, kiuchumi na kisiasa na kufanikiwa kuiweka jamii pamoja na katika mshikamano wa hali ya juu.

Jumuiya ya vijana na Nyota Njema, ni sehemu ya vijana ambao wameamua kutumia uwezo wao wa kifikra, kiuchumi na kielimu, kuhakikisha watu wanabadilisha mtazamo na kuona wana wajibu wa kuwapa matumaini watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Kupitia miradi yao tofauti, vijana hao wamewanufaisha watoto kutoka kaya zaidi ya 80, kuwa na uhakika wa chakula, elimu kwa watoto na huduma ya bima ya afya.

Miradi mingine wanayoitekeleza ni utunzaji wa mazingira, usaidizi kwa wagonjwa hospitali, kuwarudisha shuleni watoto wanaoishi mazingira magumu.

Akizungumza na gazeti hili, Mweka Hazina wa jumuiya hiyo, Hemed Lumeme, anasema Nyota Njema ilianzishwa kutokana na mawazo ya vijana hao, ambao walikuwa na ndoto ya kuona jamii inaishi katika usawa kwa wale wenye fedha na wasio nacho.

Anasema katika kutimiza ndoto yao, wanatumia rasilimali zao na kuomba ufadhili katika taasisi zingine ili kupata fedha kwa ajili ya kugharamikia miradi hiyo.

Katika muda wa miaka minne, wameanza kupata mafanikio baada ya kuwafikia watu wengi ambao kimsingi wanahitaji kuongezewa nguvu kuendesha maisha yao.

“Tulikuwa na ndoto ya kuona jamii inaishi pamoja kwa furaha bila kuwapo na mipaka ya matajiri na maskini, sasa tumenza kuona mafanikio baada ya kuwarudishia matumaini na furaha kwa idadi ndogo ya jamii tulizozifikia,” anasema Lumeme.

Anasema katika mradi wa ugawaji wa chakula kwa kaya zinazoishi katika mazingira magumu, mwaka huu pekee zimetumika zaidi ya milioni sita ambazo zimewanufaisha familia 49 ndani ya jiji la Dar es Salaam.

“Tunatembea kila nyumba ambayo ina walengwa kuwapa kile tulicho nacho, nafurahi kuona kwa mwaka huu tumekwenda mbali zaidi baada ya mwaka uliopita tuliwafikia kaya 30 pekee,” anaongeza kusema.

Ofisa Rasilimali Watu wa Jumuiya hiyo, Said Zahran, anaeleza kwamba pamoja na mradi huo wa ugawaji chakula, pia wamefanikiwa kuwarudisha shule watoto 50 ambao walishindwa kuendelea na masomo kwa kukosa pesa.

Anasema katika mradi huo unaojulikana kama ‘Rudi Shuleni’ wanajitolea kuwahudumia watoto walioshindwa kuhudhuria shuleni kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo.

Zahran anaeleza kuwa katika mpango huo, watoto ambao wamekatisha masomo kutokana na sababu za kiuchumi wanapatiwa msaada wa madaftari, vitabu vya kiada na ziada pamoja na sare za shule.

“Tumegundua watoto hawa wana nia ya kusoma, lakini kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kiuchumi wanashindwa kutimiza ndoto zao. Tangu tuanze mpango huu tumewarudisha shule na kuwapatia furaha waliyoikosa,” anaongeza kusema.

Mmoja wa walionufaika na mradi huo, Kulthum Said, anasema haikuwa rahisi kwake kurudi shuleni kutokana na kukosa madaftari na sare, lakini Nyota Njema ilimsaidia mpaka sasa hivi anaendelea na masomo yake.

“Naishukuru Nyota Njema kwa kunisaidia kurudi shuleni, wazazi wangu waliniambia hawana uwezo wa kumudu kununua sare na madaftari nikabaki nyumbani kwa muda wa mwaka mmoja, lakini sasa naendelea na masomo yangu,” anasema Kulthum.

Akizungumzia mradi wa mazingira, kiongozi huyo anasema kwamba kupitia ‘mradi wa kijani’ wanasaidia kuboresha mazingira kama upandaji wa miti, kusafisha maeneo mbalimbali ya wazi na utengenezaji wa bustani ya kupumzikia watu.

Anasema kwa kuanzia, wameomba kuboresha bustani ya Temeke Hospitali ili iwe na mvuto wa kipekee, hatua ambayo inaendelea kufanyika kwa kushirikisha Halmashauri husika.

Naye meneja mradi, Ibrahim Ally, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa kundi hilo, anasema waliangalia pia umuhimu wa watoto yatima kuwa na bima ya afya ili kuwarahisishia huduma za matibabu.

“Unajua idadi kubwa ya watoto yatima hawana uhakika wa kupata huduma za matibabu, mwaka jana tuliamua kuwakatia bima watoto 30 kwa kuanzia, mwaka huu tumepanga kuongeza idadi hiyo kama tukipata watu wa kutuunga mkono,” anasisitiza.

Anasema wao kama vijana walioamua kujitolea, hawana fedha za kutosha, wanachokifanya ni kujichangisha kidogo walichonacho na kisha kutafuta ufadhili kwa watu na taasisi watakaoguswa na wazo lao.

“Ukweli hatuna fedha za kukamilisha miradi yetu yote, tunawashukuru baadhi ya taasisi na watu wanaotuunga mkono katika hiki tunachokifanya. Tunaomba watu watakaoguswa kutuunga mkono ili tuwafikie watu wengi ambao wanahitaji kurudisha matumaini,” anasema Ally.

Columnist: www.tanzaniaweb.live