Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nilichokiona Taifa baada ya miaka 26

Mashabiki Miaka 26.jpeg Mashabiki waVilabu vikongwe vya Simba na Yanga

Sun, 21 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nilikuwa Dar es Salaam kwa siku kadhaa mwezi huu. Nimefaidika sana kuziona timu kongwe Afrika Mashariki za Simba na Yanga kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 26 ambayo ndio mara yangu ya mwisho kuwa Tanzania na kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa( zamani Uwanja Taifa).

Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuyaona matamasha ya Simba na Yanga ya kujiandaa na msimu mpya wakitambulisha wachezaji wapya na kucheza mechi za kirafiki za kimataifa.

Nimependa jinsi mashabiki wa timu hizi wanavyokuwa na hamu ya kuona wachezaji wao wapya wa kujaza Uwanja wa Mkapa.

Nimependa jinsi mashabiki wanavyoshindana au kupigania kununua Jezi mpya na za msimu uliopita zinabaki kuwa kumbukumbu tu, kama tuonavyo kwa mashabiki wa Ulaya.

Nilishangaa sana kuona foleni ndefu ya mashabiki wa Simba wenye kiu kubwa ya kununua jezi mpya kwenye duka moja pale Sinza.

Nimefurahi kuwaona mashabiki wengi wakienda uwanjani wakiwa familia yaani baba, mama na watoto wao wote ili kuwandaa watoto wakiwa bado wadogo kushabikia timu zao pendwa na vilevile kupata burudani kama sehemu ya maisha. Zamani hii haikuwepo. Ilikuwa inaonekana kama sehemu ya vurugu huwezi kwenda na familia. Ni maendeleo haya.

Kwa Mkapa pia panakuwa kama sehemu ya kutoka au kutembelea ili macho yaone mengi tofauti na yale wayaonayo nyumbani, kazini hata shuleni. Ni jambo ambalo limenifurahisha miaka 26 iliyopita halikuwepo.

Nimeshangaa jinsi biashara za kuuza vyakula na vinywaji zinavyofanyika nje ya Uwanja wa Mkapa! Nimegundua mashabiki wanapenda kwenda uwanjani bila kula chakula nyumbani ili wale chakula nje ya uwanjani kabla ya kuingia ndani kushuhudia mechi.

Unaweza ukanishangaa kidogo katika hilo. Mimi ni Raia wa Rwanda. Nchini kwetu huo utamaduni haupo. Hairuhusiwi kuuza vyakula na vinywaji barabarani kiholela kwa sababu inaweza kusababisha magonjwa. Rwanda ni nchi yenye usafi kama Singapore.

Rwanda vyakula na vinywaji vinauzwa ndani ya migahawa na baa mbele ya uwanja mkubwa kama Amahoro. Huwezi kukuta mtu kajibana pembeni ya ukuta na ndoo au beseni lake anauza pilau kama nilivyoona kwenye mitaa ya pale Kwa Mkapa.

Baada ya Rwanda kufanyia marekebisho Uwanja wa Amahoro kwa kuupanua zaidi na kuuezeka wote kutawekwa utaratibu wa kuuza vyakula na vinywaji ndani ya uwanja kama Ulaya. Hayo ni maendeleo ndio maana nikashtuka nilivyoona kinachoendelea pale Temeke.

Pia, Rwanda hakuna kuuza vitu barabarani au watembazaji wa nguo, viatu, mashuka mkononi maarufu wa Wamachinga serikali ilijenga masoko mengi madogo madogo mjini Kigali, kuanzia ya kuuza mboga na matunda pia wote serikali iliwapa mitaji kuanzia, ndio maana Mnyarwanda yeyote akifika Dar es Salaam atashangaa kama mimi.

MIAKA 26 TAIFA

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 niliishi Tanzania kama mkimbizi ndio maana kiswahili changu kidogo kimenyooka kwa kuongea na kuandika. Niliishi maeneo ya Karagwe kwa miaka kadhaa.

Imekuwa kama miaka 26 bila kuona dabi ya Kariakoo. Mwezi huu nimeiona rasmi na kushuhudia mbwembwe nyingi za nje ya uwanja ambazo hata Kigali na sehemu nyingine duniani ambako watani wapo hazikosekani.

Nilishangaa kuona Yanga wakiingilia mlango ambao si wa kawaida kutokana na sababu wanazojua wenyewe. Nilipouliza nikaambiwa ni kawaida kwa timu hizi hata Simba wanafanyaga hivyo.

Nikajiuliza hizi timu kongwe ni kipi timu changa kama Vipers ya Uganda, AS Kigali ya Rwanda, Bumamuru ya Burundi zinaweza kujifunza? Kama bado wanaamini vitu dhaifu kama hivyo?

Nilishangaa kuona mashabiki wa Simba ni wengi kuliko wa Yanga, wakati Yanga ndio walishinda sana dhidi ya Simba msimu uliopita.

Baada ya kuona vikosi nilishangaa kutomuona Dejan Georgijeviv wa Serbia kwenye kikosi cha Simba kwa sababu niliamini ana uwezo kuliko Meddie Kagere na Chris Mugalu waliotemwa. Jamaa mmoja akaniambia eti bado hajazoea mazingira. Hata kwa Mkapa? Nikakausha.

Nikashangaa kumkosa Victor Akpan kwa sababu uwezo wa Sadio Kanoute nilidhani ni wa kawaida, lakini upande wa Simba kocha alijitahidi kuweka nyota wake wengi. Nikasema ngoja mpira uanze labda nitajifunza.

Lakini nilishangaa zaidi kwa upande wa Yanga baada ya kuwakosa nyota wao Bakar Nondo, Joyce Lomalisa, Gael Bigirimana na Bernard Morrison. Nikaamini sasa Simba inakwenda kushinda.

Niliamini Kibwana Shomary, Dickson Job, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Farid Mussa wasingeweza kupambana na majina makubwa ya Simba ambayo jana yake niliona wakiwa wamekaa kambini na tajiri.

Baada ya Simba kupata bao la kuongoza kipindi cha kwanza sikuweza sana kutofautisha alichofanya Fiston Mayele wa Yanga na Habib Kyombo wa Simba. Ndio pale nikawa bado na hamu ya kumuona Dejan aliyesabisha watu kama Mugalu na Kagere watimuliwe.

Kipindi cha pili Yanga ilibadilika sana ikawa tishio mbele ya lango la Simba baya zaidi beki tegemeo wa Simba, Henock Inonga alikuwa akicheza rafu mbaya za kujitakia kupewa kadi nyekundu, lakini Mwamuzi Eli Sasii aligundua hilo akakwepa mtego huo kwa sababu ya lawama za Simba zingebaki kwake.

Kocha Zoran Maki kipindi cha pili akakosa mbinu mbadala. Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze walikuwa makini hasa kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji Stephane Aziz Ki akihamishwa kutoka pembeni kwenda kati na Feisal Salum kutoka namba 10 kwenda namba 8 ilikuwa tabu sana kwa Simba kwani wangeweza hata kufungwa mabao matano kipindi cha pili.

Ni uzoefu uliwabeba, lakini niliamini maneno ya shabiki mmoja hizo timu hata kama hazina muunganiko bado mechi ya watani huwa ngumu.

Baada ya Mayele kutetetema mara mbili nilihofia na nikaona Simba ni timu ya kawaida inahitaji kufanya mabadiliko kadhaa na kujipanga kiakili, kwani kwa aina ile ya uchezaji kwenye mashindano ya CAF hali itakuwa ngumu.

Nimegundua Simba ina wachezaji muhimu watatu tu ambao ni Aishi Manula, Clatous Chama na Sakho. Hawa wengine bado hawakunifurahisha. Nikajiuliza kuna umuhimu gani kwenda kuweka kambi Misri bila kuwa na wachezaji bora?

Yanga hata ikiweka kambi Tandahimba, Mtwara au Ngara, Kagera ni karibu ya nchi za Rwanda na Burundi. Ni vizuri kuwapeleka wachezaji wetu nje kujifunza kupitia hizo kambi lakini klabu lazima pia ifanye tathmini ya faida na hasara.

Sijazielewa mbinu za Kocha Zoran, lakini ngoja tuone. Nadhani kwa heshima ya Simba Afrika ni wakati wa Mohamed ‘Mo’ Dewji na Babra Gonzalez kufikiria mara mbili ndani na nje ya uwanja. Inawezekana hiki kinachoendelea Simba ni matokeo ya kutokuwa na muingiliano mzuri wa kimbinu kati ya Selemani Matola na Zoran.

Hata kama viongozi wanataka kuendeleza wazawa, wampe Matola majukumu mengine. Zipo timu za vijana ambazo pia ni muhimu na uzoefu wake unafaa huko. Nani hakumbuki alivyowatengeneza kina Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo.

Simba ina mengi ya kubadilika kutokana na hadhi yao Afrika. Nilichokiona kwenye hizi mechi kimenifurahisha Tanzania ina mashabiki vichaa wa mpira. Watu wanapenda sana. Ni jukumu la sasa kuwapa kile wanachotamani.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz