Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nkane anatabasamu, anacheka, haoni tatizo la msingi

Denis Nkane Vvip Nkane anatabasamu, anacheka, haoni tatizo la msingi

Mon, 2 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Dennis Nkane anatabasamu na anacheka. Haoni tatizo la msingi linalomkabili. Huwa napenda kutazama picha zake wakati Yanga ikiwa kambini, au safarini. Anafurahia maisha ya Yanga vilivyo. Yanga wana maisha mazuri kwa sasa. Ndani na nje ya uwanja.

Wakati fulani Nkane alitajwa kuwa ‘Mrisho Ngassa mpya’ katika mpira wetu. Alionekana kama vile angeweza kufuata nyayo za Uncle Ngassa. Kwa kinachoendelea kwa sasa hakuna dalili kama anaweza kuwa Ngassa mpya katika mpira wetu. Ni hadithi ile ile ya kumfananisha Geofrey Mwashiuya na Edibily Jonas Lunyamila.

Ngassa alikuwa anatabasamu, lakini alikuwa ana njaa moyoni mwake. Baadaye akalishika taifa. Akawa tegemeo la Yanga na timu ya taifa. Nkane ameridhika kabla hajawa Ngassa. Hatuioni hasira yake ndani ya uwanja wala nje ya uwanja. Bahati mbaya anacheza Yanga ambayo imejaza mastaa kuliko ile ya Ngassa.

Ana msimu wa tatu pale Yanga, lakini hachezi. Hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza na hana nafasi ya kudumu hata katika wachezaji wanaokaa benchi. Achilia mbali kutoanza katika mechi, lakini Yanga inaweza kufanya mabadiliko ya wachezaji wa nne uwanjani na usitarajie kama Nkane ataingia.

Nini kinatokea? Nkane anawakilisha tu tabia za wachezaji wetu wazawa. Hawana presha na maisha kama Watanzania wengi tulivyo. Nimeambiwa tu kwamba Nkane alikataa kuondoka kwa mkopo mwishoni mwa msimu wa uliopita. Anafurahia kuwa katika kundi kubwa la wachezaji wa Yanga. Wachezaji ambao kokote wanakokwenda wanapokewa kwa shangwe na mashabiki.

Ana kasi ana kipaji. Mchezaji mwingine wa Afrika Magharibi angetaka kulazimisha kucheza. Iwe ndani ya Yanga au nje ya Yanga. Angelazimisha kuchanwa kwa mkataba wake au kwenda kwa mkopo kwingineko ili mradi acheze. Katika umri wake wa miaka 20 kuna mambo mawili yangeweza kutokea kwa urahisi tu.

Kwanza angeweza kupambana kwingineko na kurudi katika timu kubwa za hapa hapa nchini. Angeweza kuangukia mtaa wa Msimbazi au angeweza kuangukia kule Mbande Chamazi. Hata hivyo, ameamua kuendelea kuwa tu mmoja kati ya wachezaji wa Yanga ambao hawachezi. Nadhani anapenda tu kuhesabiwa kuwa mchezaji wa Yanga hii yenye furaha ndani na nje ya uwanja.

Lakini katika umri wake Nkane angeweza pia kuwa na hasira za kuwafuata kina Simon Msuva wanaotangatanga nje ya nchi. Kasi yake, uwezo wake na mengineyo katika mchezo wake yangeweza kumfanya aibukie kwingineko katika Ligi Kuu kisha akafanya vizuri katika timu ya taifa na kisha kuonekana kwingineko.

Tatizo letu kubwa kwa wachezaji wetu ni kuwekeza mawazo yao katika soka la ndani. Ukiweka mawazo yako katika soka la nje unaweza kuona namna ambavyo muda unapotea. Wale rafiki zetu wa Afrika Magharibi wanalazimika kudanganya miaka mingi katika hati zao za kusafiria kwa sababu ya kufidia muda.

Hata hivyo, sisi tuna kijana mwenye kipaji mwenye miaka 20 ambaye anafurahia kukaa jukwaani achilia mbali kukaa benchi. Sidhani kama ana mawazo haya mawili. Sidhani kama ana njaa ya kufufua kipaji kwa ajili ya kuzikomoa akaunti za timu zetu kubwa baadaye. Kuna wazawa waliwahi kufanya hivi. Hassan Dilunga na Amri Kiemba waliwahi kupotea katika timu kubwa wakaangukia timu za mitaa ya kati halafu wakarudi tena timu kubwa kwa heshima.

Yanga na Simba huwa zinakupa heshima ya kuwa katika kikosi kwa muda fulani. Kama hauna akili unaweza kujiona umefika katika ufalme wa milele, lakini baada ya muda mfupi ukapotea kabisa. Wachezaji wenye akili huwa wanazitumia hizi timu kujitengenezea ufalme wao na sio kuwa sehemu ya kikosi tu.

Nkane anawakilisha tabia za wachezaji wetu wazawa. Namjua mchezaji mmoja wa Yanga ambaye amekataa kiasi cha Sh180 milioni kwenda katika timu nyingine ya Ligi Kuu na badala yake akasaini mpya klabuni kwa kiasi kidogo cha pesa. Ili mradi tu awe sehemu ya kikosi cha Yanga. Sawa timu ndogo zina matatizo yake, lakini kwa wenzetu wale wa Afrika Magharibi huwa wanaitumia timu yoyote ile kwa ajili ya kupanda kwenda juu katika maisha ya soka.

Siioni njaa ya Nkane. Sioni hasira katika uso wake. Sidhani hata kama anakwenda kumhoji kocha kwanini hachezi. Ndani ya makala hii hii kuna watu watamtetea Nkane kwamba bado ni kijana mdogo. Sio kweli. Ana miaka 20. Kuna mastaa wengi ambao tayari walikuwa wametengeneza maisha wakiwa na miaka 20. Asije akajidanganya kuhusu suala la umri.

Pele alitamba Kombe la Dunia mwaka 1958 pale Sweden akiwa na miaka 17 tu. Wayne Rooney alitangaza jina duniani na kuwa staa wa kudumu Everton akiwa na umri wa miaka 16 tu. Cesc Fabregas alishaanza kutegemewa Arsenal akiwa na miaka 18 tu. Miaka 20 ni umri ambao mchezaji anakomaa kisoka na sio kufurahia kupiga picha ukiwa katika bwawa la kuogelea na wachezaji ambao tayari wanaifanyia timu mambo makubwa. Au kufurahia kudansi na kugeuka ‘Joti’ kwa wenzako, wakati wewe kazi yako ni kucheza soka.

Mpira ni maisha. Muda ni maisha pia. Muda haumsubiri mwanadamu. Walio karibu na Nkane wanaweza kumshauri akafufue maisha yake ya soka kwingine na sio kufurahia kuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wa Yanga. Wenzake wanacheza wanafurahia mafanikio uwanjani, lakini wanafanikiwa pia kuiweka klabu wakati mgumu katika mazungumzo ya mkataba mpya. Nkane hana nafasi hiyo.

Kuna mahali kuna matatizo kwa vijana wetu. Sawa klabu za mitaa ya kati huwa zina matatizo fulani. Usafiri wa shida. Hawafikii kwenye hoteli zenye hadhi ya Simba, Yanga na Azam. Hazina mishahara mikubwa. Sawa, lakini mchezaji ukiwa na malengo unakwenda katika klabu hizi kwa ajili ya kutangaza njaa. Kina Duke Abuya ndio walikwenda katika timu hizi kutangaza njaa.

Nkane angepunguza kutabasamu kidogo. Kuna kitu kinapaswa kumuuma moyoni. Kitu hiki ndicho ambacho kinatutofautisha sisi na wale jamaa wa Afrika Magharibi. Sio kwamba wana vipaji vikubwa sana hapana. Kuna vitu huwa vinawauma moyoni. Kuna njaa fulani ambayo wanayo halafu sisi hatuna.

Anatokea mchezaji kama Nkane kutoka kule Afrika Magharibi anakuja na njaa zake hapa Tanzania anapambana vilivyo kuonyesha ubora wake mwishoni tunaongea ule ujinga wa kutaka kuwapa uraia ili wachezee Taifa Stars. Haikubaliki. Vipaji kama hivi vipo nchini, lakini baba yake Haji Manara, Sunday Manara aliwahi kuniambia tofauti ya sisi na wao.

Mzee Manara aliwahi kuniambia kwamba tofauti yao na wachezaji wa sasa ni kwamba wachezaji wa sasa wanacheza kwa asilimia 20 tu ya uwezo wao. Hawana njaa. Hawajitumi. Hawataki kuonyesha tofauti. Wanaridhika mapema. Ni kama ambavyo Nkane anatabasamu. Anacheka. Benchini na jukwaa ni vitu vya kawaida kwake ingawa kipaji kipo mfukoni.

Columnist: Mwanaspoti