Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Naam, Azam FC sasa imekubali kurudi njia kuu

Azam FCCC Azam FC

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatimaye Azam FC imekubali kushindana tena katika soka letu. Imekubali mchana kweupe. Inatia matumaini sasa.

Kwa miaka mingi Azam imekuwa ikiendeshwa kienyeji kama timu isiyokuwa na malengo. Haikuonyesha nia ya kuleta mapinduzi ya soka tena nchini. Ni jambo ambalo lilikuwa linafikirisha sana.

Lakini kwa msimu huu, hatimaye Bilionea wa timu hiyo, Yusuf Bakhresa amekubali yaishe. Ameirejesha timu katika ushindani wa kweli.

Kwanza, tuanze na hili la hapa majuzi tu la kumtimua Kocha Abdihamid Moallin. Ilishaonekana tangu mapema kwamba kocha huyo mwenye asili ya Somalia bado si mshindani mkubwa kwenye soka la Tanzania.

Ni kocha mzuri. Ni kocha mwenye elimu kubwa na uelewa mkubwa wa soka. Lakini bado Azam ilionekana kumzidi ukubwa.

Wachezaji wengi wamekuwa wakimuona kama kocha kijana mno. Maamuzi magumu aliyokuwa akifanya yalionekana kawaida. Wachezaji wakawa hawajitumi sana.

Pia, Moallin alikuwa anapambana sana kuonyesha ubora wake. Akawa na maelekezo mengi ndani na nje ya uwanja. Mwisho wa siku timu ikashindwa kucheza vizuri.

Ubaya zaidi ni kwamba Moallin alishindwa kuupata ubora wa baadhi ya wachezaji kwa pamoja. Mfano Idris Mbombo na Rodgers Kola walishindwa kutamba kwa pamoja.

Mbombo angecheza vizuri wakati Kola hayupo. Vipi kuhusu Prince Dube? Kila mtu anafahamu ubora wa Dube. Lakini wakati wa Moallin ubora wa Dube haukuonekana.

Pia, Azam ya Moallin ilikuwa na changamoto kubwa katika kujilinda. Msimu uliopita ilicheza mechi 12 mfululizo ikiruhusu mabao. Yaani hata kama ingeshinda, lakini ingeruhusu walau bao hata moja.

Hii sasa imekwenda hadi mwanzoni mwa msimu huu. Azam bado imekuwa na shida katika ulinzi. Ili ishinde mechi ni lazima ifunge mabao kuanzia mawili. Vipi ikishindwa?

Ni kweli Azam haina wachezaji wazuri wa kujilinda? Hapana. Wapo tena wazuri sana, lakini Moallin alishindwa kuwaunganisha pamoja. Hili lilikuwa ni tatizo kubwa zaidi.

Rafiki yangu mmoja aliniambia akitaka kuweka mkeka kwa Azam - anaweka nayo ifungwe angalau bao moja. Anasema ni mkeka ambao umekuwa na matunda mazuri. Huku ndiko ilipofikia Azam.

Pili, ni usajili ambao umekuwa ukifanywa pale Chamazi. Ulikuwa wa kawaida sana. Lakini msimu huu Azam imeamua kurudi njia kuu.

Imefanya usajili wa maana sana. Imechukua wachezaji wenye ushawishi mkubwa. Wachezaji bora kutoka maeneo mbalimbali.

Mfano mzuri yule Kipre Junior. Fundi haswa kutoka Ivory Coast. Alikuwa miongoni mwa wachezaji bora kwenye ligi ya kwao. Azam ikamshusha Chamazi. Pamoja na Yanga kumtaka Azam ndio ilimpata.

Yule Tape Edinho. Naye ni mahiri sana. Ni mchezaji wa daraja la juu. Ana utulivu akiwa na mpira. Anawapa hofu mabeki wa timu pinzani. Ni mchezaji wa timu kubwa. Naye yupo Chamazi.

Kwa wachezaji wa ndani baada ya muda mrefu hatimaye Azam imeweza kusajili wachezaji ambao walikuwa wakitakiwa na timu nyingine kubwa nchini.

Mfano yule Nathaniel Chilambo. Alikuwa akitakiwa na Simba, lakini Azam wakamchukua. Beki wa pembeni aliyekamilika. Anajua sana mpira na sasa yupo Chamazi. Inatia matumaini. Vipi kuhusu Abdul Selemani ‘Sopu’? Alitakiwa na Simba na Yanga. Timu zikapigana vikumbo baada ya fainali ya ASFC pale Arusha. Kesho yake akatambulishwa Chamazi.

Azam imelipa fedha nyingi kumpata Sopu mbele ya vigogo hao. Wasingeweza kufanya hivyo kwa miaka ya nyuma. Walisajili wachezaji ambao Simba na Yanga wala hazikuwataka sana.

Sasa unawezaje kushindana na Simba na Yanga kwa kusajili wachezaji wa daraja la kawaida? Ilikuwa ni ajabu na kweli. Ni kama kutegemea mazingaombwe.

Timu kubwa zinasajili wachezaji wakubwa kama Azam ilivyofanya msimu huu. Kila mtu anakubali kuwa sasa matajiri wa timu hiyo wamekubali kushindana tena.

Tatu, ni aina ya maandalizi ambayo Azam imefanya. Iliweka kambi pale Misri na kucheza mechi nyingi za maana. Ni kambi iliyokuwa ya kisasa zaidi kuliko hata ile ya Simba.

Wachezaji wakaandaliwa vizuri kwa msimu mpya. Hivi ndivyo timu kubwa zinafanya. Waliokuwa Kimbiji huko Kigamboni nao hawakupenda, ilitokea tu bahati mbaya. Walipanga kwenda Uturuki lakini wakakwama dakika za mwisho.

Nasikia pia Azam sasa imerudisha zile posho za wachezaji kushinda mechi. Kipindi cha nyuma zilikuwepo, lakini ndogo sana. Hazikuwasisimua wachezaji kupambana.

Yaani posho anayopata mchezaji wa Yanga au Simba kwa kushinda mechi ilikuwa mara tatu ama zaidi kuliko anayopata mchezaji wa Azam. Ni kituko kweli.

Sasa kuna haja gani ya kupambania timu ya tajiri kama unapewa posho kiduchu. Yaani wachezaji wanalipwa pesa za kawaida na kupewa posho magumashi. Watapambanaje? Haiwezekani. Ubaya ni kwamba walikuwa wanafahamu nini wanapata wachezaji wa Simba na Yanga ambao ndio washindani wao. Timu inakosa morali kabisa. Mwisho, sasa Azam imekubali kushindana Kitanzania. Yaani imekuwa na watu wanaofahamu soka letu na fitna zake.

Hii inaweza kuwasaidia sana kurejea katika ufalme wao. Muhimu wachezaji sasa wapambane kuonyesha ukubwa wao na kulipa deni kwa Yusuf Bakhresa aliyejitoa mhanga kuleta heshima kwa timu hiyo, baada ya kuishi kwa mazoea tangu ilipotwaa ubingwa wa Bara 2013-2014.

Columnist: Mwanaspoti