Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Ten Hag ataamua nini kuhusu Ronaldo mabao?

Cristiano Ronaldo Cr 77 Cristiano Ronaldo

Sun, 1 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Swali ambalo jibu lake lina thamani ya Sh10 bilioni na zaidi. Erik Ten Hag ataamua nini kuhusu Cristiano Ronaldo? Kama juzi alikuwa katika kochi lake pale Amsterdam akitazama pambano la Manchester United dhidi ya Chelsea, basi atakuwa amekuna kichwa zaidi.

Alifunga tena kwa mara nyingine bao pekee la Man United. Bahati ni kwamba lilikuwa bao la kusawazisha na United haikupoteza mechi. Hadi lini Ronaldo ataendelea kufunga? Inaonekana amebakiwa na mabao mengi mguuni kuliko hata baadhi ya wachezaji wenye umri wa miaka 22. Inaonekana hivyo. Anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji waliogusa mpira mara chache zaidi juzi usiku, lakini mwishowe alisalimiana na Edouard Mendy na kuuweka mpira nyuma ya nyavu zake na kufuta bao la uongozi la Marcos Alonso ambalo lilionekana lingekuwa la ushindi.

Siku chache kabla ya hapo itakuwa alikuwa amekuna kichwa zaidi alipomuona Ronaldo akiutokea mpira katikati ya Gabriel na Nuno Tavares na kufunga kiurahisi bao la kufutia machozi dhidi ya Arsenal pale Emirates. Ten Hag ataamua nini kuhusu Ronaldo. Ameitwa klabuni kwa ajili ya mwanzo mpya. Ronaldo katika umri wa miaka 37 anaweza kuhusika katika mwanzo mpya? Kuna mambo mawili hapa. Kwanza itaanzia kwa Ronaldo mwenyewe. Anataka nini? Anataka kucheza michuano ya Europa kila Alhamisi? Sina uhakika sana.

Nadhani hajawahi kucheza michuano hii kwa miaka 20 iliyopita. Mchezaji mwenye hadhi yake acheze Europa, huku rafiki yake Lionel Messi akicheza mechi za usiku wa Ligi ya Mabingwa? Sidhani kama mchezaji mshindani kama Ronaldo anaweza kukubali jambo hili. Anaweza kuwaambia Man United kwaheri ndani ya wiki mbili au tatu zijazo. Nahisi hivyo.

Lakini kwa upande wa Ten Hag nadhani mtihani wake wa kwanza ni Ronaldo. Ataachana na Ronaldo au atamuweka katika mipango yake? Ni swali gumu kidogo. Kocha kama yeye atataka mwanzo mpya na vijana wapya wenye kasi na damu changa. Ni mradi wa zaidi ya miaka mi-nne. Miguu ya Ronaldo kwa sasa haiwezi kukaba kwa nguvu kuanzia juu. Anachoweza kukupa ni mabao tu. Tatizo la makocha wa kisasa ni kwamba wanahitaji mambo mengi kutoka kwa mchezaji zaidi ya mabao. Mojawapo ni hili hapa la kutaka mchezaji akabe kuanzia juu, arudi katikati, arudi nyuma. Ndivyo Ajax yake inavyocheza na ndicho kitu kilichompatia sifa.

Ten Hag timu zake zinacheza kwa umoja mkubwa katika maeneo mengi. Ni tofauti na Man United tunayoiona kwa sasa. Lakini ndivyo ambavyo makocha wakubwa wanaotamba sasa hivi kina Pep Guardiola na Jurgen Klopp wanavyofanya. Ndicho ambacho Mikel Arteta anajaribu kufanya pale Arsenal na walau wanaonekana kuinyemelea Top Four.

Ten Hag atajaribu kufanya hivi katika miguu iliyochoka ya Ronaldo? Sina uhakika. Ronaldo anaweza kumpa mabao kama anavyoendelea kufanya, lakini hawezi kumpa pumzi kubwa katika staili yake ya mchezo. Anaweza kuachana naye. Anaweza kuwa mchezaji wa akiba? Bado sidhani. Ronaldo anajisikia.

Ronaldo anaupenda mchezo wenyewe. Ni shujaa. Sidhani kama atakubali kuwa katika timu ambayo itamfanya awe chaguo la pili au la tatu. Anaweza kuhisi kuna mahala anaweza kwenda na kuendelea kufunga mabao. Hawezi kukubali kukalia benchi Old Trafford. Ten Hag atachukua maamuzi kuhusu Ronaldo. Vyovyote ilivyo bado mashabiki wataamini maamuzi yake. Hata kama akiamua kuachana na Ronaldo, lakini mashabiki wataamini katika maamuzi yake kwa sababu wamechoshwa na kile wanachokiona kuhusu timu yao kila siku.

Sawa wana Ronaldo na anafunga, lakini wamechoshwa kuona wananyanyaswa kila siku na wapinzani wao. Iwe Old Trafford au kwingineko Man United ya leo ni timu inayofukuza vivuli vya wapinzani. Inafungwa na timu zinazofungwa kila siku kama Everton. Hata pambano dhidi ya Norwich kwao ni gumu.

Mashabiki watamuelewa Ten Hag katika mwanzo wake mpya hata kama ataachana na Ronaldo ilimradi tu awake moyo katika mwanzo wake mpya. Sio Ronaldo tu kuna wengi ambao wataondoka na itaeleweka kwa mashabiki wa Man United. Kwa haraka haraka Paul Pogba anaondoka. Nemanja Matic amejitoa mwenyewe. Juan Mata ni muda wa kuanza kuwa kocha. Lakini sidhani kama kina Marcus Rashford wataweza kufufuka upya. Mwanzo mpya ni kuachana na mchezaji kama yeye pia. Amekulia klabuni na alikuwa na mwanzo mzuri Old Trafford, lakini sasa anacheza kama analazimishwa. Kina Harry Maguire ni wachezaji ambao tunasubiri kuona. Je, alikuwa anaangushwa na timu au alikuwa anajiangusha mwenyewe? Ten Hag atachukua maamuzi yake mwenyewe na sidhani kama maamuzi yake yatapelekeshwa na dau kubwa ambalo Maguire alinunuliwa kutoka Leicester City miaka michache iliyopita.

Rafiki yangu Edinson Cavani najua ataondoka zake, lakini kuna mtu mwingine kutoka Amerika Kusini ambaye hata kama asipoondoka katika dirisha hili bado anaweza kuondoka katika dirisha kubwa la mwakani. Fred. United haijawahi kuwa na uhakika naye. Hata hivyo, swali la msingi zaidi ni hili la Ronaldo. Ten Hag atalazimika kulijibu katika wiki yake ya kwanza atakapotua na mabegi yake Old Trafford. Ataamua nini kuhusu Ronaldo? Wote tunasubiri kwa hamu. Ronaldo mwenyewe ndiye anasababisha tunashindwa kujijibu. Licha ya miguu yake kuchoka, lakini yeye ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi Old Trafford. Bila ya mabao yake si ajabu Man United ingekuwa inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu. Namba huwa hazidanganyi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz