Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nabi, Mgunda wakitoboa hapa freshi

Mgunda X Nabi.jpeg Juma Mgunda na Nasreddine Nabi

Sun, 4 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga usiku wa leo Jumapili wanashuka uwanjani kuikaribisha Tanzania Prisons katika mechi itakayopigwa Kwa Mkapa, lakini baada ya hapo kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi atakabiliwa na mtihani mzito ili kutoboa ndani ya mwezi huu na kumaliza mwaka 2022.

Sio Nabi tu, hata Kocha wa Simba, Juma Mgunda na Kally Ongala wa Azam nao wana vibarua kama hivyo vya kufanya kweli ili kuuaga mwaka 2022 kabla ya kuugeukia 2023, lakini fundi wa Jangwani akiwa na kibarua kizito zaidi kuliko wenzake na kama wote watavuka salama watazipa nafasi kubwa timu zao kwenye mbio za ubingwa.

Ipo hivi. Kocha Nabi ambaye leo saa 1:00 usiku ataiongoza Yanga kuivaa Tanzania Prisons katika moja kati ya mechi saba zinazomkabili ndani ya Desemba, ikiwamo ile ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Kurugenzi Simiyu itakayopiga Desemba 11, siku chache baada ya kumalizia kiporo chake na Namungo, mchezo utakaopigwa Jumatano ijayo mjini Lindi. Wakati Yanga ikikabiliwa na mechi hizo saba wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa Simba na Azam FC kila moja itacheza mechi tano.

Yanga ikimalizana leo na Prisons, itavaana na Namungo Desemba 7 kisha itacheza mechi ya ASFC na Desemba 17 itakuwa wenyeji dhidi ya Polisi Tanzania na siku tatu baadae itacheza na Coastal Union kabla ya siku ya Krismasi kuikabili wapinzani wa mbio za ubingwa wa Ligi, Azam na itafunga mwaka kwa kucheza na Mtibwa Sugar ugenini.

Kasheshe la Azam FC kwenye mechi zake tano litaanza kesho Jumatatu dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa ligi, kabla ya kuikabili Malimao FC katika mchezo wa FA utakaopigwa Desemba 9 na baada ya hapo Desemba 16 itakuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar.

Baadaye Azam itaifuata Geita Gold Desemba 21 na siku nne baadaye itawaalika Yanga ukiwa ni mchezo wake wa mwisho wa kufunga mwaka, hali inayomfanya Ongala aliyeiongoza timu hiyo katika mechi saba na kushinda zote ikiwa haijatoka sare wala kupoteza.

Katika mechi saba zilizopita, Kally aliyeichukua timu baada ya kutimuliwa kwa Kocha Denis Lavagne amepata clean sheets nne, huku timu hiyo ikifunga mabao 13 na kufungwa sita tu katika mechi hizo saba mfululizo za Ligi Kuu Bara inayomaliza duru la kwanza Jumatano ijayo.

Kwa upande wa Simba iliyokuwa uwanjani jana dhidi ya Coastal Union ratiba yake kwa Desemba inahusisha mechi ya ASFC ikivaana na Eagles ya Dar es Salaam Desemba 10 kisha siku nane baadaye itaifuata Geita Gold katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Simba ina mechi mbili tu kati ya tano nyumbani, kwani siku tatu baadaye Desemba 21 itakuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kuikabili KMC siku tano baadaye huku ikifunga mwaka kwa kuikaribisha Tanzania Prisons Desemba 30 kabla ya kuvuka bahari kwenda Zanzibar kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 inayaofikia tamati Januari 13.

Miamba hiyo inayofukuzana kwenye harakati za kuwania taji la ligi atakayechanga karata zake vizuri kwenye ratiba hiyo ndiye atakayejitengenezea mteremko mwaka mpya.

Kocha Nabi akizungumzia ratiba hiyo amekiri kumuathiri kwenye upatikanaji wa matokeo kutokana na wachezaji wake kucheza mechi mfululizo bila ya mapumziko.

“Ratiba imekuwa ngumu kwetu tuna michezo mingi mfululizo mwezi uliopita tumecheza mechi saba na mwezi huu pia tuna mechi saba sio rahisi kwetu lakini tunapambana kupata matokeo,” alisema na kuongeza;

“Tunatambua umuhimu wa kila mchezo tutapambana kupata matokeo na kutetea taji.”

Juma Mgunda alisema hawana njia nyingine ya kufanya zaidi ya kukamilisha ratiba kama walivyopangiwa lakini ni wazi wana kibarua kigumu kutokana na majeraha ya wachezaji wake.

“Ratiba tumeiona tutakamilisha wachezaji wanatakiwa kutumia kila nafasi kuipambania timu ili iweze kufikia malengo.”

Columnist: Mwanaspoti