Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ngoja tuone ‘Thank you’ za wiki hii

Kisinda Thank You Ngoja tuone ‘Thank you’ za wiki hii

Wed, 21 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mitandaoni wakubwa wameshika chati sasa hivi baada ya kuendelea kutumia kauli ya ‘Thank you’ kufukuza watumishi wasiotakiwa katika klabu zao. Instagram kumechafuka na rafiki zetu, Azam, Simba na Yanga wameanza kufyeka watumishi hewa.

Azam wanaongoza katika chati. Kwanini? Inaonekana kama vile wamekasirika baada ya kutokuwa na msimu mzuri katika Ligi kuu licha ya msimu uliopita tajiri mtoto, Yusuf Bakhresa kwenda Afrika Magharibi na kuleta vifaa vya uhakika ambavyo alihisi vingevunja ufalme wa Simba na Yanga katika soka letu.

Matokeo yake Yanga akawa bingwa, Simba akashika nafasi ya pili bila ya hofu, lakini walipokwenda katika fainali zao wenyewe za Shirikisho wakafungwa bao la mapema na Kennedy Musonda shughuli yao ikaishia hapo Yanga akawa bingwa wa mataji mawili.

Naona tajiri amekasirika na anaweka mipango sawa. Kuna wachezaji wameagwa pale. Kina Raymond Kola. Walionekana kama vile wameridhika kukaa benchi na kuchuma mishahara. Ameagwa pia mdogo wangu, Cleophas Mkandala.

Mkandara alikuwa fundi wa mpira kweli kweli pale Dodoma Jiji. Amecheza Azam kwa miezi 12 tu na wala hakupata nafasi ya uhakika. Anakuwa muhathirika wa kikosi kipana cha Dodoma. Hata Aziz Kader naye anakuwa muathirika wa hilo.

Upande mwingine hawa matajiri wameamua kumsafishia njia kocha wao mpya, Youssouph Dabo kwa kumuondolea watu wengi wa benchi aliowakuta ili aanze upya na majanga yake msimu ujao. Walianza kusafishwa wazungu halafu panga likafika kwa marafiki zangu wawili, Kally Ongala na Agrey Moris.

Hapa nilichoka kabisa. Ongala ni rafiki wa karibu wa tajiri Yusuf Bakhresa na hata sasa hivi ataenda kuwa mshauri wake wa karibu wa mambo mbalimbali kuhusu timu. Hawajakutana barabarani. Wametoana mbali.

Agrey amecheza klabuni hapo kwa muda mrefu kabla ya kugeukia ukocha. Najiuliza kama yalikuwa maamuzi ya matajiri kuwaondoa ili kumuchia Dabo utawala wake wa kujua anayemuhitaji katika benchi au vinginevyo.

Nilidhani wote wawili au mmoja kati ya Ongala na Agrey angebakia kikosini kwa ajili ya kumuelewesha kocha mpya kuhusu mazingira ya klabuni hapo na soka la Tanzania kwa ujumla. Klabu nyingine Afrika au hata Ulaya huwa zinatumia utamaduni huo.

Inachoonekana ni kwamba ‘Thank you’ za Azam zimelenga zaidi katika kumuachia kocha uhuru wake ili ashindwe mwenyewe pindi msimu mpya wa michuano mbalimbali utakavyowadia. Hawataki lawama yoyote kutoka kwake.

Rafiki zangu Simba nao wametembeza ‘Thank you’ kwa benchi karibu lote la ufundi. Amebakia kocha tu Robertinho. Nadhani kwa sababu walikuja katika njia tofauti labda Robertinho ameona ni bora alete watu wake anaowaamini.

Lakini labda pia kocha ameona wengi kati yao hawana uwezo wa kufanya kazi kwa mwendo wake. ingewezekana wengine wasiagwe kama angewaamini zaidi. Tutasubiri kujua kama na Juma Mgunda hatakutana na ‘Thank you’.

Tayari alishaagwa Augustine Okrah na sasa tunasubiri kuona barua zikitembea kwa kasi wiki hii iliyoanza jana. Naambiwa wakubwa wamekuwa na vikao vizito na wanataka kutembeza noti kwa ajili ya kuwafunga mdomo watani wao ambao wamekuwa wakitamba kwa misimu hii miwili bila ya majibu.

Kule Jangwani jana niliongea mengi kuhusu ‘Thank you’ ya kocha Nabi. Ilitushangaza wengi lakini kuna dalili kwamba hawakuachana kwa amani sana ingawa wameachana kwa mafanikio. Kila upande unaweza kujivunia kitu katika ndoa yao.

‘Thank you’ nyingine ya lazima ilikwenda kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na wote tulijua kwanini ilikuwa lazima aagwe. Kesi yake ya muda mrefu na timu yake ilimalizwa Ikulu kwa kauli ya Mama ambayo kwa wengine wanahisi kama lilikuwa ombi, lakini kwa sisi wengine tunajua kuwa ombi la Rais ni amri.

Juzi jioni wakati watu tukishuhudia pambano la Taifa Stars dhidi ya Niger pale uwanja wa taifa tukaletewa taarifa kwamba winga Tuisila Kisinda alikuwa ameagwa. Tukaingia katika simu na kukuta ukweli wa taarifa hii ambayo haijashtua sana.

Tuisila alikuwa kwa mkopo Yanga akitokea katika klabu ya Berkane. Jinsi gani maisha yanavyokwenda kasi ni namna ambavyo Yanga walipambana kuliingiza jina la Tuisila Kisinda katika orodha yao mwanzoni mwa msimu baada ya kuonekana kuwa wamechelewa kuliingiza jina hilo.

TFF ikawekwa kikaangoni na mashabiki wa Yanga kwamba walikuwa hawaitakii mema klabu yao. Baadaye jina lake likachomekwa kwa ujanja ujanja tu. kilichotokea wakati msimu unaanza walitamani hata Tuisila mwenyewe asingerudi.

Alikuwa Tuisila yule yule aliyeondoka nchini. Kasi kubwa bila ya maarifa. Kumbukumbu yake pekee aliyowaachia ni bao lake la tatu dhidi ya TP Mazembe. Vinginevyo msimu ulioisha winga pekee ambaye ambaye labda hadaiwi sana na Wanayanga anabakia kuwa Jesus Moloko.

Tuisila hakuongeza kitu, wakati Bernard Morrison hakuonekana uwanjani zaidi ya kuonekana mara nyingi mitandaoni. Sijui kama ‘Thank you’ haitamfuata lakini ninachojua ni kwamba katika eneo ambalo Yanga watakaribisha watu wa maana msimu ujao basi ni pembeni.

Wiki hii itaendelea kuamua wengi ambao wanaondoka huku wakiagwa mitandaoni. Naamini hali itakuwa mbaya zaidi ya wiki iliyopita na sisi wengine tutaendelea tu kuwachambulia ni kwanini baadhi ya watu huwa wanaagwa.

Baada ya hapo nadhani Julai mwanzoni tutanza kukaribisha vifaa vipya kwa ajili ya msimu ujao. Vyovyote ilivyo, vita kubwa ya Julai itakuwa kwa hawa mafahari watatu ambao ni Yanga, Simba na Azam. Rafiki zangu Singida Fontaine Gate wana nafasi ya kujinyakulia mastaa, lakini ni kama mastaa hao hawawaniwi na wakubwa. Kabla hawajafanya lolote, swali ni je, wataweza kumzuia Bruno Gomes asije mjini?

Columnist: Mwanaspoti