Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ngoro; mfumo wa kilimo unaohifadhi mazingira

1071e8bc342dc5aa157de8932c8240e2 Ngoro; mfumo wa kilimo unaohifadhi mazingira

Sat, 5 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NGORO ni aina ya kilimo kinachohifadhi mazingira kwa njia ya asili ambacho kinaaminika kilianza kutumika na wakulima wa kabila la wamatengo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma zaidi ya miaka 300 iliyopita.

Kilimo cha ngoro kilianzishwa na wazee maarufu wa kabila la wamatengo waliotokea nchini Malawi katika karne ya 17 ambapo tayari vizazi zaidi ya 10 vimepita hivi sasa tangu kilimo cha ngoro kilipoanzishwa katika wilaya ya Mbinga.

Ngwatura Ndunguru, Mbunge Mstaafu wa Mbinga anataja moja ya madhumuni ya kuanzisha kilimo hiki ni kuudhibiti udongo wa juu wa ardhi ambao kwa kawaida huondolewa na maji au upepo kutokana na mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba nyingi ya kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora.

‘‘Tunajua kuwa udongo ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi vizuri. Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya mmomonyoko ni hasara kubwa kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno,’’ anasisitiza Ndunguru ambaye pia ni Mkurugenzi Mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Anasema njia hizo za kuhifadhi ardhi zinazoweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo kama ni maeneo ya mwinuko au tambarare.

Hata hivyo, zinaweza kutumika njia mbili au tatu katika shamba moja. Kimsingi, ziko njia kuu mbili za kuhifadhi ardhi ambazo ni njia za asili (kienyeji) na njia ya kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina na wataalamu.

Wataalamu wakongwe kama akina Bike mwaka 1938, Stenhouse mwaka 1994, Temu na Bisanda mwaka 1966 wanaeleza kuwa Wamatengo walilazimika kutumia kilimo cha ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri uliopo katika miteremko ya eneo lao.

Katika mashimo ya ngoro hupandwa mazao kama maharage, mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo. Mkulima hufyeka shamba lake na kuzipanga nyasi zilizokatwa kwenye mashimo ya ngoro.

Mkulima akipindua udongo wa chini kuwa juu hukata nyasi na kwamba udongo wenye rutuba hugeuka kuwa mboji na rutuba huongezeka.

Maji ya mvua yakisimama katika mashimo ya ngoro hulinda unyevu wa ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.

Inaaminika kuwa kilimo cha ngoro ambacho tunaweza kukiita draft agriculture kinahusishwa na shughuli za kuwepo kwa mapango ya ya watu kuishi.

Historia ya Wilaya ya Mbinga inaonesha kuwa, hapo zamani wananchi wa Wilaya ya Mbinga walikuwa na tabia ya kufanya kilimo cha kuhamahama.

Wakulima wakati huo walilima sehemu moja na wanapogundua sehemu hiyo rutuba imemalizika walikuwa wanahamia sehemu nyingine yenye rutuba na kuendesha kilimo bila kujali athari za kimazingira ambazo zilikuwa zinajitokeza kutokana na aina hiyo ya kilimo.

Kutokana na kuwepo kwa mapango, wazee hao wa kabila la wamatengo waliamua kuanzisha kilimo cha kulima na kufukia majani ili kupata mbolea ya asili hivyo kuendesha kilimo walichokiita ngoro katika sehemu moja bila kuhama huku wakirutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na ardhi ya Mbinga kuwa na milima yenye miteremko mikali.

Mbunge mstaafu wa Mbinga, Ngwatura Ndunguru anasisitiza kuwa wamatengo tangu wameanza kutumia kilimo cha ngoro miaka 300 iliyopita hadi sasa wamekuwa wanazalisha vyakula kwa wingi na kuhifadhi mazingira kwa njia ya asili kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokea kwenye miteremko ya milima ya umatengo wilayani humo.

Anabainisha zaidi kuwa katika kilimo cha ngoro mvua zinaponyesha maji huingia kwenye mmea na majani yaliyowekwa chini yanaoza ambapo katika msimu mwingine majani yaliota kwenye shimo yatafyekwa, mazao yaliosalia yanavunwa na kutandazwa kwenye shimo na kufukuliwa majani ya mwaka jana ambayo tayari yanakuwa mboji.

John Mbunda (80), mkazi wa kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga anasema wamatengo walipoanzisha mfumo huo maalumu wa kilimo cha ngoro uliwasaidia sana na kwamba kwa kabila la wamatengo ulijulikana kama Ingoro.

Anasema mfumo huo uliwawezesha kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima bila ya kusababisha mmomonyoko wa udongo au kuathiri rutuba kwenye mashamba yao.

Alex Ndunguru, mkazi wa Kijiji cha Ilela anasema wenyeji wa Mbinga walilazimika kubuni kilimo cha ‘ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko ya Umatengo na kwamba ngoro ndiyo mkombozi katika kilimo kwa kuwa kilimo kimekuwa endelevu badala ya mfumo wa zamani ambao wamatengo walifanya kilimo cha kuhamahama.

Utafiti umeonesha kwamba teknolojia ya ngoro ni bora zaidi katika kilimo, ambapo wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakifika katika Wilaya ya Mbinga kujionea wenyewe na kujifunza teknolojia hiyo inayohifadhi ardhi na kutunza mazingira kwa muda mrefu.

Moja ya faida ya kilimo cha ngoro ni kwamba hata kama mvua hazitanyesha, bado shamba litaendelea kuwa na unyevunyevu kutokana na maji yaliyomo ndani ya mashimo hayo.

Kulingana na Mbunge Mstaafu wa Mbinga, Ndunguru, tayari wameanza kukitangaza kilimo hicho na kukiingiza kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana katika wilaya ya Mbinga pekee.

Baadhi ya wageni ambao wamekuwa wakitembea kwenye magari kupitia barabara ya Mbinga hadi Mbambabay Wilaya ya Nyasa pamoja na maeneo mengine ya milima ya umatengo wamekuwa wakisimama mara kwa mara kwenye milima hiyo na kuchukua picha za kawaida na video.

Ndunguru anasisitiza kuwa kilimo cha ngoro kimeonekana kuwavutia watu wengi wa ndani na nje ya nchi hasa mimea inayochomoza na kuonekana mfano wa mapambo yaliopambwa juu ya milima ya Umatengo.

Wizara ya Kilimo imeanzisha Mradi wa kufufua Mifumo muhimu ya asili ya kilimo duniani (Global Importance Agricultural Heritage System- GIAHS) ili kuendeleza kilimo cha asili na kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji.

Taarifa kutoka Idara ya Matumizi Bora ya Ardhi Katika Wizara hiyo inaeleza kuwa mradi huo unatekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ambao unalenga kutambua mifumo ya asili na endelevu ya kilimo na ufugaji ili kumsaidia mkulima.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo katika Afrika Mashariki, nchi ya Tanzania na Kenya ilichaguliwa kufufua mifumo hiyo kwa kuwa na sehemu muhimu za kilimo na kwamba baada ya kuchaguliwa nchi ya Tanzania ilipendekeza mifumo mitatu ya kilimo asili ukiwemo mfumo wa Ngoro ambao unatumiwa na kabila la wamatengo.

Mifumo ya asili ya kilimo ilianza kupendekezwa duniani tangu mwaka 2002. Baadhi ya nchi ambazo zimeanza kutumia mifumo hii ya asili katika kilimo ni Japan, Ufilipino, China na Ujerumani.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari Mkoa wa Ruvuma.

Columnist: www.habarileo.co.tz