Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ngoma za asili zinakufa, hajali

F2b87e7605d7cd891142c91bb7439725 Ngoma za asili zinakufa, hajali

Fri, 4 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI fulani, taifa la Tanzania lilisifika katika kuendeleza mila na utamaduni wetu, ikiwemo kupiga na kucheza ngoma za asili za kila kabila.

Ngoma za makabila zilichezwa mashuleni, majeshini na kwenye sherehe na hadhara mbalimbali. Watu mbalimbali walifanyia tafiti ngoma hizo na wengine wakaanza kuzipiga kwa kutumia ala za kisasa, lakini, katika miaka ya hivi karibuni, utaratibu huo wa kuenzi na kucheza ngoma za asili ya makabila yetu, umeshika sana na unaelekea kusahaulika.

Vijana wanaozaliwa sasa, ukiwaambia vitu kama lizombe, mdumange, sindimba, muhambo, mganda na kadhalika wataona unazungumza msamiati ambao hawajawahi kuusikia.

Mila na utamaduni wa mtanzania ni pamoja na kutukuza asili ya maisha ya makabila yetu, ngoma na lugha zetu za asili nazo zikiwemo. Hizi zilichukuwa nafasi kubwa kudumisha mhimili wa taifa hili.

Kila kabila nchini kwa kwaida ina ngoma zao za asili na kuzitukuza katika kila matukio ya kitaifa na kimataifa na hata mila na desturi za makabila zilitumika katika kujitambulisha. Taifa lilifikia katika hatua hii nzuri ambayo Mwalimu Nyerere alifanikiwa katika hili.

Moja ya mafanikio ya utambulisho wa utaifa wetu kupitia utamaduni yalionekana mwaka 1970 katika maonesho ya utamaduni wa kimataifa yaliyotambulika kwa ‘Expo’ nchini Japan.

Katika maonesho hayo yaliyotambulisha uhalisia wa utaifa wa kila nchi, Tanzania iliwakilishwa na Kikundi Brass Band cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania kiliongozwa na John Dotto Mayagilo, Bendi ya Muziki wa Dansi ya Afro 70 chini ya Patrick Balisidya, Moris Nyanyusa na Super Volcano iliyoongozwa na Mbaraka Mwishehe Mwaruka.

Kwa bahati mbaya sana walioongoza vikundi vyote hivi vilivyotuwakilisha nchini Japan kwa sasa ni marehemu.

Walio na kumbukumbu hai watakuwa mashuhuda wa taarifa kuwa banda la Tanzania lililokuwa na vikundi hivyo lilitia fora kutokana na kupiga ngoma za asili ya makabila yetu!

Walikonga nyoyo kwa sababu waliwakilisha utaifa wetu, walipiga na kucheza mirindimo ya ngoma za asali ya makabila yetu, hivyo waliwakilisha utaifa wetu na taifa likaonekana kuwa hai mbele ya mataifa lukuki yaliyoshiriki maonesho yale!

Lakini ilikuwa ni katika mwaka huo wa 1970 baadhi ya vikundi na bendi za Tanzania viling’ara katika tamasha la Mtu Mweusi lililofanyika Lagos, Nigeria ambako huko nako utamaduni wa kitanzania kupitia mirindimo ya ngoma za asili ulilitambulisha taifa hili kwa mafanikio makubwa.

Wakati huu niandikapo haya ni shuhuda pia wa namna utawala wa enzi ya Mwalimu Nyerere ulivyosimama kidete katika kutilia mkazo udumishaji wa ngoma za asili kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa na mambo yakawa sawa.

Ngoma za asili ambazo ni sehemu ya kudumisha utamaduni zilichezwa kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi mitaani ambako kulikuwa na vikundi vya utamaduni na vilitia fora.

Ikumbukwe kuwa, ngoma za asili ni kati ya mambo yaliyobeba dhamana ya uhai wa taifa uliochaguliwa na Mwalimu Nyerere, ambapo hadi mwishoni mwa mwaka 1990 uhai wa vikundi mbalimbali vilishamiri katika sehemu kubwa ya miji ya mikoa na majiji kama Dar es Salaam.

Walio mashuhuda wanatambua namna ambavyo jiji la Dar es Salaam lilivyokuwa na shamrashamra za matumbuizo ya vikundi mbalimbali vya ngoma asili katika kumbi za kila kona, ambapo pamoja na kuwa sehemu ya burudani kwa jamii, pia vikundi hivi vilitumika kama mojawapo wa ajira kwa wasanii wa rika zote!

Viko wapi hivi sasa vikundi vya ngoma asili vya Kibisa Dancing Troupe, Makutano Dancing Troupe, Ujamaa Ngoma Troupe, DDC Kibisa, Ida Nnole ama Bantu Acrobatic ambavyo enzi ya udumishaji wa ngoma zetu za asili vilikuwa vikitetemesha jiji la Dar es Salaam.

Matunda ya kuenzi utamaduni wetu kupitia ngoma za asili ndiyo yaliibua burudani ya vikundi kama Muungano Dancing Troupe na TOT ambavyo siyo tu vilikuwa vina washabiki lukuki bali vilikuwa vikicheza ngoma za makabila yetu mengi na hivyo kuwa sehemu ya kudumisha uhai wa taifa!

Siamini kuona leo hakuna tena vikundi hivi ambavyo vilikuwa na wafuasi zaidi ya burudani nyingine na hata kujaza kumbi za jijini Dar es Salaam za DDC Kariakoo, Vijana, DDC Keko, DDC Magomeni Kondoa, Dimax, Mango Village, CCM Kata 14, Mkirikiti, Kwa Mama Bar, Omax, Mazuria, Ruvuma Mpaka Maputo, Super Mini Bar, Lango la Jiji na kadhalika!

Kufanikiwa kwa vikundi hivi kuwa sehemu ya burudani ndani ya jamii kuliwezeshwa pia kwa kuhamasishwa kupitia vituo vya radio vilivyokuwapo na kutekeleza kwa vitendo udumishaji wa utamaduni wa taifa.

Ngoma za asili za makabila ya Tanzania zilitumika kwa kiasi kikubwa pia na bendi za muziki wa dansi nchi zilizotunga, kupiga na kuimba mirindimo asili na hata kupendwa pia.

Bendi kama Tabora Jazz, Kilwa Jazz, Moro Jazz, Dar Jazz, Afro 70, DDC Mlimani, Juwata Jazz ilikuja kuitwa OTTU Jazz na sasa Msondo Ngoma, UDA Jazz, Asilia Jazz, Biashara Jazz kwa kuzitaja chache ni kati ya makundi yaliyodumisha mila na utamaduni wa mtanzania kwa kupiga na kuimba nyimbo kwa mirindimo ya asili ya makabila yetu.

Wakati huu niandikapo makala haya ni kipindi ambacho jamii imeamua kusahau kabisa himizo sahihi la Mwalimu Nyerere la kuufanya utamaduni kuwa kiini cha uhai wa taifa na ngoma za asili kuwa sehemu ya udumishaji huu!

Wakati fulani majeshi yetu takriban yote yalikuwa na vikundi vya ngoma za asili na ungeweza kuviona katika hafla na dhifa mbalimbali, siku hizi ni kama hakuna.

Utamaduni ulibeba mila na desturi, lugha na maisha yetu asilia, lakini ngoma za asili zilitumika kama nembo sahihi ya kulitambulisha taifa hili na katika mazingira ya sasa ya kutozipa kipaumbele ni sawa na kuzika chaguo la Mwalimu Nyerere.

Iwapo tuna nia njema ya kuendelea kuenzi fikra za Mwalimu Nyerere za kutaka uhai wa taifa ubebwe na mila, desturi na utamaduni wetu ni wakati wa kufufua ngoma za asili na kuziendeleza kama ilivyokuwa enzi ya utawala wa awamu ya kwanza. Hii pia itakuwa ni namna ya kumuezi Mwalimu wakati tunaelekea kuadhimisha kifo chake Ijumaa ijayo.

Tuzifufue na kuzidumisha kwa kuzicheza kuanzia ngazi ya shule na mitaa kama ilivyokuwa zamani.

Zirithishwe pia kwa vijana vyetu vijavyo kwa kuziona zikichezwa mitaani ama katika kumbi kama ilivyokuwa katika kipindi cha kushamiri vikundi vya ngoma za utamaduni vilivyokuwako kwa wingi ambavyo siyo tu vilitoa burudani kwa jamii husika, bali vilizalisha ajira, hususani katika sehemu za mijini.

Columnist: www.habarileo.co.tz