Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nani aliamini Stars ingeshinda ugenini?

Kim Poulsen Kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen

Mon, 11 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni nani aliamini Taifa Stars ingeshinda ugenini kule Benin? Ni wachache sana. Tena wachache mno. Wengi waliongea kwa nje kuipa timu moyo, lakini moyoni mwao wanafahamu walichokuwa wakiwaza.

Unajua kwanini wengi hawakuamini? Tulia nitakueleza.

Katika mechi muhimu ya kushinda hapa nyumbani, Taifa Star ilijikuta ikipoteza. Ni mechi ambayo Watanzania wengi waliamini kuwa tutashinda. Ni mechi ambayo wengi waliamini imeshika hatma yetu. Lakini nini kilitokea?

Taifa Stars ilipoteza nafasi nyingi za wazi. Mwisho wa mechi tukapoteza 1-0 kwa Benin pale kwa Mkapa. Inaumiza sana. Na hapa ndipo Imani za wengi ziliishia. Wengi waliamini kama Benin ametufunga nyumbani tutawezaje kumfunga kwao? Inahitaji Imani thabiti.

Hata hivyo jana Jumapili Taifa Stars imeshinda pale Benin. Inafurahisha sana. Haya sasa ndiyo maajabu ya soka. Hii sasa ndio burudani yenyewe.

Bahati mbaya Watanzania tuna Imani Zaidi ya kushinda nyumbani. Hatuamini sana katika kupata matokeo ugenini. Hii tumeaminishwa zaidi na Simba.

Lakini leo nitawaibia siri moja. Mpira wa miguu uko tofauti sana.

Timu yoyote yenye ushindani inatakiwa kushinda popote. Hii ndiyo falsafa ya mpira wa miguu. Ukiwa unashinda kwenye uwanja mmoja tu, huwezi kufika mbali.

Unakumbuka Taifa Stars ilivyofuzu kwenda CHAN? Labda umesahau. Tulipoteza 1-0 dhidi ya Sudan pale kwa Mkapa. Tulipoteza nafasi nyingi sana katika mchezo huo. Mashabiki walifurika kwa wingi kweli kweli wakiamini Sudan ‘atakufa nyingi’, lakini mambo yakawa tofauti.

Nini kilitokea mechi ya marudiano pale Khartoum? Tulishinda 2-1 na kufuzu CHAN. Hivi ndivyo timu imara za soka zinapaswa kuwa. Unashinda popote.

Nigeria ilifungwa goli 1-0 na Afrika ya Kati hapo majuzi. Tena ilifungwa pale pale kwao Nigeria. Inauma sana. Lakini imekwenda ugenini na kushinda 2-0. Huu ndio mpira wa miguu.

Tanzania awamu hii tumepata alama nne ugenini. Tulipata sare pale DRC na kisha kushinda pale Benin. Hii ni ishara nzuri.

Shukran kwa kazi nzuri ya Kocha Kim Paulsen na mbinu zake.. Tumeanza kuwa wakubwa..

Columnist: www.tanzaniaweb.live