Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nimemfikiria Bruno Gomes mara mbili

Bruno Gomes Barosso Bruno Gomes

Thu, 11 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Yanga kuwafunga Singida Big Stars katika mchezo wa Ligi Kuu katikati ya wiki iliyopita, Yanga walikuwa na sababu mbili au tatu za kufurahi. Kwanza walikuwa wamepata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Singida ambao walihesabika kama moja kati ya wapinzani wa wagumu kwa Yanga.

Kama walifanikiwa kushinda dhidi ya Singida walioaminika ni wapinzani wagumu ina maana waliusogelea kwa karibu zaidi ubingwa wa ligi ambao unaonekana kuwataka Yanga.

Sababu ya tatu ni kile kilichotokea kabla na baada ya mchezo. Kabla ya mchezo kuanza kiungo Mbrazili Bruno Gomes alienda katika benchi la Yanga kusalimiana na wachezaji wa akiba wa Yanga pamoja na benchi la ufundi la Yanga.

Baada ya mchezo kumalizika Gomes alibaki uwanjani kwa dakika nyingi na kuzungumza na Kocha wa Yanga, Nasredinne Nabi. Kilichowafurahisha Yanga? Wameamini matendo aliyoyafanya Gomes ni ishara anatamani kujiunga na Yanga. Wataalam wa tetesi wanadai tayari Yanga wapo katika meza ya mazungumzo na Gomes na inawezekana msimu ujao ataonekana katika uzi wa kijani na manjano.

Sifahamu hizi tetesi zina ukweli kiasi gani lakini vyovyote vile itakavokuwa lazima Gomes ajiunge na timu kubwa zaidi ya Singida Big Stars. Inawezekana isiwe lazima lakini kwa kiwango alichokionyesha Gomes ni wazi wakubwa watapigana vikumbo kuinasa saini yake. Simba, Yanga na Azam wanammezea mate Gomes.

Yanga wanaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi kwa kile alichokionyesha katika mechi yao dhidi ya Singida Big Stars. Pia taarifa kutoka mtaani zinadai Singida wana urafiki mzuri na Yanga. Hiyo ni kuanzia kwa viongozi wa Singida na Yanga. Hivyo dili la Bruno linaweza kufanyika kirahisi zaidi.

Ni kama ambavyo Singida walikubali kumuachia kipa wao namba moja, Metacha Mnata kujiunga na Yanga kwa mkopo halafu wao wakabaki hawana kipa namba moja imara ni urafiki tu ulifanyika. Lakini usifikiri Gomes anaipenda Yanga wala Singida. Alitoka kwao Brazil akiwa si shabiki wa timu yoyote ile nchini alikuja kutafuta hela, hivyo kujiunga na Yanga au kuendelea kubaki Singida kutategemeana na pesa atakayowekewa mezani. Usifikiri alikuja nchini akiwa shabiki wa klabu yoyote ile.

Hata hivyo, hapo ifikirie nafasi ya Gomes katika timu ya Yanga, atacheza wapi? Yanga wana safu bora zaidi ya kiungo katika ligi, Gomes anakwenda kufanya nini? Yanga wanaweza kuanza mechi na kuwapanga Khalid Aucho, Zawadi Mauya na Salum Abubakar katika kiungo kisha mechi inayofuata katika kiungo wakaamua kuwapanga Yanick Bangala, Mudathir Yahya na Stephane Aziz Ki.

Huu ndio utajiri walionao Yanga katika safu ya kiungo hapo hatujamhesabu Fei Toto ambaye amekataa kurejea kundini Gomes anakwenda kuongeza nini zaidi Yanga? Kama Yanga wataamua kumsajili watakuwa wamefanya hivyo kwa ajili ya vurugu tu na kumzuia Gomes kwenda Simba lakini ukweli, Yanga hawamhitaji Gomes.

Kwa mtazamo wangu Yanga wanahitaji zaidi washambuliaji wa pembeni (mawinga), kuliko viungo. Kwa sababu Bruno ni mchezaji wa kigeni, Yanga hawapaswi kupoteza nafasi ya mchezaji wa kigeni kumwongeza mchezaji katika eneo ambalo tayari wapo imara.

Watunze hiyo nafasi kwa ajili ya kutibu eneo ambalo tayari wana matatizo. Lakini hapo kuna nafasi ya Gomes kujiunga na Simba. Kama si Yanga, wapi kwingine tofauti na Simba? Nafikiri Simba wanamjitaji Gomes zaidi ya Yanga. Simba hawana utajiri waliopo nao Yanga katika safu ya kiungo.

Ninaposema Simba wanamhitaji zaidi ninamaanisha wanamhitaji zaidi uwanjani akiichezea Simba, pia wanamhitaji zaidi asijiunge na Yanga kuliko ambavyo Yanga wanamhitaji asijiunge na Simba. Kama tayari Yanga wana safu bora zaidi ya kiungo nchini vipi akiongezeka Bruno ambaye ni moja ya viungo bora nchini? Ina maana Yanga watakwenda juu zaidi.

Hapo Simba watazidi kuachwa mbali na Yanga. Lakini Gomes akijiunga na Simba ataiimarisha Simba lakini Simba hawataenda juu zaidi ya Yanga. Simba wanapaswa kufanya kila wawezalo kumsajili Gomes. Wasifanye kosa kama walilolifanya la kumuacha Mudathir Yahya ajiunge Yanga halafu wao wakamsajili Ismail Sawadogo.

Columnist: Mwanaspoti