Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndemla tuliyemsubiri, tumemuona

Said Hamis Ndemla.jpeg Said Ndemla

Sun, 15 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wengi wa soka Tanzania wanakumbuka mwaka 2013, wakati Yanga ilipokuwa inavaana na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Mkapa).

Waliojaa uwanjani waliondoka dakika 45 za mwanzoni, baada ya Yanga kuwa mbele kwa mabao 3-0, wa Simba waliondoka na Yanga wakabaki wanashangilia dakika zote 15 za mapumziko, huwa yanasemwa mengi, lakini hayawezi kufunika uhalisia wa mchezo wenyewe.

Baadhi ya yale ambayo yapo wazi ni kwamba, wakati wa mapumziko Simba ambayo ilikuwa chini ya Abdallah Kibadeni, kocha huyo alipoingia kwenye vyumba aliwauliza wachezaji wake, kama kuna anayeona hataki kuendelea kucheza mechi hiyo avue jezi akae pembeni, alirudia mara tatu kauli hiyo.

Mwisho yalifanyika mabadiliko, sina haja ya kuwatajia wachezaji wengi ambao waliingia bali nakutajia jina la kiungo mwenye umbo dogo, Hamis Said Ndemla, ambaye aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya mtu.

Taarifa zinaonyesha kuwa Ndemla alijiunga Simba kutoka chini, kwa wale waliokuwa wanafuatilia mazoezi ya timu ya vijana msimu wa 2011/12, watakubaliana nami kuwa alikuwa mmoja kati ya wachezaji wadogo sana kwenye timu hiyo.

Hata alipoingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Yanga ndiyo ilikuwa mechi yake kubwa kuonekana mbele ya mashabiki wa Simba na umbo lake halikuwafanya wengi waamini kuwa angeweza kufanya mambo makubwa, alionekana kinda sana, lakini ule ndiyo ulikuwa mwanzo wa Ndemla wa leo unayemuona kwenye jezi ya Singida Big Stars.

Huyu ni Ndemla ambaye alikaa Simba karibu miaka 10 kwa uvumilivu mkubwa hadi msimu mmoja nyuma alipoamua kuondoka na kwenda Mtibwa Sugar na sasa Singida, Ndemla aliishi kwenye dunia yake mwenyewe, aliishi kwenye dunia ambayo kila shabiki anafahamu soka na kila shabiki anafahamu ni mchezaji gani mzuri na yupi mbaya.

Alikaa Simba kwa muda mrefu lakini hakuwahi kupata nafasi kikosi cha kwanza, ni sawa na kipa wa sasa wa Aston Villa, Emiliano Martinez na Arsenal, alikaa pale miaka 10 lakini hakupata nafasi kikosi cha kwanza, alipoondoka ameonekana kuwa lulu, yupo kikosi cha kwanza Aston Villa, ametwaa Kombe la Dunia na ametwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Kombe la Dunia. Utamwambia nini sasa.

Hapa ndipo alipo Ndemla, anaweza kuwa Singida kama mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kwenye ligi, lakini anaweza kuwa mchezaji aliyefundishwa na makocha wengi bora ambao walikuja nchini, sasa anavuna matunda ya uvumilivu wake.

Ndemla ni panga pangua kwenye kikosi cha Singida, timu ikifunga mabao matatu akiwa uwanjani utaona mchango wake, Singida ikishinda bao moja kwenye ligi pia utaona mchango wake, ameonekana sasa hana haja ya mashabiki kumpigia kelele, wengi wanachohoji kwa sasa ni kwa nini Simba walimuuza, lakini amefika, hapa ndiyo sehemu yake salama zaidi.

Akiwa Simba mashabiki walikuwa na sifa moja tu kwake, anajua kupiga mashuti, anajua kufunga mabao ya mbali, ni kiungo bora, lakini akipangwa wanasema siyo hadhi ya Simba, hatakiwi kuanza hawa ndiyo mashabiki wetu. Uvumilivu wa Ndemla leo unampa heshima kubwa, hakuwa na papara ya mafanikio alijua kuna siku atafika sehemu apewe ufalme na sasa ndiye mfalme kwenye kikosi cha Singida, kama kufaulu alianzia chini, shule ya msingi, sekondari hadi chuo, sasa anafanya kazi.

Inawezekana ukawa hujamfuatilia, mfuatilie sasa, huyu siyo yule wa Simba aliyekuwa anakula kucha kwenye benchi, siyo yule aliyepita Mtibwa ambaye uwanjani muda wote alikuwa na hasira, huyu ni kiungo ambaye kila mara unamuona uwanjani akitabasamu, anaonekana amefika alipokuwa anakwenda, hapa ni sehemu sahihi ambapo Ndemla anatakiwa kujenga kiota chake ni suala la muda tu lakini haionekani kama kuna ambaye anaweza kuumaliza ufalme wake kwa sasa, labda baadaye.

Sasa Ndemla akikosekana kwenye kikosi cha Singida mashabiki hawakai kimya wanauliza yupo wapi, kwa nini hayupo, lakini kipindi kifupi nyuma hakuna aliyekuwa anahoji kuhusu Ndemla, alikuwa akionekana kwenye jezi ya Simba wanauliza nani kakosekana hadi yeye ameanza.

Huyu ndiye yule aliyekuwa anasubiriwa, uvumilivu wake unamlipa sasa, kama kweli anajua kupiga mashuti, Singida ni sehemu yake sahihi ya kupiga mashuti, baba yake anaweza kukaa kila wikiendi kwenye televisheni akimuangalia mwanaye.

Jambo zuri kwa sasa ni kwamba yupo na mwenzake, walikuwa wote, anaitwa Ibrahim Ajibu Migomba, wote wamezaliwa mwaka 1996, wote ni vijana, wote wanajua mpira na walipata sifa kwa kipindi chao.

Ajibu naye hana tofauti na Ndemla alitoka timu ya vijana ya Simba, akapanda juu na kuweka mizizi, hakuna shaka kuwa ni kati ya viungo bora kuwahi kutokea hapa nchini, kila kocha amekuwa akimsifu kutokana na ubora wake.

Nakumbuka aliwahi kuwaka zaidi Simba mwaka 2015, alimaliza msimu vizuri, ni kati ya viungo bora, lakini naye maisha yake ya Simba, hayakuwa mazuri sana, alienda Yanga akapewa na unahodha, unashangaa ndiyo alikuwa nahodha kipindi cha Mwinyi Zahera, akawaka kweli kweli na heshima kubwa aliyonayo hadi sasa ni kupiga asisti 14 kwa msimu mmoja, hakuna shaka kuwa ni kati ya vizazi bora sana kuwahi kutokea hapa nchini.

Alirudi Simba baadaye, sijui nini kilitokea, hakuwa na umaarufu ule wa mwanzo ghafla akaibukia Chamazi na kujiunga na Azam, sasa yupo Singida akiwa na Ndemla, sijui kuhusu yanayosemwa sana kwake, ninachoamini ni kiungo bora akiamua ni mfungaji mahiri tena mabao ya kideoni, kama atakaa na kujitazama kwenye kioo na kusema sasa ndiyo wakati wangu.

Ndemla tumeshamuona hatuna shaka naye, tunasubiri kumuona Ajibu kwenye kilele chake cha mafanikio hatuwezi kumuona kama yeye mwenyewe atajificha, tutamuona kama ataamua mazoezini, nafikiri akae na Ndemla wanywe chai, wajadiliane kuhusu mustakabali wao.

Columnist: Mwanaspoti