Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Namna maswali ya Kiingereza yanavyotesa watahiniwa darasa la saba

Mtihanii Form Four Namna maswali ya Kiingereza yanavyotesa watahiniwa darasa la saba

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Je, wajua kama anguko la ufaulu wa somo la Kiingereza kwa watahiniwa wa mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi, linaakisi ufaulu kiduchu wa somo hilo kwa miaka kadhaa?

Makala haya ya mtaalamu wa lugha nchini, yanachambua kwa kina kiini cha ufaulu mdogo wa somo hilo na kuangazia athari zikiwamo za ujenzi wa matabaka kama hali ya sasa ya matumizi ya lugha ya kufundishia haitofanyiwa mabadiliko

Mwandishi anachambua kitakwimu na kimifano, akionyesha baadhi ya maswali ya somo la Kiingereza yalivyotesa watahiniwa katika mtihani wa somo la Kiingereza mwaka 2022.

Simulizi watoto watatu

Makala inaanza na simulizi ya vijana watatu: Emily, Evance na Tunu.

Evance ni miongoni mwa wanafunzi bora watano pekee waliopata wastani wa B katika shule yake huko wilayani Ludewa, mkoa wa Njombe.

Katika shule hiyo wanafunzi wengi wamepata wastani wa C na D. Mbali na kupata wastani wa B, pia kwenye Kiingereza ndiye miongoni wanafunzi wachache waliofaulu kwa kupata alama C. Hakuna aliyepata B wala A katika shule yake.

Emily alianza masomo yake huko Ileje, mkoa wa Songwe. Ni mtoto wa mwisho katika familia yao. Kaka yake Emily ambaye ni wa kwanza kuzaliwa katika familia yao anaishi Dar es Salaam.

Aliamua kumhamishia mdogo wake katika shule mojawapo nzuri jijini Dar es Salaam. Lakini alipomfikisha shuleni walimfanyisha mtihani wakaona hataweza kuendana na wenzake kwa sababu uwezo wake uko nyuma sana.

Kaka yake Emily aliamua kukubaliana na ushauri wa walimu. Akamrudishia darasa la nyuma ili aweze kufanya vizuri. Wakati anatoka Ileje alikuwa darasa la sita lakini alipofika Dar es Salaam akarudishwa darasa la tano.

Mwaka huu 2023 naye amefanya mtihani. Kwenye Kiingereza amepata B. Kaka yake ananiambia hata hivyo amejitahidi sana kwani alikuja akiwa hawezi hata kuongea sentensi moja ya Kiingereza.

Tunu ni binti wa miaka 12 amemaliza darasa la saba katika shule mojawapo jijini Dar es Salaam. Wazazi wake ni maofisa waandamizi serikalini.

Tunu hakuwahi kupata shida yoyote katika safari yake ya maisha kwani baba yake ni mhadhiri chuo kikuu na mama yake ni mwanasheria wa wizara. Wazazi walihakikisha mtoto wao anaenda kusoma shule nzuri na yenye huduma zote muhimu. Katika matokeo haya Tunu amepata alama A katika masomo yote ikiwemo Kiingereza.

Wanafunzi hawa Emily, Evance na Tunu wanawakilisha makundi tofauti ya watoto wanaosoma nchini Tanzania katika mazingira tofauti kabisa.

Mbali na Kiingereza kuwa kigumu Tunu anapata A, lakini Emily anapata B kwa sababu kaka yake alichukua hatua ya kumsaidia, na Evance anaonekana kinara katika mazingira yake kwa kupata C.

Hili ndilo ninalomaanisha kuhusu kuamua kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia ni suala la kitabaka zaidi.

Hali ilivyo kwenye ufaulu

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), daraja A ni alama kati ya 41 – 50, B ni 31 – 40, C ni 21 hadi 21 – 30, D ni 11 – 20, na F ni 0 – 10.

Kwa hiyo kwa matokeo haya, aliyepata 21 anahesabika amefaulu na atajiunga sekondari mwakani 2024. Na akienda sekondari atatakiwa kumwelewa mwalimu anachofundisha na kujibia mitihani ya kidato cha pili na cha nne.

Amesoma Kiingereza kwa miaka mitano kuanzia darasa la tatu hadi la saba, na ameshindwa kuimudu hiyo lugha, na tunatarajia mwanafunzi huyu kuelewa masomo yake akiwa sekondari.

Hapo ndipo tunaona kiwango cha wanafunzi kuacha masomo kinakuwa kikubwa. Huenda sababu mojawapo kubwa inayowafanya wanafunzi wasiwe na motisha ya kupenda kuendelea na masomo ni lugha ya kufundishia.

Ili tuweze kuelewa vizuri kuhusu hali ilivyo, turejee ripoti ya Baraza la Mitihani kuhusu ufaulu wa somo la Kiingereza kwa mwaka 2021 na 2022 na 2023.

Mwaka 2021, kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi waliopata kati ya 21 – 50 (A, B, na C) ulikuwa asilimia 48.02, na mwaka 2022 ulikuwa asilimia 29.39.

Mwaka huu 2023 umeongezeka kutoka ule wa mwaka jana na kuwa asilimia 34.35. Kwa haraka utabaini kuwa hali ya ufaulu wa Kiingereza ni shida sana nchini ukilinganisha na ufaulu wa Kiswahili.

Hoja ya kuwa huenda Kiingereza kinachangia ufaulu mdogo wa wanafunzi wakiwa sekondari unachagizwa na kiwango cha ufaulu wao wa somo la Kiingereza wakiwa darasa la saba.

Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2019 na 2020 walifaulu darasa la saba mwaka 2015 na 2016. Mwaka 2015 ufaulu wa Kiingereza ulikuwa asilimia 48.6 na mwaka 2016 ulikuwa asilimia 36.

Hii inamaanisha kuwa kati ya wanafunzi 518,034 waliofanya mtihani mwaka 2015 ni wanafunzi 251,765 pekee ndio waliofaulu somo la Kiingereza, huku wanafunzi 199,904 kati ya wanafunzi 555,291 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2016 ndio waliofaulu somo la Kiingereza.

Hii inamaanisha kuwa kati ya wanafunzi 503,914 waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016, wengi wao walikuwa na shida kubwa ya Kiingereza.

Hali kadhalika kati ya wanafunzi 526,653 waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2017 na ambao walihitimu kidato cha nne mwaka jana 2020, ni wanafunzi 199,904 pekee ndio waliofaulu mtihani wa somo la Kiingereza.

Wanafunzi kushindwa maswali

Wanafunzi wanapokuwa sekondari wanatakiwa kumwelewa mwalimu anapofundisha na pia waelewe kinachoandikwa kwenye vitabu.

Bahati mbaya sana, Baraza katika ripoti zake mbalimbali linaonesha kuwa mitihani ya kupima uelewa wa matini za kusikiliza na kusoma ni mdogo mno.

Kiwango cha kushindwa kujibu maswali ya kusikiliza na kusoma insha na kujibu maswali yake kinadhihirisha kuwa watoto wengi hawajifunzi vizuri Kiingereza wakiwa shule ya msingi, na hali hii kuathiiri uwezo wa kujifunza wakiwa sekondari.

Tatizo hili linaweza kutokana na uwezo mdogo wa walimu shule zetu za msingi, au njia za ufundishaji siyo rafiki, au mazingira ya kujifunza na kuitumia lugha hayapo, na sababu nyingine kama vile kukosekana kwa motisha ya kuipenda lugha, na kadhalika.

Tuone mifano ya namna wanafunzi wanavyoshindwa kujibu maswali katika mtihani wa mwisho:

Mifano ya maswali ya Kiingereza ya Darasa la saba mwaka 2021 kwa mujibu wa ripoti ya uchambuzi ya Necta.

Wanafunzi walisomewa kifungu hiki cha maneno katika imla.

‘‘Everybody is supposed to behave well in any given circumstances. The act of conducting and presenting yourself with respect and honour is what is called manners. Let us talk about Sheila, a class six girl from Mwenge Primary School. She is a good example of a girl with good manners. When she has a problem, she seeks help from her teachers. If it happens that she wants to go to the washroom or borrow something, she will say, “Please sir may I go out?” or “Please madam, may I borrow a pen from Ashura?” When she is given permission to do what she has asked for, she would say, “Thank you sir” or “Thank you madam.” When she borrows something from her fellow pupil, she uses it and carefully returns it and says “Thank you very much for your kindness.” By behaving this way, she is liked by her teachers, her fellow pupils and everyone at home including her neighbours.’’

Imla hii ilikuwa na maswali matano, na miongoni mwa maswali hayo waliulizwa “What does Sheila do when she has a problem?”.

Wanafunzi waliojibu kwa usahihi swali hilo (She asks for help from her teachers) walikuwa asilimia 47.1 pekee, wengine walishindwa kabisa kujibu swali hilo.

Hii inaonesha kuwa uwezo wa wanafunzi kuelewa imla hadi wanapomaliza shule za msingi ni mdogo.

Swali jingine lilikuwa: “According to the story, who should children respect in the society?” Wanafunzi waliojibu kwa usahihi kuwa jibu ni “All the people” walikuwa asilimia 23.6 pekee.

Hii inaonesha kuwa wanafunzi wengi hawana uwezo wa kusikiliza, kuchambua wanachokisia na kukitathmini.

Lugha ya kufundishia nchini

Wadau mbalimbali wa elimu wanatofautiana mitazamo kuhusu lugha ya kufundishia. Wapo wanaoamini na kufundisha kuwa mwanafunzi anaelewa vizuri na kuwa mbunifu zaidi endapo atafundishwa kwa lugha anayoielewa vizuri.

Wengine wanafikiri kuwa kwa Tanzania lugha inayoeleweka vizuri kwa watoto ni Kiswahili kwa sababu ni lugha ya taifa.

Lakini wapo wanaopinga hilo kwa kueleza kuwa hata Kiswahili siyo lugha sahihi kufundishia endapo tunalenga kukuza maarifa ya watoto kwani kwa baadhi ya maeneo hata Kiswahili siyo lugha mama.

Wapo wanaotetea matumizi ya Kiingereza kufundishia. Utetezi unatokana na sababu kuwa vijana wengi wanakosa fursa ya kushindana katika soko la ajira kwa sababu ya kutokuwa na umilisi wa lugha ya Kiingereza.

Wanaamini kuwa Kiingereza bado ni lugha sahihi ya kutolea maarifa kwa sababu Kiswahili bado hakijajitosheleza kimsamiati.

Tunajifunza nini?

Ukirejea mifano yangu ya watoto watatu, Evance, Emily, na Tunu, utabaini kuwa katika nchi yetu wazazi wa Tunu ndiyo wenye nguvu zaidi katika kushawishi sera nchini kuliko wazazi wa Emily na Evance.

Matokeo yake hata uamuzi wa lugha ipi itumike unafanywa na wazazi wa Tunu kwa sababu kwao Kiingereza siyo tatizo. Watoto wao wanakimudu Kiingereza kwa sababu wanakitumia shuleni, nyumbani, mtaani wanakoishi .

Ndiyo maana nasisitiza kuwa suala la lugha limekuwa la kitabaka zaidi kwa sababu tabaka hili la Watanzania linaona Kiingereza kwao siyo tatizo. Wanadhani wale wanaoshindwa kukimudu Kiingereza ni kwa sababu ya uzembe wao. Wanashindwa kutambua kuwa asilimia 92 ya watoto wa Kitanzania hawawezi kuelewa kilichoandikwa kwenye insha ya Kiingereza na asilimia zaidi ya 60 hawawezi hata kufikia alama 21 kwenye mitihani wao.

Kuendelea kuamini kuwa Kiingereza ndio mwarobaini wa tatizo la elimu nchini ni kujidanganya wenyewe.

Tunazidi kutengeneza kundi kubwa la vijana watakaochukia kwenda shuleni kama ambavyo Dickson (siyo jina lake halisi) alivyoamua kuacha shule na kwenda kujifunza ufundi uashi kwa sababu aliona kuendelea kukaa shuleni ni kupoteza muda. Sasa hivi amekuwa fundi mzuri kabisa huko Songea na watu wanampenda kwa sababu chuo cha ufundi alichosoma kinalenga kukuza vipaji na wanafundisha kwa Kiswahili.

Tusipoteze ndoto za vijana wetu kwa kifungo cha lugha ya kujifunzia, badala yake wananchi wawe huru kuamua lugha wanayopenda kujifunzia na kufanyia mitihani.

Wale wanaoona Kiingereza siyo tatizo kwao waruhusiwe kujifunza kwa Kiingereza, na wale wanaoona Kiingereza ni mzigo kwao waachwe wajifunze na kutahiniwa kwa Kiswahili

Columnist: mwanachidigital