Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ni kweli Simba ni hasara kwa Mo Dewji?

Mo Hasara Ni kweli Simba ni hasara kwa Mo Dewji?

Mon, 27 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tumesikia mara nyingi. Tumesikia tena hapa majuzi kauli ya bilionea na Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ akilalamika.

MO Dewji amekuwa akisema kila siku akitokea hadharani kuwa Simba ni hasara kubwa kwake. Amekuwa akitoa mabilioni kila mara na hayarudi.

Majuzi amedai kuwa fedha alizotoa kwa miaka yake sita ndani ya Simba zinaweza kufika hata Sh50 bilioni. Hivyo ni hasara kubwa kwake.

Hiki kimekuwa ni kilio cha MO Dewji kila anapozungumza hadharani.

Kuna wakati aliwataka viongozi wa Simba kuja na mipango thabiti ya kupata pesa. Aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Na baada ya miezi michache amekuja na kudai kuwa Simba hii bado ni hasara kwake. Inafikirisha sana.

Fedha hizi ambazo MO Dewji amekuwa akidai anatoa kila mara kama hisani zinatumika katika maeneo gani? Ni swali la msingi.

Kama Simba imekuwa hasara kwake kwanini bado yupo? Ni swali la msingi pia.

Kama kuendesha Yanga pia ni hasara kwanini GSM hawajawahi kulalamika? Unadhani matumizi ya Simba ni makubwa kuliko ya Yanga? Inawezekana, lakini sidhani kama yanapishana sana.

Nilifuatilia taarifa za mapato ya Simba kwa mwaka 2022 wakati wa Mkutano Mkuu mapema mwaka huu. Taarifa ya mtu wa fedha ilionyesha kuwa Simba imeanza kuzalisha faida kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.

Mapato ya Simba kutokana na mikataba ya udhamini, mauzo ya jezi, haki za televisheni, fedha za CAF, mapato ya mlangoni na mauzo ya wachezaji yalifikia zaidi ya Sh12 bilioni kwa mwaka jana.

Matumizi kwa mwaka jana yalikuwa Sh11 bilioni na kidogo. Ilionekana baada ya mapato na matumizi, Simba imezalisha faida ya zaidi ya Sh700 milioni. Vipi hasara inatoka wapi?

Naamini miaka ya mwanzo ya uwekezaji wa MO Dewji ilikuwa ni hasara kweli. Simba haikuwa na vyanzo vya mapato vya kuelekeweka. Ilihitaji zaidi msuli wa MO Dewji kujiendesha.

Lakini ukweli ambao MO Dewji hataki kuusema sasa ni kwamba nyakati zimebadilika. Pato la Simba limekua kwa kasi kubwaa.

Mikataba ya udhamini ya Simba, mauzo ya jezi na haki za televisheni kwa sasa vinaipa Simba zaidi ya Sh7 bilioni kwa mwaka. Ni maendeleo makubwa.

Hapo bado hatujaweka dhamana inayotokana na uwekezaji wa Sh20 bilioni za MO Dewji katika ‘endowment fund’ ambazo kwa mwaka zinazalisha zaidi ya Sh1.5 bilioni.

Hivyo Simba katika vyanzo vyake vya sasa inapata fedha nyingi sana tofauti na zamani. Kusema kuwa ni hasara labda matumizi yamepandishwa sana. Ila fedha inazoingiza Simba kwa sasa zinatosha kujiendesha kwa kiwango cha kati.

Isitoshe wakati MO Dewji akilalamika wakati ana matangazo lukuki katika jezi ya Simba. Yapo ya MO Xtra, MO Sports, MO Foundation na mengineyo. Ni kweli matangazo haya hayamlipi katika biashara zake?

Analipa kiasi gani cha fedha kwa ajili ya matangao haya kwa mwaka? Ni maswali muhimu.

Turudi kwenye hoja ya pili. Kwanini mabosi wa Yanga hawajawahi kutoka hadharani na kulalamika kuwa kuendesha timu ni hasara? Siku zote GSM wamekuwa wakifurahia maisha ya uendeshaji wa Yanga. Kama Simba inakaa kambi ya kisasa, basi Yanga nayo inakaa kambi ya kisasa pale Avic Town, Kigamboni.

Kama Simba inasajili wachezaji mahiri hata Yanga wanafanya vivyo hivyo. Kama ni mishahara mikubwa pia pale Yanga ipo.

Wote wanasafiri kwa ndege, wanakaa hoteli za kisasa na kutoa posho kubwa kwa wachezaji. Kwanini GSM kwa miaka yote mitatu hawajawahi kujitokeza na kusema ni hasara?

Simba ina mikataba mingi ya wadhamini kuliko Yanga. Lakini bado ndio mwekezaji wake anaongoza kulalamika kuwa ni hasara.

Nadhani ifike mahala tuishi kwenye ukweli. Kila biashara ina hasara katika mwanzo wa uwekezaji wake, lakini baada ya muda itaanza kulipa. Naamini Simba imeanza kusogea kwenye faida. Inazalisha fedha sasa.

Nadhani kikubwa ni kuishi katika uhalisia wa hali iliyopo. Kama fedha inatoka, itoke na ionekane iliongeza thamani.

Wakati fulani pale Yanga alikuwepo Yusuf Manji. Alikuwa akitoa pesa kuendesha klabu karibu kwenye kila kitu. Yanga haikuwa na mapato ya kueleweka, lakini Manji alikuwa akitoa kila kitu.

Hivyo nadhani ni wakati wa MO Dewji kufikiria zaidi faida anazopata kwa kuwepo Simba kuliko hasara anayozungumza kila mara anapopata nafasi ya kuzungumzia uwepo wake Simba.

Biashara kubwa kwa sasa ni hii ya jezi. Tumeona mkataba mpya wa jezi pale Yanga. Wanaingiza fedha nyingi kwa mwaka. Simba wanapaswa kutazama hii fursa ya jezi zaidi. Ni fursa kubwa.

Simba inaweza kupata mabilioni ya fedha kwenye mauzo ya jezi kila mwaka. Uzuri mkataba wa sasa unamalizika. Watapata zaidi.

Columnist: Mwanaspoti