Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nanenane iangalie wakulima wadogo

1b1b88c66ce9e9d3ea5ec8091c1fc9c4 Nanenane iangalie wakulima wadogo

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZIMEBAKI wiki mbili kuanza kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane ambayop kitaifa imepangwa kufanyika katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yanawakutanisha wadau mbalimbali na kutoa fursa ya kuonesha bidhaa, teknolojia na ubunifu kwenye kilimo kwa lengo la kuongeza tija na wakulima kulima kilimo cha kisasa kinachokuza uchumi wao na wa taifa. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020“.

Kauli ambayo inaenda na tukio kubwa lilalotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu la Uchaguzi Ukuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Hvi karibuni, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema maadhimisho ya Nanenane mwaka huu yataanza Agosti mosi hadi 8, na lengo lake ni kutoa fursa kwa wadau kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Kwa kawaida maonesho hayo huwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi, Wabia wa maendeleo, wakulima na Vyama vya wakulima, wafugaji na wavuvi, ambao kila mmoja huonesha ubunifu na teklonojia zinazotumika kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.

Maonesho hayo ya Nanenane yaje na vitu tofauti zaidi vinavyosaidia wakulima na wananchi wanaotegemea kuhudhuria kupata ufahamu ,elimu na ujuzi zaidi wa jinsi ya kuboresha kilimo na kuondokana na kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha tija na kukuza uchumi.

Pamoja na kwamba Maonesho hayo ya 28, yanafanywa kitaifa mkoani Simiyu, lakini pia yatafanyika katika kanda nane ambazo ni Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Magharibi (Tabora).

Nyingine ni Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Ziwa Mashariki (Simiyu) na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza). Ninaamini kufanywa kwake kikanda ni kutoa nafasi kwa wakulima na wananchi wengi zaidi kushiriki maeneo ya karibu na kupata ujuzi, maarifa na kisha kubadilisha aina ya kilimo chao.

Kikwazo kikubwa miongoni mwa wakulima wadogo wengi nchini ni kulima kilimo cha kujikimu na hiyo wakati mwingine huchangiwa na ukosefu wa wataalamu wa masuala ya ugani, katika maeneo yao ambao wangewashauri jinsi ya kulima kisasa.

Sasa basi serikali na taasisi husika pamoja na wadau wa kilimo, ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha nguvu inaelekezwa kwa kupata wataalamu wa kilimo kuanzia ngazi ya kijiji ili wasaidia wakulima jinsi ya kulima kisasa na kupata mazao mengi lakini pia watawashauri jinsi ya kulima kulingana na hali ya hewa ya msimu husika.

Ingawa wataalamu wa kilimo wapo, lakini ni wachache mno kiasi kwamba hawawezi kuwafikia wakulima wote ambao wengine sio kwamba hawapendi kulima kisasa lakini kwa vile tu hawana elimu au hawawezi kutambua majira ya hali ya hewa na matumizi bora ya zana za kilimo ikiwemo dawa na mbegu bora, wanajikuta wanalima kwa mazoea na kupata mazao kidogo.

Sasa basi, rai yangu katika maadhimisho haya ya nanenane yajayo, nguvu zaidi itumike kuwafikia wakulima hususan wadogo ambao ndio wengi lakini wengi wao hawana elimu ya ugani hivyo hulima kwa mazoea.

Columnist: habarileo.co.tz