Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Na sasa Bale akacheze Gofu kwa furaha na amani tele

Gareth Bale Mls Gareth Bale

Sun, 15 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wanadamu tumeumbwa tofauti. Ni kweli. Najaribu kuwatafakari wachezaji wawili waliowahi kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia. Mmoja alianza kuvunja halafu mwingine akaja kuvunja ya mwenzake. Cristiano Ronaldo halafu Gareth Bale.

Alianza kuvunja Cristiano mwaka 2009 aliponunuliwa kwa dau la Pauni 80 milioni kutoka Manchester United kwenda Real Madrid halafu Wahispaniola hao wakarudi tena England mwaka 2013 kumchukua Gareth Bale kutoka Tottenham Hotspurs.

Miaka mingi baadaye Ronaldo akiwa na umri wa miaka 37 amekorofishana na watu wengi akiwemo kocha Erik Ten Hag akiwa na kiu kubwa ya kutaka kucheza soka katika kiwango cha juu. Hadi anaondoka Man United kwenda Riyadh - Saudi Arabia, Ronaldo naamini anaamini kwamba anastahili kucheza katika klabu kubwa Ulaya.

Halafu kuna Gareth Bale. Katika umri wa miaka 33 ametangaza kustaafu soka jumla. Ndio. Miaka 33 tu. Alikuwa nchini Marekani na hakuwa majeruhi. Ameamua tu kuachana na soka. Hakuna kitu ambacho kimenishangaza kutoka kwa Bale.

Sielewi tu kiini cha yeye kuwa tofauti na Ronaldo. Labda ni makuzi yao. Ronaldo akiwa mtoto alilazimika kulala na dada zake kwa sababu nyumba yao ilikuwa ya vyumba viwili. Chumba kimoja alilala mama na baba kingine alilazimika kulala na dada zake kwa sababu hakukuwa na chumba cha mwanaume huku akiwa ni mwanaume pekee nyumbani.

Majuzi Ronaldo akatupa stori nyingine ya msukumo wake wa maisha. Kwamba wakati wakiwa wanacheza timu ya vijana ya Sporting Lisbon walikuwa wanakwenda kuomba mabaki ya chakula cha mkate wenyewe nyama (Burger) kutoka kwa dada mmoja anayeitwa Edna ambaye alikuwa anafanya kazi katika mgahawa wa McDonald.

Labda hii ilimsukuma Ronaldo kuondoka katika umasikini. Labda hasira zake za maisha katika kazi yake zilianzia hapo. Upande wa pili kuna Gareth Bale. Sijawahi kusikia akisimulia upande mwingine wa maisha yake lakini yeye kama ilivyo kwa watoto wengine wa Kiingereza wamekulia katika maisha mema.

Haishangazi kuona Ronaldo akiwa bado na hasira. Katika umri wa miaka 37 na mwezi ujao anatimiza miaka 38, Ronaldo bado ana kiu. Bado ana kitu kinamsukuma. Lakini hili la Bale kustaafu halijanishangaza sana.

Alianza kupoteza kiu mapema tu akiwa Real Madrid. Sawa alikuwa na majeraha lakini katika ubora wake alikuwa bora pale Santiago Bernabeu akatengeneza utatu ulioitwa BBC yaani yeye, Karim Benzema pamoja na Cristiano Ronaldo. Bale pia alitwaa mataji kadhaa ya ubingwa wa Ulaya na La Liga.

Baada ya hapo alifurahia kukaa benchi. Picha zake wakati akiwa katika benchi la Real Madrid zilikuwa zinachekesha. Msimu wa 2019/2020 katika pambano dhidi ya Alaves Bale alionekana akiwa amejiziba sura yake huku akisinzia katika benchi. Hakujali chochote ambacho kilikuwa kinaendelea uwanjani.

Katika pambano dhidi ya Granada Bale alitengeneza viganja vyake vya mikono kama darubuni na kujifanya anatazama mechi kwa kupitia darubini. Hata hivyo mawazo yake hayakuwa uwanjani. Alikuwa anacheka tu bila ya kujali sana kilichokuwa kinaendelea uwanjani.

Katika pambano jingine dhidi ya Real Betis ambalo Real Madrid walichapwa mabao 2-0 nyumbani, Bale alionekana katika benchi akicheka pamoja na staa wa kimataifa wa Ujerumani, Toni Kroos. Kitendo hiki kiliwaudhi mashabiki wengi wa Real Madrid lakini hakuonekana kujali.

Katika pambano moja dhidi ya Real Sociedad Bale hakuwekwa hata benchi. Katika dakika ya 78 ya pambano hilo akaamua kuondoka zake uwanjani kwenda nyumbani kufanya mambo mengine. Kama ilivyo kawaida, watu wa Real Madrid walionekana kuchukizwa na kitendo chake hiki.

Lakini zaidi Bale alikuwa anawaudhi watu wa Madrid kutokana na tabia yake ya kuondoka Hispania na kurudi kwao Wales kucheza gofu mara kwa mara. Walichokuwa wanashangaa ni namna ambavyo alikuwa na ari kubwa wakati wa kuichezea timu ya taifa ya Wales kuliko Real Madrid.

Hata hivyo jambo hili hakutaka kulificha. Akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Wales aliwahi kuwa na bango lililoandika WALES, GOFU, MADRID. Akimaanisha kwamba vipaumbele vyake vilikuwa kuchezea Wales, halafu kucheza gofu huku kipaumbele chake cha mwisho kikiwa kuchezea Real Madrid. Hii ilisababisha mashabiki wa Real Madrid wamzomee.

Kuna wakati nilikuwa nadhani kwamba Bale alikuwa amechoshwa na Real Madrid tu lakini hata alivyokuja Tottenham kwa mkopo nadhani hali ilikuwa hiyo hiyo. Binafsi naamini kwamba Bale ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wanapoteza hamu ya kucheza soka wakiwa na umri mdogo au umri wa kawaida.

Ni wanasoka wachache ambao waliamua kustaafu soka wakiwa na umri huo. Bale amekwenda Marekani na hakuandamwa na majeraha yoyote yale. Kustaafu kwake akiwa na umri mdogo kulikuwa kunakuja kwa sababu tangu akiwa na Madrid ilionekana wazi kwamba kiu yake ya kucheza soka ilikuwa imekatika. Huwa inatokea. Ukichora picha ya nje unaweza kudhani Bale ni mkubwa kuliko Thiago Silva. Leo Silva ana miaka 38 lakini Bale ana miaka 33. Thiago bado anapiga kazi nzito pale Chelsea na haionekani kama atastaafu hivi karibuni.

Olivier Giroud ana miaka 35 lakini haionekani kama ni mzee kulikoi Bale. Messi ana miaka 35 lakini anaonekana kuwa kijana kuliko Bale. Nini kimemtokea Bale? Ni kukosa tu hamu ya kucheza. Huwa inawatokea wanasoka wachache na Bale ni mmoja kati ya mifano hiyo. Iliwahi pia kumtokea Eric Cantona ambaye aliamua kustaafu soka akiwa na miaka 30.

Columnist: Mwanaspoti