Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndayiragije asiifanyie mzaha Stars

240d22d8b1e3324559ea6539b3315cfb Ndayiragije asiifanyie mzaha Stars

Sat, 17 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWISHONI mwa wiki iliyopita timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 na Burundi katika mechi ya kimataifa ya kirafi ki iliyochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Ingawa ilikuwa mechi ya kirafiki, lakini matokeo hayo yalihuzunisha mashabiki wengi wa soka nchini. Kwa sababu wengi waliamini yangepatikana matokeo mazuri kutokana na uwekezaji unaofanywa siku hadi siku kwenye malezi na matunzo ya timu hiyo.

Lakini pia inaaminika Stars ina kocha bora, baada ya kumuondoa Emmanuel Amunike aliyefutwa kazi baada ya michuano ya Afcon 2019 ambapo Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza baada ya takriban miaka 39 kupita.

Kila mtanzania aliyeona ile mechi na Burundi hakuridhika kwa namna timu ilivyopangwa mpaka mechi ilivyochezwa.

Tusijifanye hatuoni, mamlaka husika wamshtue mapema kocha Etienne Ndayiragije asifanye masihara na timu ya taifa, watu wanataka ushindi na pamoja na matokeo ya mpira yapo matatu, lakini bado timu ilikuwa na uwezo wa kuifunga Burundi katika mechi ile.

Stars ilifuzu hatua ya makundi ya kombe la dunia kwenye mgongo wa Burundi baada ya kutoka nayo sare kwenye mechi zote mbili kabla ya kuiondoa kwa matuta. Jambo la kushangaza, Burundi imebadilika maradufu ya vile mwanzo katika mechi zake na Stars, lakini Tanzania imeporomoka kiwango, nini shida.

Kwanini Watanzania wamekuwa wakali na matokeo ya mechi ile ya kirafiki, ni sababu ilikuwa mechi muhimu ya maandalizi kabla ya kuikabili Tunisia mwezi ujao kuwania kufuzu fainali za Afcon.

Kwa maana hiyo, wachezaji waliopangwa kwenye mechi ile ndio waliokuwa wakinolewa kutafuta kikosi kwa mechi hiyo na Tunisia. Si mechi nyepesi, na ndio maana watanzania wamekuja juu baada ya masihara yaliyofanywa na kocha katika kupanga kikosi.

Katika mechi hiyo na Burundi Ndayiragije kampanga kipa David Kisu wa Azam, hakuna shaka kipa huyo anafanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu kwa sasa, lakini ukweli lazima usemwe kuwa kipa namna moja wa Stars bado.

Kila mmoja aliyetizama mechi ile aliona mapungufu ya kipa yule, ingawa kila kipa ana upungufu wake lakini Kisu bado anatakiwa kutengenezwa na kujengewa uwezo kwa ajili ya kuandaliwa kuchukua namba Stars lakini sio kwa sasa timu ikijiandaa na michuano mikubwa.

Kama benchi la ufundi liliona lisimpange Aishi Manula siku ile, basi Metacha Mnata haikuwa vibaya kukaa langoni, huku Kisu akisoma kwa wenzie na kabla ya kuanza kuandaliwa.

Stars ina michuano mingi ukiacha hiyo ya kufuzu Afcon lakini tayari ipo kwenye fainali za Chan, ipo kwenye hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kombe la dunia Quatar 2022, yote hiyo michuano mikubwa na muhimu haitakiwi kufanywa masihara ya kujaribu kikosi kwa sasa, inatakiwa kazi kazi!.

Tuambiane ukweli kuna wachezaji kwenye kikosi kilichopita hawakutakiwa kuitwa, na kama waliitwa hawakutakiwa kuanza na wengine kuwekwa nje.

Mchezaji kama Ditrim Nchimbi ambaye hata kwenye klabu yake Yanga anakaa benchi ameitwa kwenye kikosi iweje? Kana kwamba haitoshi na kucheza akacheza na kila aliyetizama ile mechi aliona kilichotokea.

Kana kwamba haitoshi, kuna wachezaji wameitwa kutoka nje, Ally Msengi anayecheza Afrika Kusini, Thomas Ulimwengu anayecheza Congo DR, Simon Msuva anayecheza Morocco na Mbwana Samatta anayecheza Uturuki.

Si kwamba nalipangia benchi la ufundi mchezaji wa kuanza kwenye kikosi chake lakini kama linaona halina mpango kuwatumia wachezaji wanaocheza nje ya nchi basi haina haja ya kupoteza fedha kuwaleta.

Msengi, alicheza dakika za mwishoni mwa kipindi cha pili, Ulimwengu ndio kabisa sidhani hata kama mpira aligusa, aliingia bado dakika mbili kati ya zile tatu za nyongeza ziishe.

Huko ni kuwadhalilisha wachezaji wanaocheza nje ya nchi na kutowatendea haki. Kila mchezaji ana ndoto za kwenda kucheza soka ya kulipwa nje, sasa kama hao wanaocheza nje wakiitwa Stars hawapati namba hiyo hamasa ya wachezaji wa ndani kwenda nje itatoka wapi? Benchi la ufundi halilazimishwi kutumia wachezaji, lakini kama mchezaji anaitwa kutoka nje halafu hatumiki maana yake hayupo kwenye mipango ya kocha, ni vema hizo pesa zikatumika kwa kitu kingine mchezaji abaki anakocheza.

Ndiyo kuna mambo mengi ya kufanya kwenye soka yanahitaji fedha, timu za taifa za wanawake, Twiga Stars na ile ya vijana Tanzanite Queens ziko kambini kujiandaa na michuano mbalimbali, hizo fedha zinazogharamia wachezaji wasiotumika si ziwekwe huko kwa wanawake ambao kila kukicha shida kwao haziishi kutokana na kukosa udhamini wa maana.

Mamlaka ya soka, Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, isizunguke sana imwambie kocha Ndayiragije watanzania wanataka ushindi na furaha kwenye timu yao ya taifa sio kufanya majaribio ya wachezaji wakati huu tuko kwenye michuano muhimu.

Ndayiragije asiifanyie mzaha Stars Wachezaji wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije

Columnist: habarileo.co.tz