Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ni kweli Simba amekufa kiume?

Simba Rejea Ni kweli Simba amekufa kiume?

Fri, 5 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imetolewa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Wydad Casablanca. Huu ni muda wa Simba kurudi kuutazama mchoro upya. Ni muda wa kujipanga upya kwenye usajili. Ni muda wa kuendelea kuboresha masilahi ya wachezaji. Ni muda wa kumaliza mechi kama hizi nyumbani.

Simba imewahi kucheza hatua ya fainali ya mashindano ya CAF kabla kanuni na mifumo haijabadilika, kwa hiyo kufika robo fainali sio lolote sio chochote. Moja kati ya sehemu ambayo Simba wanapaswa kuboresha ni eneo la wachezaji hasa wale wa kigeni. Kwenye wachezaji 12 waliosajiliwa na Simba msimu huu ni kama sita tu ndiyo wamekuwa na msaaada. Wengine wote ni kama watumishi hewa.

Hata wachezaji wa ndani nao ni wanne tu ndiyo wamekuwa na mchango mkubwa. Ukiondoka Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Aishi Manula na Dennis Kibu waliobaki wote kwa sehemu kubwa hawakuwa na msimu mzuri. Hakuna dawa nyingine, ni kuendelea kuwekeza kwa Wachezaji wazuri.

Simba inahitaji sasa kutanua ufalme wake wa Uwanja wa Mkapa. Ni muda wa kuwa na timu yenye uwezo pia wa kuvuna pointi nyingi ugenini. Simba inahitaji kuwapa mkono wa kwaheri wachezaji wote hewa kikosini.

Ni muda wa Simba kuanza kutengeneza sasa timu mpya. Timu ya ushindi yenye mchanganyiko mzuri wa umri na uzoefu. Kujivunia robo fainali ni mawazo ya kimasikini. Simba ni kubwa sana. Ni muda wa kwenda kuweka heshima Afrika. Ni muda wa kujipanga kikubwa kuelekea msimu mpya wa mechi za kimataifa.

Marekani wana msemo wao maarufu sana unaosema “America is too great for small dreams." Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kuwa “Marekani ni taifa kubwa ambalo watu wenye ndoto ndogo sio mahali pao."

Marekani sio saizi yako. Kama una ndoto za kustaafu ukiwa na genge la kuuza matunda Marekani sio saizi yako. Kama una ndoto za kuuza mitumba miaka yote, pale sio mahali pako.

Baada ya mikwaju ya penalti kupigwa kwenye Dimba la Mohammed V, jijini Casablanca, Morocco katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kushindwa kusonga mbele, tuliona kila aina ya pongezi kwenye vyombo vya habari.

Simba kwa mara nyingine ilishindwa kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali, lakini watu wanapongeza. Wapo wanaosema Simba waliupiga mwingi. Wengine wanasema Simba wamekufa kiume.

Mpira wetu wakati mwingine tunauendesha kwa mihemko sana. Kuna muda tunajifariji tu. Tunaridhika na vitu vidogo. America is too great for small dreams. Lazima tujifunze kuwa na ndoto kubwa na tupunguze kupongezana kwa mafanikio kidogo. Lazima tuishi Kimarekani sasa. Lazima tuwe na mtazamo wa kuwaza mambo makubwa. Kwenye mchezo wa soka kushinda kombe ndiyo mafanikio ya kweli. Nyingine ni hatua tu za kujifariji.

Hata timu ikitolewa fainali hayo sio mafanikio. Ni hatua tu kubwa kwenye soka. Mchezo wa soka una bingwa mmoja. America is too great for small dreams. Kama una ndoto ndogondogo Marekani sio saizi yako.

Ni kweli Simba imekufa kiume? Jibu la mtu mwenye ndoto ndogo ni ndiyo. Jibu la mtu mwenye ndoto za Kimarekani ni hapana. Huku kupongezana na kupokeana airport huku tukiamini Simba iliupiga mwingi ni kujifariji.

Kutiana moyo kila siku, Simba imefanikiwa sana kwenye soka la Afrika ni kujidanganya. Simba bado haijafanikiwa kimataifa isipokuwa kuna hatua wamesogea mbele kidogo tofauti na rekodi yao miaka 20 ya karibuni.

Mambo ya kuambiana Simba imekufa kiume hayausaidii mpira wetu. Kitendo cha Simba kushindwa kwenda nusu fainali kwa mara ya tatu sasa ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni sio jambo la kufanya sherehe. Sio jambo la kujipongeza.

Ni habari mbaya kwa wana Simba. Ni majonzi kwa mpira. Simba haina cha kujivunia chochote kutolewa na Wydad Casablanca. America is too great for small dreams. Kama una ndoto ndogo, Marekani sio saizi yako. Kama una ndoto ndogo Ligi ya Mabingwa Afrika sio saizi yako.

Kufa kiume haipaswi kuwa sifa ya Simba. Haiwezekani timu inatolewa hatua ya robo fainali kila siku halafu wanaona ni ushindi. Kama Simba inatolewa kila siku kiume, ni kwa nini na wao wasishinde kiume? Kutolewa ni kutolewa tu na hakuna jipya lolote la kufurahia msimu huu kimataifa.

Kufa kiume sio jambo la kujivunia. Ni aibu kwa timu kama Simba. America is too great for small dreams. Simba inahitaji wachezaji wenye malengo ya ubingwa wa Afrika. Simba inahitaji kocha mwenye malengo makubwa. Simba inahitaji uwekezaji mkubwa.

Kama uko Simba na unawaza kushangilia robo fainali ya Mabingwa Afrika, Simba sio saizi yako. Simba ni kubwa sana kwa watu wenye malengo madogo. Kushinda peke yake nyumbani bado inaonekana haitoshi kukufanya kutwaa ubingwa.

Columnist: Mwanaspoti