Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ni kweli tumeamua kuwaiga Nigeria na Ghana?

Kikosi Cha Timu Ya Tifa Ya Vijana Kikosi Cha Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23

Thu, 5 Aug 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Nigeria na Ghana wamekuwa wataalamu sana wa kupunguza umri wa wachezaji wao. Wamekuwa mashughuli sana kwenye kushinda mataji ya vijana. Kwenye michuano ya U-20 Afrika, Nigeria ndiyo mabingwa mara nyingi.

Wana mataji saba kibindoni. Kwenye michuano hiyo, Ghana ndiyo bingwa mtetezi na tayari ana mataji manne. Nguvu ya Nigeria na Ghana kwenye michuano ya vijana ni kubwa sana, lakini kwenye timu zao za wakubwa ni sarakasi tupu. Mchezo wa mpira wa miguu hauna njia ya mkato. Unahitaji mipango ya muda mrefu, unahitaji uwekezaji wa hali ya juu, unahitaji mwendelezo wa vijana.

Majuzi timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 23 ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Cecafa nchini Ethiopia, ni habari njema kwetu. Lakini mara tu baada ya kikosi kutangazwa, watu waliibua mjadala kama Wanigeria. Baada tu ya majina ya wachezaji kuonekana, sura za wachezaji wakubwa kwenye timu ziliibua mjadala kama Waghana! Kwenye nchi za Afrika ni vigumu kumpata mchezaji mahiri chini ya miaka 23 akiwa nĂ¡ misimu mitatu ligi Kuu. Wachezaji wengi wanaanza kuchanganya kuanzia miaka 25 na kuendelea.

Ukitazama kikosi kilichoitwa na Kocha Kim Poulsen kilisheheni majina makubwa ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara. Ni kweli kanuni inaruhusu walau kuwe na watatu wanaozidi miaka 23, lakini ukitazama vizuri tulikuwa na wengi wenye umri kama wa wachezaji wa Nigeria na Ghana.

Wachezaji wakubwa kwenye timu za vijana. Tunaweza tukafurahia Kombe la Vijana, lakini hapo baadaye hatutaona mwendelezo wa vijana hao. Uzuri wa umri kwenye mpira haudanganyi. Unadhani ni kweli tulipeleka vijana chini ya miaka 23 kule Ethiopia kwenye Cecafa? Naomba maoni yako Kwa ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kudanganya umri kwenye soka kutawapa taji la vijana tu. Huwezi kwenda zaidi ya hapo ndiyo maana mpaka leo Ghana na Nigeria hawajawahi hata siku moja kuwa na makeke kwenye Kombe la Dunia. Hata robo fainali ya Kombe la Dunia walilofika Ghana 2010 haikutokana na timu zao za vijana, bali ni uwepo wa wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya Bara la Afrika.

Waafrika wengi sio wakweli hasa linapokuja suala la umri. Mifumo yetu ya maisha inatuchelewesha sana kutoboa. Wachezaji wengi wanatoboa umri ukiwa umeshaenda sana. Ndiyo maana ni vigumu kumpata mchezaji ambaye ni U-23 lakini kacheza Ligi Kuu kwa misimu mitatu au minne. Nimeona majina mengi ya wachezaji ambao wamecheza ligi Kuu Bara, lakini naambiwa ni U-23! Naanza kupata wasiwasi kama wa wachezaji wa Nigeria. Napata wasiwasi kuona tabia ya Ghana ni kama tumeanza kuitekeleza Tanzania.

Hakuna asiyependa ushindi kwa Taifa lake. Hakuna asiyeitakia mema timu yake ya Taifa, lakini nina wasiwasi kidogo na aina ya wachezaji waliokwenda kutuleta Kombe la Vijana. Duniani kote, U-23 ndiyo wachezaji ambao huenda kutengeneza timu ya Taifa ya wakubwa. Ni kundi la wachezaji ambao wamepikwa na wakapikika. Ni watu ambao wamekuwa pamoja timu za U-17 na U-20 muda mrefu. Wanajuana, wamezoeana.

Ukiona kuna mchezaji amecheza Ligi Kuu misimu mitatu au minne wa Kitanzania na bado ni U-23 unapata wasiwasi kidogo. Labda awe anatoka Afrika Kusini, labda awe anatoka Misri. Wenzetu wameendelea sana kwenye soka la vijana Afrika. Wametengeneza mazingira mazuri kwenye soka la vijana.

Waswahili wana msemo wao, kawia ufike! Kila mtu anataka ubingwa lakini usije kwa mbinu za watu kama Nigeria. Tunataka vijana washinde mataji lakini sio kwa mbinu kama wanazotumia wenzetu wa Ghana.

Msingi mkubwa wa soka la vijana ni maandalizi ya baadaye. Sio lazima washinde makombe. Hawana presha yoyote. Ni wakati wa kuandaliwa ili kuja kuliletea faida Taifa letu baadaye. Tukianza mbinu za Nigeria na Ghana hatutafika mbali. Tutaishia kushinda mataji ya vijana.

Tumekuwa tukifuzu kwenye michuano mbalimbali na mikubwa siku za hivi karibuni. Ni jambo jema. Ni jambo la kupongeza. Tunahitaji kwenda kushindana kwenye michuano tunayofuzu. Tunahitaji kwenda kushindania makombe. Hatuwezi kushinda chochote kama mbinu zetu za soka la vijana ni zile za Nigeria na Ghana. Wenzetu walau Afrika wanafanya vizuri kwa sababu wachezaji wao tegemeo wako Ulaya. Sisi wachezaji wetu tegemeo wako hapahapa. Ni lazima tuwe wakweli. Kikosi chetu cha U-23 kilikuwa na mashaka kidogo kwa baadhi ya wachezaji. Tunahitaji kweli mataji, lakini sio kwa mbinu za Nigeria na Ghana.

Kim Poulsen anapaswa kututengenezea wachezaji wa baadaye. Kazi yake kubwa ingekuwa kutuandalia wachezaji warithi wa kina Mbwana Samatta, Saimon Msuva. Poulsen alipaswa kuja kutuletea kina Kelvin Yondani wa baadaye. Kombe sio jambo baya lakini kwenye soka la vijana tusiwe na haraka sana. Bado kuna changamoto kubwa na hasa kutengeneza muunganiko wa timu za U-17, U-20, U-23 na Taifa Stars.

Katika hali ya kawaida, timu za vijana ndizo zinatakiwa kuijenga timu ya Taifa. Tusitumie nguvu kubwa kuwaleta wachezaji wa Taifa Stars kwenye timu za vijana. Najua wapo wachache ambao wanaweza kuwa na vigezo vya timu zote lakini kwa mazingira yetu, tusijikite huko. Ni kweli tumeamua kuwaiga Nigeria na Ghana? Naomba maoni yako kupitia namba ya simu hapo juu.

Kiukweli Watanzania wana kiu ya kushinda taji, lakini lazima lile lenye tija.Michuano ya vijana ihusishe vijana na michuano ya wakubwa ihusishe wakubwa. Ushindi ni lazima ulete furaha. Ushindi usiwe na chembechembe za udanganyifu. Kama Mtanzania nimefurahia sana ubingwa wa Cecafa wa vijana wetu, lakini nina wasiwasi wa mbinu za Nigeria na Ghana.

Columnist: Mwanaspoti