Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nani angeweza misimamo hii ya JPM

379735efdf70919222fda2de8e6839fe Nani angeweza misimamo hii ya JPM

Wed, 2 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

LEO ngoja nizungumze kidogo kuhusu mambo mbalimbali ya taifa letu na huu ni uwazi kabisa kutoka ndani ya moyo wangu.

Mimi kwa umri wangu huu wa miaka 23 nimekuta, kuonana, kusikia na kuwasoma mashujaa kadhaa hapa duniani waliopita na wengine waliopo bado kwenye kizazi chetu cha sasa.

Nimesikia na kusoma habari za watu waliopambana kwa ajili ya Watu Weusi nchini Marekani; akina Martin Luther King Jr, William Sylvester, Malcolm X, William Du Bois, Marcus Garvey na wengineo.

Aidha, nimesoma magwiji wengi waliobadilisha mtazamo wa dunia kuhusu haki za wanyonge waliokuwa wakinyonywa na mabeberu, akina Carl Max, Mao Zedong, Vladimir Lenin na kadhalika.

Nimesikia na kusoma pia wanaharakati na wanamapinduzi wakubwa wa ukombozi wa Bara la Afrika kutoka kwenye uonevu na unyonyaji wa kikoloni; akina Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkurumah, Patrice Lumumba, Nelson Mandela na wengine walioweka rehani uhai wao kwa ajili ya watu wao.

Kutoka moyoni mwangu, huyu mtu anayeitwa John Magufuli kwangu ndiye shujaa na jasiri wa Afrika kwa sasa. Wahenga walisema kweli kwamba ‘shujaa hasifiwi nyumbani kwao’.

Kwangu, Rais John Magufuli ni mmoja wa mashujaa na majasiri wachache sana ambao dunia imewahi kuwashuhudia.

Kwa kweli, kama kuna watu ambao sitawasahau kwa ujasiri, misimamo na ushujaa wao hasa linapokuja suala lenye maslahi ya watu wao, basi kwa sasa sijapata kuona mtu kama Rais Magufuli.

Huyu ni mtu aliye tayari kwa lolote linapokuja suala la nchi bila kuwa na woga wala kuangalia sura ya mtu yeyote.

Tuachane na jinsi alivyowashughulikia watu waliokuwa wamejikusanyia ukwasi mkubwa huku wakiutumia kuendelea kunyonya jasho la Watanzania wakiwa wamejivika ngozi ya ufadhili wa miradi mbalimbali ya wananchi, bali tuangalie msimamo wake wakati wa balaa la corona.

Wakati dunia ikiamini na ikihamasishana kufungia watu ndani kama njia ya kupambana na ugonjwa huo, Rais Magufuli yeye alikataa kuingia kwenye mtego huo wa kuua uchumi na watu.

Akahamasisha watu kuendelea kuchukua tahadhari zote dhidi ya corona na zaidi akalikabidhi taifa kwenye mikono ya Mungu, lakini siyo kumfungia mtu ndani.

Taifa likamtumainia Mungu, likaondoa hofu na Rais Magufuli akahamasisha watu kuomba na kufunga kwa ajili ya taifa kukombolewa na nguvu za muumba dhidi ya corona na hakuna nyumba ya ibada iliyofungwa.

Dunia nzima kuanzia Shirika la Afya Duniani (WHO), mataifa ya nje na mpaka majirani zetu katika eneo hili la Afrika Mashariki wakabeza sana njia tunazotumia kupambana na corona.

Wakaanza kuipigia kelele Tanzania kwa namna inavyopambana na corona huku wakianza kututenga, lakini bado Rais Magufuli aliendelea kusimamia imara.

Watu wakaendelea kufanya shughuli zao kwa tahadhari kubwa huku Serikali ikiwahimiza kufuata kufuata taratibu na kanuni zote muhimu dhidi ya ugonjwa huo.

Leo wakati dunia nzima na majirani zetu waliotupigia kelele kwa njia tunazochukua wakiendelea kuteswa na corona, sisi Tanzania makali ya gonjwa hilo yamebaki historia na kila mtu anaendelea na shughuli zake. Corona imepotea na imeshaisha.

Nani angeweza kuendelea na misimamo ile licha ya kila mtu kubeza huku wengine wakitutabiria kuokota maiti kila sehemu?

Leo hii ni wapi katika Tanzania ambako kumeokotwa maiti inayotokana na corona? Nasikia vyombo vya mabeberu vilikuja hadi vikaweka kambi kwenye makaburi, lakini havikuona kile walichopania kukiona. Ushujaa wa namna gani huu wa rais huyu?

Tuachane na suala la corona, twende kwenye msimamo wake kwenye madini. Nadhani tunakumbuka namna sekta ya madini ilivyokuwa kama ‘shamba la bibi’ kwa kila mtu kujitwalia rasilimali hizi za Tanzania bila woga.

Mfano mzuri ni kwenye madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee, lakini nchi yetu haikuwa kwenye orodha ya nchi zinazouza kwa wingi madini hayo duniani!

Hapa palithibitisha ushujaa mkubwa wa mwana huyu wa kweli wa Afrika, Rais Magufuli ambaye ‘amepindua meza’ na sasa Tanzania inachomoza kama kinara wa kuuza madini yake.

Unalikumbuka sakata la mchanga wa madini ya dhahabu kati ya nchi yetu na kampuni ya Acacia? Baada ya ripoti mbili za Profesa Mruma na Profesa Osoro kuthibitisha wizi wa madini yetu uliokuwa ukifanywa na migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, Tanzania tulidai fidia yetu ya kikodi kutoka kwa Acacia.

Kutokana na kuchukua hatua hizo huku majadiliano yakianza ili kampuni hiyo ilipe fidia zake na kodi, ghafla tukaanza kutishwa na Watanzania wenzetu kwa hatua hizo.

Mengi yakasemwa; kwamba tusingelipwa fidia yoyote, kwamba tunatafuta matatizo na mataifa makubwa, kwamba tutashitakiwa kutokana na kuvunja ghafla mikataba mibovu iliyokuwapo na kwamba, kinachofanyika ni kuua kabisa shughuli za madini Tanzania.

Rais Magufuli hakuangalia vitisho wala nini, bali kusimamia haki na sasa madini yanatuingizia pesa maradufu kuliko ilivyokuwa kabla ya Rais huyu huyu kuchukua hatua madhubuti bila kutetereka wala kuangalia ‘makunyanzi’ ya watu.

Hatua hiyo pia imetufikisha kwenye kuunda kampuni ya madini ya Twiga baina ya serikali na Barrick kwa kugawana faida huku kila upande ukinufaika. Nani angeweza misimamo hii?

Nawaza kwa ujasiri na misimamo hii ya Rais Magufuli, kama tungepata walau marais watano kama yeye hapa Afrika tungekuwa wapi leo jamani?

Hivi hawa mabeberu wanaolinyanyasa na kulibagaza Bara la Afrika kwa maslahi yao binafsi ,wangepata upenyo huo kweli?

Vipi kuhusu suala la ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere katika Mto Rufiji, eneo la Pori la Akibna la Selous? Kuliibuka maneno mengi sana kutoka kwa mabeberu na vibaraka wao wa ndani.

Madai makubwa yalikuwa mradi huo ungeenda kuharibu na kuathiri viumbe hai na binadamu waishio eneo hilo.

wa Kimataifa (WWF) ulipinga vikali mradi huo kwa madai kwamba ungesababisha mmomonyoko mkubwa wa ardhi na kupunguza rutuba ya eneo la Rufiji. Kama hiyo haitoshi, Bunge la Ujerumani lilipitisha muswada wa kuitaka serikali ya nchi hiyo kuzungumza na Serikali ya Tanzania ili kusitisha mradi huo.

Pamoja na kelele hizo, Rais Magufuli aliendelea kuweka msimamo mkali na kusisitiza kwamba mradi huo ni lazima ujengwe na kutekelezwa kwa sababu eneo lililokuwa linapigiwa sana kelele ni asilimia tatu tu ya eneo lote la Pori la Akiba la Selous.

Rais, mbali ya kueleza namna serikali yake ilivyojiridhisha kwamba mradi huo unatunza mazingira na siyo kuyaharibu, alisema kukamilika kwake kutapunguza gharama ya umeme kwa kiwango kikubwa nchini sambamba na kuipa nchi umeme wa uhakika.

Rais Magufuli aliusoma mchezo wa mabeberu ambao walishajua hatua anayochukua ni sahihi katika kuifanya Tanzania kujitegemea, wakaona hilo halijawakalia vyema.

Kwa mara nyingine Rais alisimamia msimamo wake wenye maslahi makubwa kwa nchi na mradi huo mpaka sasa unaendelea kujengwa.

Hadi utakapokamilika mwaka 2022, utaipatia nchi yetu umeme wa megawati 2115.

Huu ni msimamo imara na muhimu kwa taifa hili ambalo limejipanga kujenga uchumi wa viwanda unaohitaji kuwa na umeme mwingi, rahisi na wa uhakika.

Yako mengi kama nilivyogusia hapo mwanzo kama ya kupambana na watumishi hewa, mafisadi na wala rushwa, lakini ngoja nimalizie kwa msimamo wake mkali dhidi ya wakandarasi wazembe.

Toka kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Magufuli amekuwa mkali na ameweka misimamo dhidi ya wakandarasi wazembe wasiokamilisha miradi mbalimbali ya maji, barabara na majengo kwa wakati, au wanamaliza kwa wakati, lakini mradi ukiwa chini ya viwango vya ubora.

Waswahili wanasema, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Magufuli ni shujaa wa Tanzania, shujaa wa Afrika na dunia kwa jumla.

Mwandishi wa makala haya ni mchangaji wa makala haya. Mawasiliano yake ni 0657 475 347.

Columnist: habarileo.co.tz