Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Ukishangaa ya Ronaldo utayaona ya Messi

Cristiano Ronaldo 4zr9r103wbw51g8s97mtlueti Cristiano Ronaldo

Sun, 13 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika mchezo wa chess kuna Garry Kasparov na Anatoly Karpov. Katika uhasama wa kisiasa kuna Marekani na Russia. Katika soka kulikuwa na Diego Maradona na Pele. Subiri kwanza, zama hizi kuna Cristiano Ronaldo CR 7 na Lionel Messi ‘La Pulga’.

Hawa wawili wa mwisho, Ronaldo na Messi bado tunawashuhudia. Lakini nakukumbusha kushuhudia mambo mawili ya mwisho baina yao. Kwanza nakukumbusha kwamba ubora wao unatoweka. Ulitazamia siku moja Ronaldo auzwe kutoka klabu moja kwenda nyingine kwa dau la Euro 25 milioni tu?

Ulitazamia siku moja Lionel Messi aondoke Barcelona bure kabisa. Bila kuuzwa. Yote haya yametokea kuashiria mwisho wao. Ndani ya uwanja pia wametoa viashiria vingi kwamba siku zao za kucheza soka katika viwango vya juu zimebakia kuwa chache. Hata msimu huu maajabu yao yamebaki kuwa machache na namba zao hazidanganyi.

Zaidi nakukumbusha mwisho mwingine unaotia kichefuchefu baina yao. Inawezekana hizi klabu ambazo wanachezea sasa hivi zikawa klabu kubwa za mwisho katika ligi kubwa Ulaya. Manchester United na PSG. Hata hivyo wanaonekana kumaliza na nuksi. Kinachotokea hakikupaswa kuwa.

Ronaldo anataabika na kiwango cha Manchester United, Messi anataabika na PSG. Katika matatizo yao ya siku za mwisho wameongezewa na utoto mwingi katika klabu hizi. Wanaelekea kushindwa kustarehe katika klabu zao ambazo zinaweza kuwa za mwisho katika kiwango cha juu.

Matatizo ya Ronaldo yanajulikana. Ilitazamiwa ashirikiane na wenzake kuifanya Man United igombee ubingwa wa England hasa alipotua Old Trafford akiwa ameambatana na Jadon Sancho na Raphael Varane. Kilichotokea ni kwamba waliowakuta walikuwa hoi. Labda Bruno Fernandes ndiye aliendelea kuwa yuleyule.

Aliokuja nao, Varane alimkuta Harry Maguire na wameshindwa kutengeneza kombinesheni yoyote tishio. Sancho alikuwa ovyo mpaka majuzi ambapo ameanza kuibuka tena. Siku zote alikuwa wapi? Hatujui. Tunachojua ni kwamba bei yake kutoka Borrusia Dortmund na kiwango chake vilikuwa vitu viwili tofauti.

Matokeo yake ni kwamba si tu Man United imeachwa pointi nyingi na kina Manchester City na Liverpool kufikia mwezi huu wa Machi, lakini pia Man United ina asilimia chache za kutinga Top Four. Wanasubiri miujiza tu Arsenal na Tottenham wakose.

Nadhani Ronaldo anajuta. Kwanini hakwenda Manchester City? Wangempumzisha zaidi. Si ajabu angefunga zaidi na mwishoni mwa msimu angeambulia chochote. Man United hii sio ile aliyoiacha ambayo ilikuwa na kiburi cha kumpatia ubingwa wa Ulaya. Ameondoka Man United ambayo mlinzi wa kushoto alikuwa ni Patrice Evra, leo anacheza Luke Shaw.

Tukihamia kwa rafiki yake, Messi. Unadhani kwanini aliitaka PSG au kwanini PSG walimtaka? Unadhani kwanini walitakana. Achana na ukweli kwamba PSG ilikuwa ni klabu yenye uwezo wa kifedha kando ya Manchester City ambayo ingemudu mshahara wa Messi, lakini pia walijua kwamba Messi angewaweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Hata yeye mwenyewe alifahamu kwamba huenda taji la mwisho kubwa la Ulaya angeweza kulipatia PSG akicheza sambamba na Kylian Mbappe, Neymar na Angel Di Maria. PSG nao walikuwa wanajua kwamba baada ya utoto wa kina Mbappe kwa misimu mitatu sasa ubingwa wa Ulaya huenda Messi angekuwa mkomavu wa kumalizia eneo dogo la ukomavu lililobaki.

Bado haikuwezekana. Jumatano usiku pale Santiago Bernabeu utoto umeendelea. Messi ameshindwa kuivusha PSG na pia tunaweza kusema PSG nayo imeshindwa kumvusha Messi. Kinachokera ni kwamba PSG walikuwa wanaongoza katika dakika 90 za kwanza pale Paris, Ufaransa.

Kinachokera zaidi ni kwamba hata mechi hii ya Jumatano usiku pale Madrid PSG walipata bao la kuongoza. Na kinachokera zaidi ya zaidi ni ukweli kwamba katika kipindi hiki cha kwanza PSG walifanikiwa kuichezea Real Madrid kama vile timu ya wakubwa ilikuwa inacheza na watoto wa shule ya msingi kwenye bustani ya nyumba ya mtu.

Kipindi cha pili kila kitu kiligeuka na hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Messi. Tayari akiwa na Barcelona waliwahi kufanya ujinga huo dhidi ya Roma pale Italia, kisha dhidi ya Liverpool pale Anfield. Unaongoza kwa amani mechi ya kwanza halafu matokeo yanaponyoka mkononi mechi ya marudiano.

Ni kweli kwamba Messi atatwaa ubingwa wa Ufaransa na PSG lakini hilo sio jambo ambalo litaamsha hisia kwa mashabiki wa PSG. Kwao sio jambo jipya. Ni sawa na Bayern Munich kuchukua ubingwa wa Ujerumani. Kwao kitu kipya zaidi itakuwa kuchukua ubingwa wa Ulaya ambao hawajawahi kuuchukua.

Kuanzia kwa mashabiki hadi matajiri, wachezaji kama Neymar, Mbappe na Messi walinunuliwa kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ulaya na si vinginevyo. Kwa mara nyingine tena wameukosa na maswali yatakuwa mengi juu ya vichwa hivi vitatu. Messi anaendelea kuzeeka na Juni mwaka huu atatimiza miaka 36.

Sawa, Neymar yupo katika ubora wake lakini Mbappe kuna asilimia tisini akaondoka mwishoni mwa msimu kwa uhamisho huru kwenda Real Madrid. Amegomea ofa nyingi za PSG ambazo zingeweza kumfanya kuwa bilionea kabla hajatimiza miaka 25. Ni wazi kwamba anataka kutimiza ndoto za kucheza Real Madrid. Wachezaji wengi wa kiwango chake huwa wanawaza hivyo.

Messi amejibu maswali mengi katika soka na sasa alikuwa anataka kulijibu hili la kuweza kutamba nje ya Barcelona au nje ya Ligi ya Kuu Hispania kwa kutwaa ubingwa na klabu nyingine. Jumatano usiku yeye na PSG kila mmoja alihitimisha ndoto za mwenzake msimu huu. Sijui msimu ujao utakuwaje

Kwa Messi na Ronaldo kitu kikubwa ambacho wanasubiri kutuaga mwaka huu wakiwa wanaelekea mwisho wao ni michuano ya Kombe la Dunia pale Qatar. Usijidanganye kwamba Man United wanaweza kufanya lolote katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata Ronaldo anafahamu hilo. Safari yao inaelekea tamati wakati huu ambapo Real Madrid, Bayern Munich, Liverpool, Manchester City bado wapo katika michuano.

Kitu kibaya zaidi kwa Ronaldo ni kwamba hata Ureno yake yenyewe italazimika kucheza Kombe ka Dunia kama tu wakishinda pambano lao la mtoano. Bado wapo katika mstari mwembamba ambao unaweza kuona Ronaldo akikosa michuano yenyewe.

Columnist: www.tanzaniaweb.live