Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nabi ataja sifa za kocha mpya Yanga, ampa saluti GSM

Nabi X Kaze Ahadi Kocha Nabi na Kaze

Thu, 22 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tunaendelea na mfululizo wa mahojiano yetu na aliyekuwa Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ambaye kwanza amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo akisema wala hawatakiwi kuingiwa na ubaridi kwani mabosi waliomleta yeye bado wapo ambao anawaamini watashusha kocha muafaka kwa kikosi chao.

Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa sifa ya kwanza mrithi wake angependa awe mwenye ubora levo yake au hata wa juu yake ambapo itakuwa rahisi kuendeleza mafanikio ambayo ameyaacha kwa miaka miwili.

Lakini pili, anaweza kuwa na rekodi nzuri ya sasa katika kuchukua mataji ya Afrika ambapo Yanga itaangaliwa kwa umakini kwenye kurejea kwao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Pamoja na hayo, Nabi ameshauri Kocha ajaye apewe nguvu ya kusajili mashine za kuingia kwa nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, adhibiti kwa nguvu nidhamu ya baadhi ya mastaa nje na ndani ya Uwanja.

Kocha huyo ameongeza bosi mpya anapaswa kujiandaa kikamilifu kupambana na nguvu ya Simba na Azam ambao wameamua kuingia sokoni kwa nguvu kulipiza kisasi na kupunguza kasi ya Yanga msimu ujao.

“Nawaamini viongozi wa Yanga, kila unapopita unaona watu wanasikitika juu ya kuondoka kwangu lakini haitakiwi kuwa hivi nadhani Yanga bado ipo salama, Nabi akiondoka wale waliomleta Nabi bado wako hapa, hawa ndio watu muhimu zaidi unapokuwa na Ghalib (Said Mohamed), injinia (Hersi Said) na Arafat (Haji) sidhani kama lipo ambalo linaweza kuharibika kwa Yanga hii. “Nimefanya nao kazi kwa ukaribu ni watu ambao wakati wote wanatamani mafanikio kwa ajili ya klabu hii, swali la kocha yupi anafaa kuja kuchukua nafasi yangu nadhani ni yule ambaye atakuwa na ubora wa kuendeleza haya ambayo tumeyafanikisha.

“Kama wakimpata mtu wa ubora kama wangu au zaidi ambaye pia atakuja kuwa na muendelezo mzuri wa hapa tulipoishia hasa mashindano ya Afrika itakuwa ni hatua kubwa, sina mashaka na Yanga kuweza kuchukua mataji ya ndani lakini watu wengi wataiangalia huko Afrika wanafanya kipi baada ya kucheza fainali.”

“Nadhani pia kocha mpya hatakuwa na kazi ngumu kuanza kutengeneza kikosi msimu uliomalizika tulikuwa na safu nzuri ya ulinzi ambayo wengi watakuwepo pale kati pia watu kama kina Aucho (Khalid), Mudathir (Yahya) wapo kule mbele kama atabaki Fiston (Mayele) zitakuwa habari njema pamoja na wengine.

“Kama wachezaji watashika mapema falsafa zake ndani ya muda mfupi na kama wachezaji wapya watakaosajiliwa wataunganika haraka nadhani Yanga itaendeleza moto wake, sina wasiwasi kabisa na hii timu, mashabiki na wanachama watulie timu ipo mikono salama kabisa,” anasema.

Kocha huyo anaeleza ushirikiano alioupata na namna wadhamini chini ya mdhamini mkuu GSM walivyowezesha mambo;

“Kambi ilikuwa bora, wachezaji na sisi makocha tuliishi maisha sahihi ili kutoa ufanisi kwenye majukumu yetu. Kwa kambi ile ilitupa nguvu na kujiona tuna deni mbele yake na hata klabu kwa ujumla.”

KUPANGIWA TIMU

“Nisiseme uongo haijawahi kutokea kwangu, labda kutokana na maisha yangu wanajua hilo na wananijua isingeweza kutokea. Nilishawaambia (viongozi) wakati nafika tu kwamba kutakuwa na vikao vya kujadiliana na maendeleo ya timu. Pengine tunaweza kuulizana na nikawapa majibu,” anasema.

“Mimi sio kocha wa kuingiliwa majukumu. Sikuwahi kuona kitu cha namna hiyo na hakuwahi kutokea mtu kutaka kufanya kitu cha namna hiyo. Nisingeweza kukubaliana na hili.

DHIDI YA SIMBA

“Haikuwa rahisi kushinda mechi kubwa kama hizi. Pale tulipokuwa tunashinda zilikuwa nyakati bora. Kocha yeyoye ana furaha anaposhinda mechi ya watani.

“Ukweli ni kwamba presha inakuwa kubwa kabla ya mechi na baada ya mechi. Hapa watu wanapenda sana klabu hizi mbili. Binafsi huwa napenda mechi ngumu zinakusaidia kama kocha kuthibitisha ubora na kwa kuwa nilikuwa na kikosi kizuri haikuwa shida kubwa.”

MECHI KUBWA HALI

“Niwape siri moja katika maisha yangu ya soka ile siku ambayo tunakwenda kucheza mechi kubwa na ngumu huwa siwezi kula. Hii imeshindwa kuondoka. Huwa napenda kunywa maziwa au kunywa kahawa basi, labda baada ya mechi hata kama nimeshinda au nimepoteza hapo ndipo naweza kula. Sina maana kwamba labda presha inakuwa kubwa, hapana, ila ni utaratibu tu nimejijengea.”

“Hizi mechi kubwa tayari ni’shazoea. Mechi kubwa ya watani kwangu ilikuwa pale DR Congo wakati naifundisha Motema Pembe dhidi ya Vita Club. Unakuta uwanja ndani umejaa na nje kuna watu wanataka kuingia hapo nilikuwa na miaka 35 mpaka nakuja hapa tayari nilishazoea. Bahati mbaya sana kule DR Congo watu ni wakorofi sana hapa Tanzania ni wastaarabu.”

MPENI GSM MAUA YAKE

“Kwa muda ambao nimeishi hapa akili yangu inaniambia kwamba Yanga si lolote bila nguvu ya fedha za GSM. Ukiangalia gharama za usajili, kutunza timu kubwa kama hii kisha ikasafiri kokote inapotakiwa na kushinda hiki sio kitu rahisi. Klabu hii bado ilichelewa kupiga hatua kwa kujiendesha yenyewe. Nawapongeza viongozi wa klabu kwa hatua yao ya kuanza kuitafutia nguvu za kiuchumi.

“Kwa sasa bado watu wa Yanga wanatakiwa kumtunza Ghalib amefanya makubwa. Nadhani wanaweza kuona timu zingine kule DR Congo ligi imesimama muda mrefu kwa kukosekana fedha. Soka la sasa hakuna kitu utakifanya kwa urahisi na ukafanikiwa bila fedha,” anasema kocha huyo.

“Watu wana furaha kuona Yanga imecheza fainali ya Afrika ukiniuliza nitampongeza sana huyu mtu aliifanya kazi yangu kuwa rahisi, alikuwa chachu kubwa kwa wachezaji kujituma kwa kujiona wana deni kwake.”

SIRI YA ‘SUB’ ZAKE

“Sio kwamba kulikuwa na lolote la maajabu, hapana. Kocha mzuri ni yule anayejua kubadilisha mambo hasa pale anapoona kuna vitu haviendi sawa.

“Tulikuwa tunafanya kazi kupitia taaluma. Zipo nyakati tulikuwa tunashauriana pia na wasaidizi wangu kama Kaze (Cedric), Khalili (Ben Youssef), Helmy (Gueldich) na hata Milton (Nienov).

“Tunapoingia kwenye chumba cha mapumziko kikubwa tunaangalia tumechezaje kipindi cha kwanza. Kama mambo hayakuwa mazuri unawaambia wachezaji ukweli. Zipo nyakati wachezaji wanajiweka katika ugumu wa mechi wenyewe, kazi yako kama kocha ni kuwakumbusha kurudi kucheza kwa malengo.

“Kuna wakati ndio unaweza kuwa mkali wakati unaona mchezaji anaweza, halafu anacheza tofauti, lakini haina maana kwamba unamchukia.

“Kwenye ujumbe wangu wa kuwaaga wachezaji niliwaambia wanisamehe pale nilipokuwa mkali kwao kwa sababu moja tu - nilitaka wapambane tupate kilicho bora na si vinginevyo na baada ya ushindi sote tunakuwa pamoja. Kuusoma mchezo ni jukumu langu la msingi na kwa kuwa tulikuwa na wachezaji bora ambao wanaweza kubadilisha kitu mafanikio yalikuja.”

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: